RAIS Jakaya Kikwete amesaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, katika moja ya matukio ya nadra kwa mkuu wa nchi kusaini sheria kwa mbwembwe tofauti na mazoea ya kusainiwa kimyakimya na kisha kuwekwa katika Gazeti la Serikali.
Februari 25 mwaka huu, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mwanza, Rais Kikwete aliahidi kuisaini sheria hiyo kwa mbwembwe kutokana na umuhimu wake, jambo lililothibitishwa na shughuli ya jana Ikulu.
Shughuli hiyo ilitangazwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni nchini na ilihudhuriwa na waalikwa mbalimbali wakiwamo mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi wa nje, viongozi wa vyama vya siasa, majaji na waalikwa wengine.
Mbali na hao walikuwapo pia, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Lewis Makame, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah.
Miongoni mwa watu maarufu waliokosekana katika shughuli ya jana ni Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta ambaye anaongoza moja ya mihimili mitatu ya Dola.
Aidha, wakati Rais Kikwete akisaini sheria hiyo saa 5.55 asubuhi, alikuwa amezungukwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na viongozi wa vyama vya siasa kutoka vyama 12 ikiwamo CCM.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati walioshiriki ni wabunge Pindi Chana, Kingunge Ngombale-Mwiru na Nimrod Mkono, walioungana na viongozi wa vyama 12 vya CCM, CUF, Chadema, TLP, AAPT, Jahazi Asilia, Chausta, SAU, Tadea, UDP, NRA na UMD.
Alipomaliza kusaini sheria hiyo, wageni walipiga makofi kupongeza hatua hiyo kabla ya wimbo wa Taifa kupigwa, ikiwa ni ishara ya kuhitimisha moja ya shughuli ambazo matunda yao yanasubiriwa na wadau wengi hasa kutokana na ukweli wa kuwapo malalamiko mengi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi.
Baada ya kusaini sheria hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa nchi kufanya hivyo hadharani tangu Uhuru, Rais Kikwete alipiga picha na viongozi waliomshuhudia akisaini sheria hiyo, kisha akapiga picha na viongozi wakuu aliokaa nao meza kuu, kabla ya kujumuika na wageni kupata viburudisho.
Awali, kabla ya Rais kusaini sheria hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Philip Marmo, alitoa maelezo ya utangulizi, kwamba kutungwa kwa sheria hiyo ni ishara ya azma ya Serikali ya Awamu ya Nne ya mapambano yake dhidi ya rushwa na kudhamiria kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Marmo alisema tangu Uhuru umekuwapo uchaguzi wa aina mbalimbali, lakini pia malalamiko zaidi kuhusu matumizi ya fedha katika miaka ya karibuni kwenye uchaguzi wa 1995, 2000 na 2005.
“Yamekuwapo malalamiko kwamba kuna fedha zisizo na ukomo, ushindani usio dhahiri na kwamba wapiga kura wamekuwa wakichagua watu si kwa uzuri wa sera za vyama vyao, bali kwa misingi ya fedha,” alisema Marmo na kuongeza kuwa sheria hiyo imezaliwa kutokana na kusudio la Rais Kikwete alipolihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Desemba 30, 2005; mara alipoingia madarakani.
Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alizungumzia kutoridhishwa kwake na hali ya matumizi mabaya ya fedha katika uchaguzi ndani ya vyama vya siasa na baina ya vyama vya siasa, katika uchaguzi wa Serikali na kueleza nia yake ya kutaka kuchukua hatua thabiti za kuweka utaratibu utakaoongoza na kudhibiti fedha katika uchaguzi.
Marmo alisema sheria hiyo inakusudia kuweka utaratibu wa kusimamia gharama za uchaguzi kwa vyama na viongozi wao; kuweka utaratibu wa kisheria kwa kuwa na uwanja sawa na halisi wa ushindani; kudhibiti rushwa kwa vyama vya siasa na wagombea; kudhibiti zawadi, misaada na michango katika kampeni na kuwapo kwa uwajibikaji wakati wa kampeni na kuoanisha adhabu kwa watakaokwenda kinyume.
“Hii ni sheria nzuri, lakini si mwarobaini wa matatizo yote ya fedha katika uchaguzi. Ni mwanzo, lakini si haba,” Marmo alimweleza Rais Kikwete na wageni wengine waliohudhuria shughuli hiyo.
Tendwa alisema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kuridhia Azimio la Maputo la mwaka 2003, lililoelekeza nchi wanachama kuwa na sheria inayokataza matumizi na upatikanaji wa fedha haramu kwa vyama vya siasa na kuweka vifungu vyenye kuonesha uwajibikaji kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi na kampeni.
Tendwa, ambaye alisema sheria hiyo itatumika Tanzania Bara kwa nafasi zote tatu huku kwa Zanzibar ikihusika na uchaguzi wa Rais na wabunge tu, ni jambo jipya na ili kuepuka kuanza vibaya, “tumefanya utafiti wa kutosha na kujifunza kutoka mifano ya nchi ambazo zina utaratibu wa aina hii.”
Alisema nchini, walihusisha wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wa dini, asasi zisizo za Serikali, NEC na watu mbalimbali. Msajili, ambaye alisema sheria hiyo imetungwa kwa nia ya kuelewa (kuondoa) tatizo la matumizi mabaya ya fedha katika shughuli za uchaguzi, aliwasihi wadau wote wa sheria hiyo, kila mmoja kwa nafasi yake, ahakikishe inafanya kazi ili kuona matunda ya kweli na umuhimu uliokusudiwa katika kutungwa kwake.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo, gharama za uchaguzi ni fedha zote ambazo zimetumika au gharama zote zilizotumika kwa ajili ya mgombea wakati wa mchakato wa uteuzi, wakati wa kampeni na uchaguzi kwa chama cha siasa, mgombea na Serikali.
Akielezea namna walivyojipanga kutekeleza sheria hiyo, Msajili Tendwa alisema hadi Aprili 15 mwaka huu, ofisi yake itakuwa imekamilisha ufunguzi wa kanda tatu za Arusha, Mwanza na Mbeya na tayari imeomba ajira ya dharura ili kukamilisha rasilimaliwatu kwa ajili ya Mratibu wa Elimu ya Uraia na wanasheria sita kwa ajili ya kanda hizo tatu mpya.
Aidha, watakutana na wadau wa vyama vya siasa Machi 22 na 23, mwaka huu, kujadili kanuni zilizoandaliwa na kikosikazi kabla ya Waziri Mkuu kuzisaini kwa utekelezaji na pia kutakuwa na elimu ya uraia itakayoanza Machi 25 katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Akizungumzia sheria hiyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Chadema, Anthony Komu, alisema ni nzuri, lakini utekelezaji wake ndio changamoto kubwa inayoikabili Serikali na wadau wake. Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, alisema ni nzuri na imemsafishia njia ya kuwania ubunge Vunjo, akisema “watu walikuwa wakishinda kwa fedha haramu, fedha za wizi na ufisadi, lakini sasa wananchi, polisi, Takukuru wawe makini, wagombea wachaguliwe kwa ridhaa ya watu.”
Jaji Mkuu Augustino Ramadhani alisema sheria hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa, wakati Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alidai itakuwa ngumu kutekelezwa kwa sababu Ofisi ya Msajili wa Vyama ina upungufu wa watumishi.
Naye John Cheyo ambaye ni Mwenyekiti wa UDP, alisema sheria hiyo ni nzuri, lakini itategemea utekelezaji wake kwa vitendo, huku akisema anawaonea huruma CCM kwa sababu ndio wenye fedha.
No comments:
Post a Comment