Monday, December 7, 2009

Magazeti ya udaku na Jinsia

Na Privatus Karugendo

MAGAZETI ya udaku, ama magazeti pendwa kama wenyewe wanavyotaka yaitwe duniani kote, yana sifa mbalimbali, ikiwamo kutangaza uongo na hata umbeya. Pamoja na ukweli kwamba magazeti ya aina hii nchini yanasomwa na wengi, bado tunayadharau na kufikiri kwamba yanasomwa na watu wasiokuwa makini.

Kamusi ya Kiswahili sanifu inaelezea neno udaku kama tabia ya kutafuta na kutaka kujua habari za watu; kilimilimi na umbea. Kuyabatiza magazeti haya kuwa ya udaku ni lengo zima la kutoa ujumbe kwamba haya ni magazeti ya umbea na uzushi.

Je, ni kweli kwamba magazeti haya ni ya umbea na uzushi? Je, watu wengi, na hasa vijana wanapenda kusoma umbea na uzushi? Kila mahali magazeti haya yanauzwa sana. Ukweli ni kwamba magazeti ya udaku yanasomwa sana. Lakini kwa nini watu wapende kusoma umbea na uzushi?

Hoja ninayoijenga katika makala hii si kununuliwa kwa magazeti au kutonunuliwa; bali ni kutaka kumshirikisha msomaji ufunuo nilioupata juu ya magazeti ya udaku. Mimi pia nilikuwa kati ya watu waliokuwa wakiyapiga vita magazeti ya udaku. Nimeandika makala nyingi nikipinga utamaduni wa watu kuacha kusoma vitabu na magazeti makini na kukimbilia magazeti ya udaku. Niliamini kabisa kwamba wale wote wanaoyasoma magazeti ya udaku si watu makini.

Inawezekana kabisa nikawa sijafanikiwa kufahamu vizuri sababu inayowasukuma watu kusoma magazeti ya udaku; na inawezekana pia kwamba wale wanaoyaandika magazeti ya udaku wana malengo na nia tofauti na ile niliyofunuliwa. Hata hivyo, ukweli unabaki pale pale kwamba magazeti ya udaku yanaandika maswala ya jinsia kuliko magazeti tunayoyaita ni makini.

Karibia magazeti yote ya udaku kurasa zake za mbele zinapambwa na masuala ya jinsia. Mifano ya magazeti haya na habari zinayoandika ni mingi. Inahusu wanasiasa kushiriki ngono; mafumanizi, ufusika wa kupindukia na nyingine nyingi. Ingawa hapa ninatoa mfano wa habari katika magazeti machache tu, ukweli ni kwamba karibia magazeti yote ya udaku yanaandika mambo ya jinsia na yaliyo tofauti. Hakuna gazeti linalorudia yale yaliyoandikwa na gazeti jingine. Kila gazeti linajitahidi kuibua kitu kipya. Ukitaka kufahamu hali ya jinsia ilivyo katika taifa letu la Tanzania, soma magazeti ya udaku.

Wanaharakati wa kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi, wanaharakati wa haki za binadamu na wanaharakati wote wanaotetea usawa wa kijinsia, watakubaliana na mimi kwamba niliyoyataja hapo juu ni masuala ya jinsia. Ni nadra sana kuona magazeti makini yakibeba maswala ya jinsia kwenye kurasa za mbele. Ikitokea yakawemo ni katikati na yanapewa nafasi ndogo kinyume na yanavyofanya magazeti ya udaku.

Inawezekana kwamba habari hizo zinakuwa zimehakikiwa na kuchujwa na wamiliki au na hata Serikali. Habari nyingine zinachujwa na viongozi wa dini na zile ambazo ni nyeti zaidi zinafunikwa na kufichwa kabisa hadi Kristo atakaporudi mara ya pili! Kwa njia hii hatuwezi kujisahihisha, kwa njia hii hatuwezi kuendelea. Nchi nyingi zilizoendelea zimeheshimu na kukumbatia usawa wa kijinsia.

Magazeti tunayoyaita makini yanaandika habari za siasa, za wanasiasa na matukio yanayowahusu wanasiasa hasa katika kurasa zile za mbele. Haina maana kwamba haya nayo si muhimu katika jamii. Ila ni kwamba magazeti yale tunayoyaita makini hayazingatii habari za jinsia.

Pia waandishi wa magazeti haya tofauti na ilivyo kwa magazeti ya udaku, hawaitumi kutafuta habari kwenye vyanzo mbali mbali. Mara nyingi wanajikita kwenye vyanzo vya kiserikali; kusubiri pale Maelezo au kusubiri mikutano ya viongozi wakuu na waandishi wa habari. Pia wamejenga utamaduni wa kutafuta habari za matukio mbali mbali kama vile vifo, kupigwa, kubakwa kutoka kwa makamanda wa polisi wa wilaya na mikoa.

Matokeo yake ni kwamba, haya magazeti yetu makini, ukisoma mmoja huna haja ya kusoma jingine. Wakati mwingine unakuta karibia magazeti yote yana habari ile ile kwenye kurasa za mbele.

Hata ukisoma kurasa za ndani unakuta habari zinafanana. Kwa wale wanaosikiliza mapitio ya magazeti kwenye runinga watakubaliana na hoja yangu maana anayeyapitia magazeti akishasoma habari za gazeti linalotangulia, anabaki kusema; “ habari hii imejirudia karibia katika magazeti yote”. Jambo hili linaeleweka vizuri, maana magazeti haya vyanzo vyao vya habari ni vilevile. Hawatafuti habari, wanasubiri kuletewa habari. Wanasubiri kuambiwa ni lipi la kuandika na ni lipi la kuacha. Kwa njia hii wanajikuta wanayaweka maswala ya jinsia pembeni.

Magazeti ya udaku hata yote yakitoka siku mmoja, ni vigumu yawe na habari zinazofanana. Waandishi wao wanatafuta habari. Hawategemei kupata habari kutoka maelezo au kusubiri mikutano ya waandishi wa habari na viongozi au watu maarufu katika taifa letu. Wanaingia ndani ya jamii na kutafuta habari zinazogusa maisha ya watu. Wanaibua mambo mengi ya jinsia. Wanaibua ukatili majumbani, wanaibua vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake na watoto, wanaibua matendo ya udanganyifu katika ndoa, wanaibua rushwa ya ngono, kwa ufupi wanaibua mambo yote yanayokwenda kinyume na maadili.

Ni kiasi gani yale yote yanayoibuliwa na magazeti ya udaku yanafanyiwa kazi ni swali la kujiuliza. Ni kiasi gani yanayoibuliwa yana ukweli pia ni swali la kujiuliza. Je, mashirika ya kutetea haki za binadamu, mashirika ya harakati za kujenga vuguvugu la kumkomboa mwanamke kimapinduzi ni kiasi gani wanatumia habari za udaku kuimarisha mapambano yao na mfumo dume? Je, na wanaharakati wanayanyanyapaa magazeti ya udaku? Wanayanyanyapaa magazeti yanayoandika na kuibua maswala ya jinsia?

Swali jingine, ambalo nimeligusia mwanzo mwa makala hii ni kiasi gani wamiliki na wahariri wa magazeti ya udaku wanafahamu umuhimu wa habari wanazoziandika? Ni kweli kwamba wanaandika habari hizi kuibua maswala ya kijinsia au imetokea tu bahati mbaya wakati wakiwa kwenye harakati za kutafuta fedha? Au walifanya utafiti na kudungua kwamba vijana wengi wanapenda kusoma habari zinazoelezea mahusiano ya mwanamke na mwanaume? Habari za mapenzi, habari za ngono na mambo yote yanayofanana na hayo? Vijana ni wengi – hivyo soko ni kubwa?

Je, wanaadika kuuza magazeti yao? Ili wapate fedha na kuwa matajiri? Kuwa matajiri kuisaidia jamii au kuwa matajiri kwa faida yao na familia zao? Au wanaandika kufundisha jamii? Wanaandika kuibua maswala ya jinsia kwa lengo la kusambaratisha mfumo dume ili kuleta usawa wa kijinsia? Wanaandika kwa vile wao ni wanaharakati? Au nao pamoja na kuandika majumbani kwao wanaendeleza mfumo dume?

Kuna haja ya kuyaangalia magazeti ya udaku kwa mtizamo mpya! Hata kama wanaoyaandaa wana malengo mengine, lakini yale wanayoyaibua kuna haja ya kuyafuatilia; kuna haja ya kufanya utafiti zaidi ili kubaini ukweli. Kwa njia hii tunaweza kutoa mchango mkubwa katika kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu na kuzingatia usawa wa jinsia.

Wakiandika juu ya fumanizi, tukio hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya ukatili majumbani, kwa vile wanatoa majina ya watu na wakati mwingine maeneo ya tukio, ni vyema matuko haya yafuatiliwe kwa karibu. Wakiandika juu ya rushwa ya ngono, jambo hili lifuatiliwe. Wakiandika juu ya wabunge wetu kuwa na nyumba ndogo kule Dodoma, kuwasafirisha watoto wadogo hadi Dodoma ili kufanya nao vitendo vya ngono , jambo hili lifuatiliwe ili waheshimiwa wetu wawajibishwe na kusaidiwa kuyabadilisha maisha yao.

Wakiandika juu ya waheshimiwa wabunge kununua dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wingi wakati wa vikao vya Bunge, jambo hili lifuatiliwe – kwa nini wabunge wetu wahitaji nguvu za ziada kufanya tendo la ngono wakati wako mbali na familia zao? Bungeni wanahitaji nguvu za kufanya ngono au nguvu za kufikiri na kufanya kazi? Lolote litakalo andikwa na udaku lifuatiliwe, hsasa kama linaibua habari za jinsia.



Simu:
0754 633122

No comments: