KAMATI Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeiagiza Serikali kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa na kuhakikisha mafuta yote yanayoingia nchini yana ubora unaotakiwa.
Pia Kamati hiyo imeitaka Serikali kutafuta suluhu ya uchakachuaji wa mafuta, kwani uwezo wa kufanya hivyo inao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema Kamati Kuu ya Chama hicho iliyokutana juzi pamoja na kujadili mambo mbalimbali ya chama, haijaridhishwa na kiwango cha bei ya mafuta ya taa.
Alisema nishati hiyo ndiyo inayotumiwa na wananchi wengi wa kipato cha chini nchini, na kwamba kupandishwa bei kwa kisingizio cha kupunguza uchakachuaji, si sahihi.
Aliongeza kwamba, kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta hayo Serikali inapaswa kukaa na kutafuta njia zitakazoshusha bei hiyo na kuvitaka vyombo husika kuhakikisha ubora wa mafuta yanayoingia nchini.
“Tunaitaka Serikali itafute njia ya kushusha bei ya matufa ya taa na pia kutafuta suluhisho la uchakachuaji na si kupandisha bei,“ alisema Nape.
Aidha, alisema suala la umeme ni nyeti na kwa hali ilivyo sasa si nzuri na kuishauri Serikali kuja na njia za kunusuru hali hiyo.
“Athari ya kukosekana kwa umeme nchini ni kubwa, hivyo Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, itumie muda iliopewa kurekebisha bajeti yao vizuri na kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hili na pia kuja na majibu ya suluhu ya tatizo hili,” alisema Nape
Aliongeza kwamba madhara yanayoipata nchi na mtu mmoja mmoja ni makubwa na inasikitisha kwa hali ilivyo na kwamba lazima Serikali ije na suluhu ya jambo hilo.
Aidha, Nape alisema Kamati Kuu pia ilijadili masuala yanayogusa wananchi likiwamo la migogoro ya ardhi, madini bei ya pamba na kuagiza Serikali iyashughulikie kabla migogoro hiyo haijawa mikubwa.
Hivi sasa mafuta ya taa yanauzwa bei kubwa kuliko dizeli na petroli ambapo katika baadhi ya vituo bei elekezi ni Sh 1,940 na kikomo ni Sh 2,086 kwa Dar es Salaam wakati kigoma elekezi ni Sh 2,117 na kikomo ni Sh 2,334 kwa lita.
Kwa hali hiyo hiyo, bei elekezi ya dizeli kwa Dar es Salaam ni Sh 1,939 na kikomo ni Sh 2084 huku kwa Kigoma elekezi ni Sh 2170 na kikomo ni Sh 2,333.
Hatua ya kupandishwa kwa bei hiyo ya mafuta ilifikiwa bungeni katika Bajeti ya Mwaka huu wa Fedha, kwa lengo la kuhakikisha kwamba kodi ya mafuta ya taa haizidiani sana na ya dizeli na hivyo kuondokana na uchakachuaji.
Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya uchumi wanadai kwamba wachakachuaji wanafahamika na hivyo ni wajibu wa Serikali kuwabana kuliko kumwumiza Mtanzania masikini anayeishi kwa kutegemea mafuta ya taa.
Lakini pia wanasema tatizo linalosababisha yote haya ni kwamba mafuta yote yanaagizwa kutoka nje ya nchi ambako bei inatoka huko huko lakini pia kodi ya mafuta nchini ni kubwa.
Wanatoa mfano kwamba lita moja ya mafuta ya taa huitozwa kodi ya Sh 400.30, ya petrioli ni Sh 534 na dizeli ni Sh 415.
Wachambuzi hao wanasema pia kwamba hata thamani ya sarafu kulinganisha na dola ya Marekani ni tatizo, “angalia Machi kiwango kilikuwa dola moja kwa Sh 1,400 leo ni Sh 1,600,” alisema mchambuzi ambaye hakuta kutajwa jina.
Asilimia 14 tu ya Watanzania ndio wanaotumia umeme huku asilimia iliyosalia ambayo wengi ni wananchi masikini waishio vijijini, wanatumia mafuta ya taa kumulikia na hata kupikia, hivyo bei ya nishati hiyo inapopanda inawaumiza.
Wakati huo huo, habari zilizopatikana jana jioni Dodoma, zilisema leo Serikali inatarajiwa kutangaza bei mpya ya mafuta nchini, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kukokotoa kwa kuzingatia maoni ya wadau mbalimbali
No comments:
Post a Comment