MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Job Ndugai amekiri kuwa, kamati hiyo imeyaona maboma ya wafugaji wa jamii ya wamasai yaliyochomwa wakati wa operesheni ya kuwahamisha kutoka eneo la uwindaji, Loliondo mkoani Arusha.
Akizungumza mara baada ya kumaliza ziara ya kutembelea vijiji ambavyo vimeathirika wakati wa operesheni hiyo Ndugai, amesema, maboma yaliyochomwa baadhi ni ya muda na mengine ni ya kudumu na kwamba wafugaji walikuwa wakiishi humo.
“Kwa kweli hilo halina ubishi,tumeshuhudia kuchomwa kwa maboma jambo ambalo si zuri,“ amesema Ndugai.
Mbunge huyo wa Kongwa (CCM) ameyasema hayo wakati anazungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Sointsambu ambacho kilikuwa cha mwisho kutembelewa na kamati hiyo.
Bunge liliipa kamati hiyo jukumu la kuchunguza mgogoro wa Loliondo baada ya Mbunge wa Ngorongoro, Kaika Telele (CCM) kutoa maelezo binafsi bungeni kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu uliodaiwa kufanywa na Polisi wa kutuliza ghasia(FFU).
Wafugaji walihamishwa katika eneo hilo linalodaiwa kukodishwa kwa kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC) kwa ajili ya uwindaji.
Ndugai amesema,wabunge walipotembelea maeneo mbalimbali na kuzungumza na baadhi ya wawekezaji, viongozi wa mkoa na wilaya wamegundua kuwepo kwa upungufu kwenye sheria za vijiji na sheria za wanyama pori.
“Hii sheria ya wanyama pori ya ina mapungufu makubwa haielezi mpaka wa pori tengefu katika eneo hili ni ipi, kwani sheria ya vijiji inatambua kuwa maeneo yanayopigiwa kelele ni maeneo halali ya vijiji hadi mpakani na mbuga ya Serengeti,” amesema Ndugai.
Ndugai amesema, Rais Jakaya Kikwete amesaini sheria mpya ya wanyama pori hivyo inaweza kutumika Loliondo kuepusha matatizo hayo kwani inaeleza mipaka ya hifadhi za taifa, pori tengefu.
Amewasihi wananchi wa Loliondo wawe na subira na matumaini kwa kamati hiyo ya Bunge iliyotembelea vijiji saba. “Nawahakikishia kuwa tutakuja na ushauri mzuri kwa Serikali kuhusu tatizo hili la Loliondo.”
Kamati hiyo ilitembelea vijiji vya Oloipiri, Oleirien Magaiduru, Losoito Maalon, Arash, Piyaya, Ololosokwan, na Soint Sambu.
No comments:
Post a Comment