BAADA ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Sheria ya Gharama za Uchaguzi wiki iliyopita, Serikali imependekeza matumizi kwa mgombea urais yasizidi Sh bilioni moja kuanzia kwenye mchakato wa kuteuliwa na chama hadi kampeni.
Kwa upande wa wagombea ubunge, gharama hizo zinategemea eneo la jimbo, idadi ya watu na hali ya miundombinu. Mgombea ubunge ambaye jimbo lake liko makao makuu ya mkoa ambalo watu wake ni zaidi ya 300,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 40.
Jana wadau mbalimbali zikiwamo asasi za kiraia na vyama vya siasa, walijadili rasimu hiyo ya kanuni na taratibu zitakazotumika wakati wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, CCM haikuwakilishwa kwenye majadiliano hayo ambayo yalifanyika kwenye ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam.
Kwa mgombea ambaye jimbo lake liko nje ya makao makuu ya mkoa na idadi ya watu haizidi 100,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 20 wakati kwa jimbo lenye watu ambao hawazidi 150,000 kiasi cha fedha anachotakiwa kutumia ni Sh milioni 30.
Mgombea ambaye jimbo lake liko nje ya makao makuu ya mkoa na wapiga kura wake ni kati ya 150,000 na 300,000, atatumia fedha isiyozidi Sh milioni 35.
Lakini kwa mgombea ubunge katika majimbo yaliyoko kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza bila kujadili idadi ya watu, atalazimika kutumia fedha zisizozidi Sh milioni 20.
Katika mchanganuo huo pia wagombea ubunge wa Zanzibar ambao majimbo yako katika makao makuu ya mikoa na wapiga kura wanazidi 10,000 watatakiwa kutumia Sh milioni 10.
Wagombea ubunge wa Zanzibar ambao majimbo yao yako nje ya makao makuu ya mikoa na yana watu ambao hawazidi 10,000 watatumia si zaidi ya Sh milioni saba.
Kwa upande wa viti maalumu Tanzania Bara ambao wapiga kura ni zaidi ya 10,000 kiasi cha fedha kinachopendekezwa kutumiwa ni Sh milioni tatu.
Katika mpango huo wagombea udiwani katika maeneo ya mjini kiasi wanachotakiwa kutumia si zaidi ya Sh milioni saba na wale ambao kata zao ziko vijijini, matumizi yao yatatakiwa yasivuke Sh milioni 10. Wakati wagombea udiwani wa viti maalumu matumizi yao hayatakiwi kuzidi Sh milioni moja.
Kwenye rasimu hiyo ya kanuni katika kipengele kinachohusu timu ya kampeni kwa ajili ya gharama za uchaguzi, mgombea urais wajumbe hawatazidi 50, mgombea ubunge wajumbe hawatazidi 20 wakati mgombea udiwani wajumbe hawatazidi 10.
Wajumbe hao wa kampeni watatakiwa wathibitishwe baada ya mgombea kuwasilisha maombi kwenye Mamlaka iliyoamuliwa na sheria hiyo siku 10 kabla ya uteuzi au siku 10 baada ya uteuzi.
Mgombea ambaye atabadili timu yake ya kampeni, atalazimika kutuma maombi kwenye Mamlaka inayohusika kwa ajili ya mabadiliko hayo. Katika rasimu hiyo mamlaka inayohusika inaweza kukataa kufanya mabadiliko kama itaridhika kuwa mjumbe huyo hawezi kuathiri kampeni za uchaguzi.
Katika rasimu hiyo, licha ya kupendekezwa kuwa mgombea aliyepata kura nyingi kwenye chama ndiye ateuliwe na chama chake kugombea urais, ubunge na udiwani, lakini wadau walikikataa kifungu hicho.
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, alisema kipengele hicho hakifai kwani kuna baadhi ya wagombea wanaweza kutumia fedha kurubuni wapiga kura; hivyo akapendekeza kifungu hicho kiongezwe maneno kuwa “itakapothibitika kuwa aliyeongoza alitumia rushwa basi chama kitumie taratibu zake kumpata mgombea”.
Mwenyekiti wa Chausta, James Mapalala, alisema eneo hilo ndilo msingi wa demokrasia na kama kanuni hazitasema wazi kuwa mtoa rushwa aondolewe, anaweza kuingia mtu madarakani akaharibu Taifa kwa rushwa.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, alisema lazima kifungu hicho kirekebishwe, ili kuvipa vyama fursa ya kupokea malalamiko ya walioshindwa na ikithibitika kuwa aliyeshinda alitumia rushwa, aondolewe.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema utaratibu uliopo ndani ya vyama utumike. Alisema iwapo kifungu hicho kitaachwa kilivyo, CCM itasaidia wagombea wa upinzani ambao ni dhaifu, ili kushinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya vyama.
“Tukikiacha hivi hiki kifungu vyama vingine vinaweza kupata wagombea dhaifu ambao hawauziki … na hii ndiyo kazi ya Kamati Kuu na Baraza Kuu kuchambua ni mgombea gani anakubalika anayeweza kukipa ushindi.
“Ili kutopata mgombea dhaifu, tupeni nafasi ya kurekebisha hili, wewe Msajili (wa Vyama vya Siasa) na meza yako hiyo hamna vyama, sisi ndio tunajua mambo yaliyoko ndani ya vyama vyetu, tunaomba mturudishie taratibu za kupata wagombea,” alisema Profesa Lipumba.
Msajili wa Vyama John Tendwa alikubaliana na mapendekezo ya wadau hao “hizi ni kanuni zenu na wala si za CCM. Kwa mapendekezo yenu na sisi tunakubaliana nayo,” alisema Tendwa ambaye alifuatana na Mwandishi wa Sheria, Casmir Kyuki.
No comments:
Post a Comment