Friday, August 19, 2011

Mkurugenzi Wanyamapori asimamishwa kazi

MKURUGENZI wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid Mbangwa amesimamishwa kazi kuanzia jana kupisha uchunguzi kuhusu wanyamapori 120 na ndege 16 waliotoroshwa Novemba mwaka jana kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amelieleza Bunge kuwa, Mbangwa amesimamishwa kazi na watumishi wengine wawili wa Wizara hiyo lakini hakuwataja ili kutoathiri uchunguzi.

Maige amewaeleza wabunge kuwa, Mbangwa ataendelea kulipwa, na wote waliohusika kutorosha wanyama na ndege hao watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kwa mujibu wa Maige, Wizara hiyo inashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza utoroshaji huo, na kwamba, watu sita tayari wameshitakiwa katika Mahakama mjini Moshi kwa tuhuma za kuhujumu uchumi.

Waziri Maige amewaeleza wabunge kuwa, ndege ya jeshi la Qatar iliyowatorosha wanyama na ndege hao ilikuja nchini kihalali kwa kuwa ilikuwa na kibali cha kumleta mwanadiplomasia nchini kwa safari binafsi.

Amesema, ndege hiyo ilionekana kwenye vyombo vya usalama, lakini haikukaguliwa wakati inaondoka na hadi sasa haijulikani wanyama na ndege hao walipelekwa wapi.

Maige amewaeleza wabunge kuwa, biashara ya kukamata wanyama na kuwasafirisha nje ya nchi ni halali, kampuni 180 zina leseni, na kwamba, waliokamata maliasili zilizotoroshwa walikuwa na vibali vyote muhimu vilivyowaruhusu kukamata na kumiliki wanyama hao lakini ukaguzi ulipofanywa hawakuonekana.

Amesema, Wizara inashirikiana na vyombo vya ulinzi na upelelezi vya kimataifa likiwemo shirika la Interpol ili kufahamu nyaraka zilizotumika kuwasafirisha wanyamapori na ndege, walipelekwa wapi na wapo kwa nani hivi sasa.

Ameomba wabunge wenye taarifa kuhusu utoroshaji huo wampe taarifa na anaamini wanamuamini, wakishindwa wawape mawaziri wengine, na endapo taarifa hizo hazitatumika ipasavyo wamuwajibishe bungeni.

Maige amesema bungeni kuwa, kutoroshwa kwa ndege na wanyama hao kumemkasirisha kuliko jambo lingine lolote katika utumishi wake wa umma.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira jana ilihoji ilichodai kuwa ni kigugumizi cha Serikali kuhakikisha kuwa wanyamapori 116 hai na ndege 16 walioibwa nchini Novemba 24 mwaka jana wanarudishwa nchini.

Kamati hiyo ililieleza Bunge kuwa, wanyama hao wakiwemo twiga wanne na ndege hai ambao wana jumla ya thamani ya Sh. 170,570,500 waliibwa kwa kutumia ndege ya jeshi la Qatar kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

Bunge lilielezwa kuwa, wanyamapori walioibwa wana thamani ya Sh. 163,732,500.00/- na ndege hai wana thamani ya Sh. 6,838,000.00/-

Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli alisema, hadi jana kamati ilikuwa haifahamu wanyama na ndege hao walipelekwa wapi na kama bado wapo hai.

Aliyasema hayo wakati anasoma taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2010/2011 pamoja na maoni ya kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2011/2012.

Lembeli alisema, uharamia huo ulifanywa na Watanzania na kwamba, kigugumizi cha Serikali kushughulikia suala hilo kimeisikitisha Kamati kwa kuwa rasilimali iliyoibwa ni adimu na haijulikani itarudishwa lini nchini.

“Kwa hakika kuna dalili kubwa ya uzembe na kulindana ndani ya Wizara hii na ndiyo maana kumekuwa na kigugumizi katika kushughulikia ushauri wa kamati. Ukweli wa mashaka haya unajidhihirisha katika zoezi zima lililofanyika hivi karibuni ndani ya idara husika la kuhamisha maafisa” alisema Lembeli.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amelieleza Bunge kuwa, wanyama hai wa aina mbalimbali 120 na ndege hai 16 walitoroshwa Novemba 26 mwaka 2010 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

No comments: