Monday, March 15, 2010

Turudishe Azimio la Arusha – Sumaye


WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ameonesha wasiwasi kuhusu sheria inayotarajiwa kutungwa ya kutenganisha siasa na biashara, huku akipendekeza kurudishwa kwa misingi ya Azimio la Arusha kwani itasaidia nchi kurudi katika maadili.

Licha ya kuweka wazi utenganishaji huo kuwa ni jambo jema na kuliunga mkono, alisema utekelezaji wake utakuwa mgumu kutokana na kutokuwapo mipaka ya biashara na ya maadili.

“Tukitaka kufanikiwa kwa kutenganisha siasa na biashara, turudi kwenye maadili na turudishe Azimio la Arusha,” alisema Waziri Mkuu huyo aliyekaa madarakani kwa miaka 10. Azimio la Arusha lilianzishwa mwaka 1967 ambapo misingi yake ilikuwa kujenga usawa baina ya watu, kuweka maadili katika uongozi kwa kudhibiti kwa kiasi kikubwa rushwa katika uongozi. Lilizikwa mwaka 1992 Zanzibar.

Katika hotuba yake ya kila mwezi ya Januari mwaka juzi pamoja na kurudia mara kwa mara, Rais Jakaya Kikwete alieleza nia ya serikali ya kupeleka muswada bungeni wa kuanzishwa kwa sheria ya kutenganisha siasa na biashara, kwa kile alichokieleza kumekuwapo na mgongano wa kimaslahi.

Aliwataka mawaziri na wabunge kuchagua siasa au biashara, lakini si vyote kwa wakati mmoja. Sumaye alikuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotoa Sh milioni tano kwa Jukwaa la Wahariri jana Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa mafunzo ya maadili kwa waandishi wa habari.

Waziri Mkuu huyo mstaafu aliwahi kuahidi kutoa fedha kwa wanahabari wapewe mafunzo kutokana na fedha alizokuwa akidai mahakamani dhidi ya gazeti la Tanzania Leo ambalo alilishitaki kwa madai ya kumdhalilisha.

Fedha hizo ni sehemu ya malipo hayo. Aliunga mkono hatua ya wanachama mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumpigia debe Rais Jakaya Kikwete aweze kuendelea kuiongoza Tanzania katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, Sumaye ambaye aligombea urais pamoja na Kikwete mwaka 2005 na kutopitishwa na chama chake, alisema si vibaya watu wengine wakajitokeza kugombea urais na kupigiwa debe huku kwa upande wake, akiweka wazi kutogombea nafasi yoyote katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Alipoulizwa juu ya kuwepo makundi ndani ya CCM, alisema “suala hilo halininyimi usingizi kwani CCM ni chama kikubwa makundi lazima yawepo, lakini CCM ina utaalamu wa kutatua matatizo yake, hivyo tutakwenda katika uchaguzi vizuri.” Sumaye ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alipongeza kupitishwa kwa sheria ya gharama za uchaguzi, akisema sasa wagombea wasiokuwa na fedha, lakini wanapendwa na wananchi watashinda.

Mwanasiasa huyo alitetea kuwepo kwa mgombea binafsi, lakini akasema kwa Tanzania haitawezekana katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kutokana na marekebisho ya sheria kuchukua muda mrefu.

Akizungumzia sakata la ununuzi wa rada, alisema uamuzi wa serikali ulikuwa sahihi ila matatizo yalitokea kwenye utekelezaji wake.

“Kuna wakati ndege ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ilitaka kuanguka hapa nchini kutokana na kutokuwa na rada, mataifa mbalimbali yalishatishia kusimamisha ndege zao kuja nchini hivyo ilitulazima kununua rada,” alifafanua Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu wakati wote wa Serikali ya Awamu ya Tatu.

Waziri Mkuu huyo mstaafu ambaye sakata hilo la rada lilitokea wakati wa utawala wake, alisema waliosimamia ununuzi huo walileta matatizo, lakini sasa wanachunguzwa hivyo uchunguzi ukikamilika wafikishwe mahakamani.

Miongoni mwa viongozi wanaotuhumiwa kupokea rushwa katika ununuzi huo na kuilazimu serikali kununua kwa gharama kubwa kuliko gharama halisi ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge.

Kwa upande wa suala ya wizi katika fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Sumaye alisema suala hilo halifahamu na wakati wake serikali isingeweza kuingilia mambo ya ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwani ilikuwa na Bodi ya Wakurugenzi waliokuwa wakifanya uamuzi.


Kuhusu kutangaza mali zake, Sumaye alisema kwa sasa haoni sababu ya yeye kutangaza na kusisitiza, “nilipoingia madarakani kila mwaka nilikuwa natangaza na baada ya kumaliza muda wangu nilitangaza, sasa nimeshakaa miaka mitano kama raia sihitaji kutangaza labda kuwe na tuhuma, nako si kuwaambia ninyi, bali vyombo vya usalama."

Alipotakiwa kuzungumzia mapigano yanayotokea katika maeneo ya Hanang mkoani Manyara na Tarime, Mara, alisema, “Tangu enzi za Mwalimu Nyerere (Julius), Tarime kumekuwa na mapigano ingawa sasa yamezidi hii inaonesha mmomonyoko wa maadili, Hanang tatizo si kubwa, viongozi wanaweza kushughulikia.”

Awali, alieleza kusudio lake la kulishitaki gazeti la Changamoto mahakamani kwa kumshushia hadhi yake, kwa kuandika habari inayoeleza kuwa akishirikiana na aliyekuwa Waziri wa Mipango na Ubinafsishaji, Dk. Abdallah Kigoda, walipora shamba la Mamlaka ya Chai la Mlangali Lupembe, mkoani Iringa lenye hekta 200 bila kulipa malipo yoyote serikalini.

No comments: