Wednesday, March 10, 2010

Mrema ataka alipwe Sh bilioni 1 na Sitta

MWENYEKITI wa Chama chaTanzania Labour (TLP) amemtaka Spika wa Bunge, Samuel Sitta, amlipe fidia ya Sh bilioni moja ndani ya wiki moja kuanzia juzi, vinginevyo atamfungulia kesi ya madai Mahakama Kuu kwa kile anachodai kwamba amedhalilishwa.

Mrema amempa Sitta taarifa ya kusudio la kumfungulia kesi ya madai mahakamani endapo hatatimiza masharti ya kumfidia na kumwomba radhi.

Katika barua aliyoiandika juzi, Mrema amempa Sitta siku saba hadi Jumatatu ijayo, kutimiza masharti yake kabla ya kumfikisha mahakamani.

“Naomba kukufahamisha, kwamba ninakusudia kukufungulia kesi ya madai Mahakama Kuu ya Tanzania kutokana na wewe Mheshimiwa Sitta kunitukana, kunikashifu, kunivunjia heshima na kunidhalilisha kupitia magazetini,” inasema sehemu ya barua ya Mrema kwa Spika Sitta.

Barua hiyo inaendelea: “Vinginevyo, uniombe radhi kupitia magazeti yale yale na kwa uzito ule ule katika kipindi cha siku saba tangu utakapopokea barua hii; unilipe fidia ya Sh bilioni moja.”

Akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Pili, Mrema alikuwa na kawaida ya kutoa siku saba kwa wahusika kutekeleza maagizo yake kabla hajachukua hatua.

Alinukuu gazeti la Mwananchi la Machi 5 mwaka huu, ambalo lilimkariri Sitta akimwita Mrema mhuni na aliyepitwa na wakati, aliyefilisika kisiasa na kifedha na kwamba sasa anatafuta njia ya kujinasua kutoka hali hiyo.

Mrema anadai kwamba kauli hizo, akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, zimesababisha wanachama wapatao 500,000 nchini wakose imani naye. Na pia kauli hizo anadai zimemvunjia heshima aliyojijengea kutokana na utumishi wake wa zaidi ya miaka 30 akiwa Ofisa Usalama wa Taifa, Mbunge, Waziri na Naibu Waziri Mkuu.

Alisisitiza: “Kauli zako zimeniathiri, kwa sababu nimeshajitangaza kugombea ubunge wa jimbo la Vunjo.

Hivyo kauli zako zinaweza kutumiwa na wapinzani wangu dhidi yangu.” Akizungumza na gazeti hili, Mrema alisema anaendelea na mchakato wa kuandaa mwanasheria atakayesimamia shauri lake.

Alisema Mahakama pekee ndiyo itakayotoa tafsiri halali kama Sitta alimdhalilisha au la. Gazeti hili lilimtafuta Spika Sitta kwa simu kwa lengo la kumuuliza kama amepokea taarifa ya Mrema, lakini simu yake haikupatikana.

Mazingira ya kutofautiana kati ya Spika Sitta na Mrema yamekuwa yakidhihirika kupitia vyombo vya habari.

Mrema aliitisha mkutano wa waandishi wa habari hivi karibuni na kudai kwamba Sitta ni mchochezi, mjenga makundi na mtu anayehatarisha amani na usalama wa nchi, kauli ambayo inadaiwa pia Spika aliijibu kupitia Mwananchi.

2 comments:

Anonymous said...

Mrema siku zote ni mtibuaji. bado ni ccm iliyomafichoni ili kuvuruga watu wanaotafuta kuponya nchi. Yeye mrema ahamie ccm. Kwani ya Sitta na CCM yanamhusu nini? Kwanza yeye ashitakiwe kwa kusumbua wapinzani na kuwavuruga.

Anonymous said...

Lyatonga sasa anaelekea kubaya, hiyo fidia kwa haraka haraka nadhani anataka kumalizia shida zake maana naambiwa kipindi hiki ana matatizo sana ya kifedha, Sitta kuwa makini huyo jamaa sasa hivi hafanyi yote hayo kwa kupenda bali dhiki ndio inamlazimu hivyo