WANASIASA wa vyama mbalimbali vya upinzani wamependekeza matumizi kwa wagombea katika kampeni za uchaguzi mkuu ziongezwe, kwa maana fedha zilizopendekezwa na Serikali ni kidogo.
Serikali ilipendekeza gharama za matumizi ya mgombea urais yasizidi Sh bilioni moja, huku ubunge na udiwani gharama zikiwa zinategemea eneo la jimbo, idadi ya watu na hali ya miundombinu.
Katika majadiliano ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi yaliyomalizika Dar es Salaam, jana, wanasiasa hao walisema gharama zilizowekwa hazilingani na hali halisi ya sasa na wala haziendani na kupanda kwa gharama za maisha mwaka hadi mwaka kutokana na sababu mbalimbali, likiwamo ongezeko la watu na ukame.
Aidha, walisema sheria hiyo inatakiwa kufanyiwa marekebisho ya kina ili isilete usumbufu siku za baadaye kwa kutakiwa kubadilishwa kutokana na ongezeko la mahitaji au kupanda kwa gharama za maisha.
John Mnyika wa Chadema alisema viwango vilivyopendekezwa ni vidogo kutokana na maeneo mengine kuwa na majimbo makubwa na vituo vingi vya uchaguzi, hivyo Sh bilioni moja haitatosheleza shughuli zote za uchaguzi.
“Chadema tulifanya kampeni katika uchaguzi uliopita na tulitumia zaidi ya Sh milioni 700 na hatukuzunguka majimbo yote, hivyo Sh bilioni moja kwa sasa ni kiwango kidogo ikilinganishwa na gharama za maisha zilivyopanda, labda angalau Sh bilioni mbili au tatu,” alisema.
Alisema pamoja na viwango hivyo kuwa vidogo, lakini kinachopaswa kuangaliwa zaidi ni matumizi sahihi ya gharama ambapo pia alisema sheria hiyo imechelewa kujadiliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema ni ngumu kufanya makadirio ya gharama za uchaguzi kwa sababu kila chama kina mapendekezo yake ya jinsi ya kufanya kampeni ambapo wengine hutumia matangazo mengi kwenye vyombo vya habari na wengine magari na helikopta kufuata wananchi.
“Ni ngumu sana kufanya makadirio ya gharama za uchaguzi maana hata wananchi nao wana mtazamo tofauti, sasa hivyo mtu huwezi kuwaendea kwa miguu tu, wengine wanalazimika wakati mwingine kutumia magari na wengine helikopta,” alisema.
Alisema tatizo si fedha ila kinachopaswa kuangaliwa ni jinsi inavyotumika na kueleza kuwa wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakizitumia kununua watu na wengine kuzigawa kama njugu wakati wa kampeni za uchaguzi.
“Kwa kipindi cha nyuma, tumekuwa tukivumilia uchaguzi wa aina hiyo ila kwa sasa uchaguzi wa ‘kumwaga’ fedha utadhibitiwa na wengi waliokuwa wakifanya hivi ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), maana walikuwa wanaona uongozi ni pesa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbrod Slaa, alisema uchaguzi ujao unaonekana kuwa mgumu kutokana na sheria hiyo na kueleza kwamba ingawa lengo ni kuzuia rushwa, lakini fedha hizo ni kidogo.
Aidha, wadau hao walitaka kifungu cha kuwapo kwa watu maalumu wa kampeni kubadilishwa, kutokana na kifungu kinachoonesha kwamba baada ya watu hao kutambuliwa, hatatakiwa mtu mwingine kumnadi mgombea kama si mwanakampeni.
Walisema hiyo ni kuwanyima Watanzania haki za msingi za kumnadi mgombea wanayemtaka na wakataka mgombea anapohitaji kubadilisha watu wanaomkampenia kutoomba kibali upya na badala yake kutoa taarifa tu kwa Mamlaka iliyopo.
Rais wa Tadea, John Chipaka, alisema haina haja ya kubanwa kwa fedha hiyo na badala yake wananchi wasimamie uchaguzi wenyewe na kutoa taarifa kwa wanaogawa vitenge au sukari, ili wapewe kura maana hao ndio wanaoua maendeleo ya nchi kutokana na kutorudi kuwaangalia wanapochaguliwa.
No comments:
Post a Comment