Monday, December 14, 2009

Makamba hajatulia ! Jaji Warioba

WAZIRI Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais (mstaafu), Jaji Joseph Warioba, amesema matusi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba kwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere na washiriki wa kongamano la miaka 10 kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, hayawanyimi usingizi na kwamba, kiongozi huyo ndiye kinara wa kundi la chuki CCM.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hoja zilizojadiliwa kwenye kongamano hilo jijini Dar es Salaam, zinahusu Taifa na si watu binafsi, akitolea mfano, kuporomoka kwa maadili na viashiria vya kusambaratisha umoja wa kitaifa.

“Rais Kikwete akisema nchi inakabiliwa na matatizo ya kuporomoka kwa maadili, ubaguzi, rushwa na ufisadi ni sawa. Salim na Warioba wakisema hayo hayo wanaitwa watu wenye chuki na wivu.

“Waziri Mkuu Pinda akisema kwamba tofauti ya kipato kati ya matabaka ni hatari kwa usalama wa taifa Makamba anaona ni sawa. Lakini maneno hayo hayo yakisemwa na Salim na Warioba wanaonekana ni wehu na wahuni.

“Maneno hayo hayo yamesemwa kwenye makongamano na semina nyingi, bungeni na mahali pengine lakini Mh. Makamba hakuita waandishi wa habari. Lakini yaliposemwa kwenye kongamano la Taasisi ya Mwalimu Nyerere ameita waandishi wa habari na kutukana.

“Makamba alikuwa anawasifu sana viongozi waliopita. Sasa anawalaumu. Hivi Makamba anamsifu kiongozi kutoka moyoni kwake au ni kutekeleza ajenda binafsi. Kumsaidia kiongozi wako siyo lazima kumsifu wakati wote bali pia kutoa ushauri mgumu.”

Alisema Warioba wakati akizungumza na Raia Mwema jijini Dar es Salaam mapema wiki hii.

Ameelezea kushangazwa na Makamba kutoa matusi bila kugusia hoja zilizopo na wala kupata muhtasari wa yaliyojadiliwa kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, George Mkuchika, ambaye alihudhuria kongamano hilo.

Siku chache baada ya kongamano hilo kumalizika, Makamba alizungumza na waandishi wa habari na kuwaita baadhi ya washiriki wehu kutokana na hoja walizotoa na hasa kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua uamuzi mgumu ili kudhibiti mwenendo wa mambo yanaonekana kuwa ya ovyo na akishindwa astaafu.

“Sisi tumesikia matusi aliyotoa Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Makamba, lakini hayatunyimi usingizi. Mheshimiwa Makamba siyo Waziri Mkuu wa Rais Kikwete lakini inaonekana anatumia muda mrefu sana kuzungumzia mambo ya serikali badala ya kujishughulisha na mambo ya chama.

“Kwa muda sasa, kumetokea maneno ya kubeza, kukejeli, matusi kila baadhi yetu tunapozungumzia mambo ya msingi ya kitaifa na hayo yamesemwa kutoka Makao Makuu ya Chama, siyo kutoka serikalini.

“Oktoba (mwaka huu), nyinyi waandishi wa habari mlituhoji mimi na Salim (DK. Salim Ahmed Salim) ili tutoe maoni yetu kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 10 tangu Mwalimu alipotutoka.

“Baada ya kusema tuliyosema alitokea mtu makao makuu ya chama akatutukana. Hakushughulika na hoja tulizotoa, sisi tulizungumzia mambo mawili makubwa.

“Moja, ni kuporomoka kwa maadili katika taifa letu, la pili mmomonyoko kwenye umoja wa taifa lakini tulitukanwa kwamba sisi ni watu tunaomwandama Rais Kikwete.

“Lakini mwezi huo huo, Rais Kikwete akahutubia taifa kutokea Butiama akazungumzia mambo yale tuliyozungumza tena kwa ufasaha zaidi kuonyesha kwamba ni matatizo kwenye nchi.

Alizungumzia kuporomoka kwa maadili, hatari inayooneka kwenye kusambaratika kwa umoja wetu, alizungumzia rushwa akazungumzia ufisadi. Ni yale yale tuliyokuwa tumeyasema na sisi tulifarijika, tukapumua tukaona kumbe Rais wetu anaelewa haya matatizo,” alisema Warioba na kuongeza kuwa:

“Sasa wakati ule tumetukanwa kulikuwa na reaction ya watu mbalimbali baadhi walituambia kwamba yule kijana aliyesema alikuwa ametumwa na Makamba ili atutukane, sisi hatukuamini.

