-Luhanjo, Ngeleja ‘kubebeshwa msalaba?”
-Serikalini sasa kwafukuta kila eneo
BAADA ya Bunge kuunda Kamati Teule ya kuchunguza sakata la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, hali sasa si shwari serikalini na Rais Jakaya Kikwete, anaelezwa kujiandaa kufanya maamuzi mazito kusafisha hali ya hewa ya kisiasa inayoelekea kuvuruga mkakati wake kukisafisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mtindo maarufu sasa wa ‘kujivua gamba’.
Habari za ndani ya Serikali zimethibitisha kwamba kwa sasa kuna mtikisiko mkubwa uliotokana na mkanganyiko uliosababishwa na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza kurudishwa kazini kwa Jairo aliyekuwa likizo akisubiri kuchunguzwa, uamuzi ambao ulitenguliwa na Rais Kikwete.
Sakata hilo la Jairo sasa limewagusa kwa namna isiyo nzuri viongozi wote wa juu wa Serikali, akiwamo Rais Kikwete mwenyewe, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, (aliyetamani hata kutimuliwa kabisa kwa Jairo), Luhanjo (aliyemrudisha kazini) na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyempokea wizarani kwa mbwembwe, akiruhusu hata wafanyakazi wengine kusukuma gari lake.
Kuguswa kwa waandamizi hao wa juu serikalini, kunatishiwa zaidi na hatua ya Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza sakata hilo, jambo ambalo si ishara nzuri kwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Bunge kuchunguza mtendaji wa juu wa Ofisi ya Rais Ikulu, ambaye ni Katibu Mkuu Kiongozi.
Habari za ndani ya Serikali zinaeleza kwamba uamuzi wa kutengua uamuzi huo, saa chache baada ya kuwa umetangazwa na Luhanjo, ulitokana na Rais Kikwete kukwerwa na uamuzi huo ambao imethibitika kwamba ulifanyika katika mazingira tata.
Ikulu ililazimika kutoa taarifa ya ufafanuzi baada ya baadhi ya vyombo vya habari kutafsiri kwamba kulikuwapo na ugeugeu kwa ofisi moja (Ikulu) kutoa maamuzi yanayokinzana; yaani uamuzi wa kumrudisha Jairo kazini kwa mbwembwe na uamuzi wa kutaka aendelee kuwa likizo akisubiri hatima yake.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Agosti 26, 2011 kwa vyombo vya habari ikionyesha kuwa na uharaka (urgent) ilieleza hakukuwa na mkanganyiko wowote kati ya Rais Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi wake, Luhanjo, kwa maelezo kwamba wote walikua sahihi kwa mamlaka waliyonayo kisheria.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ikiwa na baadhi ya meneno yaliyowekewa msisitizo kwa herufi kubwa ilieleza;
“Julai 21, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi Phillemon Luhanjo, akitumia madaraka yake ya Mamlaka ya Nidhamu ya Watumishi wa Umma, alitangaza hatua ya kumpa likizo ya malipo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishatai na Madini, David Kitundu Jairo, ili kupisha uchunguzi aliokuwa ameuagiza ufanyike dhidi yake.
“Luhanjo alichukua hatua ya kumsimamisha Jairo kufuatia tuhuma zilizokuwa zimeelekezwa dhidi yake (kwake) na baadhi ya wabunge wakati wa mjadala kuhusu Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2011/12 katika kikao cha Bunge kilichofanyika tarehe 18 Julai, 2011.
“Katika mjadala huo, baadhi ya wabunge walihoji uhalali wa Wizara kuomba michango ya fedha kutoka kwenye taasisi zilizoko chini ya usimamizi wake ili kusaidia Bajeti ya Wizara hiyo kupita kwa urahisi.
“Kufuatia hatua hiyo ya kumsimamisha kazi Bw. Jairo, Katibu Mkuu Kiongozi alimwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kufanya ukaguzi maalumu na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma hizo.
“Tarehe 9 Agosti, 2011, Utouh aliwasilisha Ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, na tarehe 23, Agosti, 2011, Katibu Mkuu Kiongozi akiambatana na Utouh, alitangaza mbele ya waandishi wa habari matokeo ya ukaguzi huo maalumu na uchunguzi wa awali juu ya tuhuma dhidi ya Jairo,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika Ripoti yake mbele ya waandishi wa habari, taarifa ya Ikulu ilinukuu taarifa ya Utouh ikieleza: “Ukaguzi maalum haukuthibitisha kuwapo kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini David Kitundu Jairo.”
Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kwamba Katibu Mkuu Kiongozi alitumia taarifa ya CAG kuwaambia waandishi wa habari kwamba: “Matokeo ya uchunguzi huo ni kwamba tuhuma zilizotolewa Bungeni tarehe 18 Julai, 2011, hazikuweza kuthibitika.”
Akitumia vifungu vya sheria, Luhanjo amenukuliwa na Ikulu akisema; ”mimi kama Mamlaka ya Nidhamu ya Katibu Mkuu, Nishati na Madini, David Kitundu Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma (notice) na Hati ya Mashitaka kwa sababu Bwana David Kitundu Jairo, hajapatikana na kosa la kinidhamu (disciplinary offence) kwa mujibu wa Taarifa ya Ukaguzi Maalumu.”
Luhanjo alinukuliwa akisema kwamba kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Sheria Na. 8 ya Utumishi Umma ya Mwaka 2002 na kanuni zake za Mwaka 2003, aliamuru Jairo aendele kazini siku ya Jumatano Agosti 24, 2011.
Katika ufafanuzi wake, Ikulu ilieleza kwamba, “baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi ya CAG na uamuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi kuhusu suala hilo asubuhi ya tarehe 25 Agosti, 2011, Rais Kikwete, aliamua kuwa Jairo asirudi kazini mpaka kwanza yeye Rais atapoamua namna gani ya kurudi kazini, lini na wapi.
“Katibu Mkuu Kiongozi alifikisha uamuzi huo wa Rais kwa David Jairo ambaye mapema asubuhi ya siku hiyo alikuwa ameripoti kazini. Ndugu Jairo alitii uamuzi huo wa Rais. Tunapenda kusisitiza kuwa Rais hajawa kigeugeu kwa sababu alifanya uamuzi mmoja tu baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.”
Taarifa ya Ikulu ilionyesha pia kwamba uamuzi huo aliufanya kabla ya Bunge kulizungumzia suala hilo na hivyo uamuzi huo wa Rais haukutokana na shinikizo la Bunge na kwamba pamoja na kumweleza Katibu Mkuu Kiongozi, Rais pia alimfahamisha Waziri Mkuu kuhusu uamuzi wake huo asubuhi hiyo ya Agosti 25, 2011.
Maelezo hayo ya Ikulu yanaashiria kwamba kwamba uamuzi wa Luhanjo umechokoza mambo mengi yanayomhusu mtendaji huyo wa juu serikalini, zikiwamo taarifa zinazohusu muda wake wa kustaafu na maamuzi na mahusiano yake kikazi na watendaji wengine katika wizara alizowahi kufanya kazi kabla ya kuhamishiwa Ikulu.
Luhanjo amewahi kuwa Katibu Mkuu katika Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na WIzara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuhamishiwa Ikulu kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, nafasi ambayo inaelezwa kwamba alitarajiwa kuwa amestaafu kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010.
Baadhi ya wachambuzi na asasi za kiraia na vyombo vya habari vimekuwa vikitoa tafsiri mbaya kwa Serikali kuhusu suala hilo la Jairo vikianzia na kauli ya Pinda Bungeni kwamba angekuwa na mamlaka kisheria angemchukulia hatua Jairo siku hiyohiyo ya tuhuma, kabla ya Serikali kumpa likizo na kutokea kwa utata baada ya taarifa ya CAG.
Miongoni mwa waliotoa matamko waziwazi ni Mbunge wa zamani wa Bumbuli na mtendaji mwandamizi mstaafu serikalini William Shellukindo, ambaye alisema moja kwa moja kwamba Luhanjo ameshindwa kumsaidia Rais Kikwete.
Shelukindo ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Rais Ikulu (cheo ambacho sasa kinaitwa Katibu Mkuu Kiongozi) katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi, amenukuliwa na gazeti la Mwananchi Jumapili iliyopita akisema Luhanjo ameonyesha utovu wa nidhamu na ameidhalilisha Ikulu kutangaza kumrejesha Jairo bila kupitia bungeni.
Soma zaidi
No comments:
Post a Comment