KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeishauri Serikali kusitisha moja kwa moja uchimbaji wa madini ya urani hadi hapo itakapokuwa imewaelimisha wananchi.
Aidha, kwa maeneo ya wilaya za Bahi mkoani Dodoma na Manyoni katika Mkoa wa Singida, kituo kimeshauri uchimbaji wa madini hayo kusitishwa kabisa kutokana na kuwa katikati ya makazi ya watu.
Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Francis Kiwanga alisema hayo jana Dar es Salaam katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi wa Sera na Maboresho, Harold Sungusia wakati akitoa tamko la LHRC kuhusu uchimbaji wa madini hayo ambayo utekelezaji wake haujaanza.
Alisema tamko hilo linatokana na utafiti uliofanywa na wataalamu wa kituo hicho katika
maeneo ya Bahi, Manyoni na Namtumbo mkoani Ruvuma na kugundua mambo mbalimbali ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kabla utekelezaji wa uchimbaji wa madini katika maeneo hayo.
“Miongoni mwa yaliyogunduliwa ni pamoja na wananchi kutoelimishwa na kuhadharishwa kuhusu taadhira na athari za madini hayo ya urani kwa afya zao, mifugo yao, mazao yao na mazingira kwa ujumla,” alisema Kiwanga.
Hata hivyo, alisema wananchi hawajashirikishwa katika kazi ya utafiti inayoendelea katika maeneo hayo na hata hatma ya maisha yao haijajulikana.
Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Aloyce Tesha alisema madini ya urani yakiwa katika hali yake ya kawaida bila kuchakachuliwa hayana madhara. Hata hivyo alisema kwa sasa hakuna shughuli za uchimbaji, bali utafiti ambao ni muhimu kwa ajili ya kujua kiasi cha madini kilichopo na ubora wake.
No comments:
Post a Comment