“Kongamano limetambua juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya madini lakini wametoa ushauri namna ya kuboresha zaidi, wametambua juhudi za serikali kuhusu umiliki wa ardhi lakini wamesema juhudi zaidi zinahitajika, wametambua juhudi za serikali katika kuboresha elimu lakini wanasema juhudi zaidi zinahitajika.

“Lakini kubwa zaidi walizungumza sana kuhusu kuporomoka kwa maadili, dalili za kusambaratisha umoja wetu, sasa haya ni mambo ya msingi na kama nilivyosema Rais mwenyewe alikwishayatambua.”

Jaji Warioba alisema hawaoni kosa walilofanya kuzungumzia masuala ya kitaifa kiasi cha kumfanya Makamba atukane na kwamba msimamo wa Makamba ni tofauti na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alitoa mfano kwa kurejea hotuba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumzia hatari ya kuongezeka pengo kati ya masikini na matajiri nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwenya kumbukumbu ya miaka 75 ya Kanisa Anglikana, Dar es Salaam.

“Mgeni rasmi ilikuwa awe Waziri Mkuu lakini kwa bahati mbaya akawa amesafiri kwenda Vienna kwa hiyo akamtuma Waziri Marmo (Philip Marmo) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-(Bunge) kusoma hotuba yake, ilikuwa ni hotuba ya Waziri Mkuu iliyosomwa na Waziri Marmo.

Na sehemu ya hotuba hiyo inasema ifuatavyo; “Kama nilivyoeleza Tanzania ina watu wapatao milioni 40. watu hawa wana viwango tofauti vya mapato na hili linaeleweka. Hatuwezi kuwa na mapato sawa.

“Tatizo linakuja pale ambapo tofauti ya kipato inapokuwa kubwa miongoni mwa makundi katika jamii. Lakini tatizo hili linazidi kuwa kubwa pale ambapo tofauti ya kipato inapokuwa kubwa miongoni mwa makundi katika jamii.

“Lakini tatizo hili linazidi kuwa kubwa pale ambapo ukubwa wa tofauti hiyo unapoongezeka. Madhara ya ongezeko hilo mnayafahamu kwani kuna hatari ya matajiri wachache kuendesha maisha ya maskini walio wengi kwa njia ambayo itazidi kuwaongezea utajiri huku ikiwadidimiza zaidi maskini.

“Si ajabu matajiri hao wachache wakawa ndio wanaoendesha vyama vya siasa, Serikali, Mahakama, Bunge, Makanisa, Misikiti n.k. Katika hali hiyo Taifa halina usalama.

“Hivyo hatuna budi kuwa na misingi inayopunguza tofauti kati ya masikini na tajiri. Kama Serikali tunazo njia mbalimbali tunazotumia kupunguza tofauti hiyo. Lakini ninaamini madhehebu ya dini nayo yana jukumu la kufanya.

“Licha ya kuchukua tahadhari yasiendeshwe kwa matakwa ya matajiri hao, wanalo jukumu la kuona na kuhakikisha kuwa vyanzo vya utajiri wa waumini wao ni vya haki na havitokani na mapato haramu au kuvunja amri za Mungu.

“Hivyo, ningependa kuwaomba viongozi wa dini kushirikiana na mihimili yote ya dola ili kupunguza kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya matajiri na maskini kwa kuwa mwisho wake si mwema,” alihitimisha kunukuu hotuba ya Waziri Mkuu na kuendelea kusema:

“Sasa haya maneno hayana tofauti kabisa na yale yaliyozungumzwa katika kongamano. Tulichoona hapa ni kwamba Serikali kama serikali inasikiliza ushauri. Rais amewahi kuyasema na Waziri Mkuu anayasema.

“Na kongamano lilikuwa linaishauri Serikali, kama Serikali haina tatizo na hayo yaliyosema huko, mheshimiwa Makamba ana matatizo gani mpaka atutukane kwamba sisi ni wehu na wahuni.

“Uongozi ni kuonyesha njia, mheshimiwa Makamba ni kiongozi wa ngazi ya juu katika chama ndiye mtendaji mkuu na ukiwa kiongozi mwenye madaraka lazima uchunge lugha yako.

“Rais pamoja na cheo chake anaheshimu sana watu, anatuheshimu sana sisi wazee hatutukani, hatubezi hata pale ambapo tunatofautiana mawazo, Rais anatuheshimu sana nasi tunamheshimu.”

Source:www.raiamwema.co.tz

No comments: