MWELEKEO wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kusaidia taifa kuondokana na hatari ya kuzidi kutanuka kwa pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho nchini umeanza kutia shaka, malalamiko yakianza kuibuka miongoni mwa wafanyakazi wake wa ngazi za chini, baada ya menejimenti hiyo kuamua kuongeza kiwango cha mikopo kwa watumishi wake katika hali inayozua maswali zaidi.
Malalamiko ya baadhi ya wafanyakazi wa chini BoT kuhusu kuwapo kwa tofauti kubwa ya kipato kati yao na wakurugenzi, yanaungana na hadhari iliyowahi kutolewa na baadhi ya viongozi wastaafu nchini kuhusu taasisi za serikali kushiriki kutanua pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho.
Menejimenti ya BoT, Desemba 2, mwaka huu imetoa taarifa kwa wafanyakazi wake inayoeleza kuongezeka maradufu kwa viwango vya mikopo katika hali inayotafsiriwa na wafanyakazi wadogo kuwa, inalenga kuwanufaisha zaidi vigogo wa chombo hicho nyeti nchini.
Tofauti hiyo inajitokeza kwenye viwango vya utoaji mikopo, ambapo wakurugenzi, wakurugenzi washiriki, watalaamu washauri waandamizi watakopeshwa Sh milioni 100 ikiwa ni mikopo ya nyumba wakati makarani, madereva, walinzi na wahudumu wa ofisi, zahanati na jikoni wakipewa haki ya kukopa kiasi kisichozidi Sh milioni 30, hali inayozusha malalamiko ya chini chini.
Uchunguzi wa Raia Mwema kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu umebaini kuwa licha ya BoT kuwa na jukumu zito kitaifa la kuisaidia Serikali kupunguza pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho, pia uamuzi wa menejimenti ya benki hiyo umeanza kukabiliwa na malalamiko miongoni mwa wafanyakazi wa ngazi za chini.
“Tulidhani utoaji mikopo utazingatia kupunguza pengo lililopo la kipato miongoni mwa wafanyakazi na kwamba wale ambao mishahara yao midogo wapewe mkopo wa muda mrefu zaidi lakini kwa kiwango kikubwa, mambo yamekuwa kinyume.
“Kiwango cha mikopo muhimu kama ya makazi kimeongezwa mara mbili lakini wale wa juu wamebaki pale pale na wa ngazi ya chini wamebaki chini zaidi, mfano huu unawasilisha hali halisi ya utendaji serikalini, wakubwa wanapata zaidi wakati wadogo wanazidi kubaki chini,” alisema mfanyakazi mmoja wa BoT, katika ngazi ya ofisa mwandamizi (professional I).
Juhudi za Raia Mwema kumpata Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, hazikuzaa matunda, baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa na majibu.
Kumekuwapo na kilio cha muda mrefu kutoka si tu kwa viongozi wastaafu bali hata wanaharakati kuwa pengo la kipato nchini limekuwa likizidi kutanuka na kuibua matabaka yasiyo ya lazima. Moja ya taasisi zilizoko mstari wa mbele kukosoa mwenendo mbovu wa kusimamia mgawanyo sahihi wa rasimali za nchi ni taasisi ya Policy Forum.
Taasisi hiyo imewahi kutoa ripoti inayoeleza namna Tanzania ilivyofanya vibaya ukilinganisha na nchi zingine katika kupunguza umaskini.
Kwa mujibu wa Policy Forum, kwa kulinganishwa na nchi zilizoko kwenye kiwango chake cha uchumi, nchi hizo zimetekeleza vizuri sera za kupunguza umasikini ambazo zimekuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwenye ukanda wa Afrika.
Kati ya nchi zilizoingia kwenye rekodi hiyo ni pamoja na Ghana, Uganda na Asia hususan nchi za Vietnam na India.
Inaelezwa kuwa wakati Tanzania idadi ya watu masikini ilipungua kwa asilimia 2.4 kati ya mwaka 1991 na 2007, kwa Uganda, Ghana na Vietnam ilipungua karibu mara 10 zaidi, ikiwa kwa wastani wa asilimia 23 hadi 24. India nayo ilifanikiwa kupunguza idadi hiyo kwa kiasi kikubwa takriban asilimia saba kwa kipindi kifupi mno.
Inaelezwa kuwa uchumi wa soko huria Tanzania, kwa sasa umeshindwa katika kupunguza umasikini wa kipato kwa Watanzania wengi, ingawa pia tahadhari ikiwekwa kutambua mafanikio katika nyanja nyingine kama watoto masikini kujiunga shuleni, lakini inaonyesha kuwa kwa Watanzania wengi uwezo wa kujikimu wao wenyewe haujabadilika.
Hali hiyo yote inahusishwa na kuongezeka kwa pengo kati ya masikini na matajiri nchini. Moja ya vyombo vya umma vinavyopaswa kutafakari na kuwa mfano bora katika kuweka mwelekeo wa uchumi unaomkumbuka zaidi masikini ni pamoja na Benki Kuu ya Tanzania, kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi.
Mwishoni mwa wiki Raia Mwema, lilipata nakala ya waraka wa kuongezwa kwa viwango vya mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi wa BoT, makao makuu na katika matawi yake kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Zanzibar na katika Chuo cha benki hiyo, jijini Mwanza.
Katika taarifa hiyo, wafanyakazi wa daraja la chini wanakopeshwa Sh milioni 30 kutoka milioni 15 za awali kwa ajili ya mikopo ya nyumba lakini kinachozua hisia za malalamiko ni kwa wakurugenzi kupata donge nono zaidi la Sh milioni 100, kwa kisingizio cha uwezo wa kulipa unaojengewa hoja na kuwa na mishahara minono, ambayo hata hivyo imepangwa na vigogo serikalini.
Mameneja na wataalamu washauri watapata mkopo wa milioni 90, wakati daraja la tatu linawagusa meneja wasaidizi na maofisa wakuu waandamizi wanakopeshwa Sh milioni 70.
Kundi jingine la nne linawahusisha maofisa wakuu (professional I) na maofisa wakuu waandamizi (professional II), wakikopeshwa Sh milioni 60, huku wafanyakazi wenye vyeo vya maofisa waandamizi (professional I) na maofisa wakuu (professional II) watapata mkopo wa Sh milioni 55.
Daraja la sita ni maofisa ngazi ya III-I (professional I), maofisa waandamizi (professinal II) na maofisa- makarani wakuu (cleric officers) watakaoambulia Sh milioni 45.
Maofisa-makarani kuanzia ngazi ya III hadi ngazi ya maofisa-makarani waandamizi (cleric officers), makarani waandamizi na makarani wakuu (clerks) wamepangiwa mkopo wa Sh milioni 40.
Kundi la nane ni ambalo ni la chini ni walinzi, wapishi, madereva, wahudumu wa ofisi na wa zahanati na makarani ngazi ya daraja la III-I ambao watakopeshwa Sh milioni 30.
Hata hivyo, licha ya uamuzi huo kutajwa kuwafurahisha baadhi ya wafanyakazi lakini umezidi kuzua maswali zaidi kwa kuwa msingi wa kutoa mikopo imekuwa ikitokana na kiwango cha mishahara, ambacho hata hivyo ni kikubwa kwa wakurugenzi ikilinganishwa na wafanyakazi wa chini.
Hoja zinazotolewa na baadhi ya wanaoona hatari ya kuzidi kutanuka kwa pengo la wenye nacho na wasio nacho nchini na hususan mfano mbaya ukianzia BoT ni kuwapo kwa pengo kubwa la mishahara, ambalo ndiyo msingi wa pengo kubwa la mikopo.
Uchunguzi zaidi wa Raia Mwema umebaini kuwa hali hiyo ya kuwapo kwa pengo kubwa la mishahara miongoni mwa wafanyakazi wa serikalini nchini kumezidi kukandamiza kimaendeleo wafanyakazi wa kawaida, na kwa kiasi kikubwa kuchangia mmomonyoko wa maadili, na wakati mwingine taarifa nyeti za serikali zikiwafikia matajiri wachache wanaozitumia kwa manufaa yao wakizinunua kutoka kwa wafanyakazi wenye njaa.
No comments:
Post a Comment