Wednesday, September 30, 2009

Pinda akataza ununuzi wa magari ya kifahari


WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewaagiza watendaji wa Serikali watafute namna ya kupunguza matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na kutonunua magari ya kifahari.

Amewataka watendaji hao wabadilike, waache ubinafsi, na wasijifikirie wao tu, kuna mamilioni ya watanzania wanaohitaji fedha kidogo zilizopo.

Waziri Mkuu ametoa mfano kuwa, katika Wizara za Serikali kuna magari mengi ya aina ya Toyota Land Cruiser VX yanayouzwa kati ya Sh milioni 160 hadi 220 na kwamba Tanzania sin chi ya neema kiasi cha kutaka ufahari kiasi hicho.

“Watanzania hembu tubadilike, kuna watu kule chini wanahitaji hizi fedha kidogo tulizonazo” amesema Waziri Mkuu.

Pinda amesema, Serikali isiponunua magari hayo ya kifahari kwa miaka miwili au mitatu maisha ya watanzania yatabadilika kwa kuboresha kilimo na sekta ya mifugo.

Waziri Mkuu amesema, kuna mtazamo usio sahihi miongoni mwa watumishi wa Serikali, viongozi ni wabinafsi, na kwamba, wanajifikiria wao tu.

“Lakini mindset za watanzania bado bado kweli kweli” amesema Waziri Mkuu mjini Dodoma, wakati anafungua mkutano wa siku tatu wa Watendaji wa Serikali na wadau wa sekta ya mifugo.

Sitta ajitoa mhanga kumaliza ufisadi

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, ametangaza rasmi kuwa amejitoa mhanga kupambana na ufisadi ili nchi isiangamie.

Sitta amesema, ufisadi nchini ni wa kiwango cha juu hivyo yeye na baadhi ya wabunge wameamua kujitoa mhanga kupambana nao, na hawafanyi mzaha.

Amesema, ufisadi unatisha Tanzania, na kwamba, mafisadi wanaiangamiza nchi.

“Nyinyi vijana mnakua wakati wa mikataba hii mibovu mimi naweza kuwa nimeshakufa kwa wakati huo, ndio maana baadhi ya watu wakiwemo baadhi ya wabunge wanachukia rushwa,” Sitta amewaeleza waandishi wa habari leo mjini Arusha.

Rais huyo wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola amesema, gharama za ufisadi nchini zinaweza kuambukiza vizazi vijavyo.

“Rushwa ni tatizo kubwa katika bara letu la Afrika, wala rushwa wanatumia utajiri wao kuingia kwenye siasa huku wakiwa na nguvu kubwa ya kiuchumi,” amesema Sitta.

Ametoa mfano wa ufisadi huo nchini kuwa ni viongozi wa Serikali kusaini mikataba feki itakayoliingiza taifa kwenye gharama kubwa siku zijazo. Amesema,Tanzania itaonja machungu ya gharama hizo kupitia madeni.

“Sasa tunatumia kama asilimia 35 ya bajeti kwa ajili ya kulipia madeni ya nje; lakini kuna uwezekano wa kufikia asilimia 50 kama tutaendelea kuingia mikataba feki na ikifikia hapo tumekwisha.

“Ufisadi umefikia hatua ya juu ndio baadhi yetu hatufanyi utani na tumeamua kujitoa mhanga kupambana dhidi ya wahusika wa ufisadi huo.

Kwa mujibu wa Sitta, mwaka jana Afrika ilipoteza takribani dola za marekani bilioni 20 kutokana na vitendo vya ufisadi. “Kiasi hiki ni kikubwa kwani ni zaidi ya msaada ambao bara hili linapata, hii ni hatari kubwa.

Sitta amesema, mkutano huo wa CPA utalijadili suala hilo la ufisadi wakati watakapokuwa wanajadili moja ya mada zitakazowasilishwa.

Amesema, rushwa ni chanzo cha migogoro mingi Afrika kwa kuwa watu wachache wana utajiri walioupata kwa njia ya rushwa, wananchi wengi ni masikini.

Kwa mujibu wa Sitta, watu wamekuwa wanakasirishwa na ustawi huo kwa watu wachache na hivyo kuwa chanzo cha mapigano na migogoro isiyokwisha katika baadhi ya nchi.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, kitendo cha watu wachache kumiliki uchumi na kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa kunasababisha watu wengi wawe masikini.

Katika mkutano huo baadhi ya mada zitakazojadiliwa ni Serikali ya mseto, majukumu ya Bunge katika kutoa habari kwa jamii, na mabadiliko ya hali ya hewa.

Friday, September 25, 2009

Gadaffi ataka Afrika ilipwe fidia

RAIS wa Libya Muammar Gadaffi, amesema, wakoloni walioitawaka Afrika waliiba rasilimali na malighafi hivyo bara hili linastahili fidia ya dola za Marekani trilioni 7.7.

“Umefika wakati kwa nchi za Afrika kulipwa fidia kutokana na wingi la rasilimali zake kuibiwa katika miongo mingi iliyopita wakati wa utumwa na utawala wa kikoloni,” amesema Gadaffi leo katika mkutano wa Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Mwenyekiti huyo wa Umoja wa Afrika (AU) amezikosoa nchi tajiri duniani zinazoendele kutawala kwa mbinu mbalimbali.

Amesema, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Urusi zina nguvu kubwa na mamlaka dhidi ya mataifa zaidi ya 190.

“Wanachama wote wa UN wanatakiwa kuwa sawa, lakini kuna baadhi ya nchi zimejitwalia kinachoitwa nguvu na kutawala nchi zingine,” amesema.

Gadaffi amesema, yanahitajika mabadiliko UN yakiwemo ya mfumo ili kubadilisha tabia ya baadhi ya nchi kuwa na haki ya kutawala na kuzionea nchi nyingine.

Kiongozi huyo ametaka kuwe na demokrasia katika Baraza la Usalama la U, N na kwamba, Afrika inastahili kuwa na angalau kiti ndani ya baraza hilo.

Ameshauri Makao Makuu ya UN yahamishwe kutoka New York, yawe katika eneo ambalo ni la katikati kama vile Geneva, Uswisi.

“Kwa nini baadhi ya wajumbe walazimike kusafiri kwa zaidi ya saa 20 kwenda Makao Makuu. Wakifika hapa wanakuwa wamechoka hata kufanyakazi na wanaishia kulala badala ya kuchangia majadiliano,” amesema Gadaffi.

Awali, Rais wa Brazil Louis Ignacio Da Silva, alitaka kuwapo kwa ushirikiano wa uchumi na kijamii ili kuleta maendeleo ya sawa katika maeneo yote duniani.

Amesema,UN inahitaji mfumo mpya iweze kukabiliana na changamoto za karne ya 21 katika maeneo ya uchumi, siasa, na kijamii.

Wakatoliki wapuuza

KANISA Katoliki nchini limepuuza makaripio na kejeli zinazotolewa na wanasiasa na baadhi ya viongozi wa dini nyingine kuhusu waraka wao unaozungumzia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Raia Mwema limebaini.

Kwa wiki mbili sasa, Raia Mwema limebaini kwamba kila baada ya sala katika makanisa yote Katoliki nchini, viongozi wa Kanisa hilo wamekuwa wakiwatangazia waumini wake ambao hawajaupata waraka huo kuununua nje ya makanisa hayo.

Maeneo ya nje ya makanisa yote ambako huuzwa maandiko ya kiroho, rozali na vitu vinginevyo kumekuwapo na vijitabu hivyo vya waraka ambavyo vimeendelea kuuzwa kwa wingi kuliko ilivyokuwa awali kabla ya makemeo kutolewa.

Joseph Ibreck, Mwenyekiti wa Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania (CPT), ambacho ndicho kilichochapisha waraka huo ameiambia Raia Mwema wiki hii kwamba wao wanaendelea kuchapisha na kusambaza waraka huo bila kujali wanaopinga.

Ibreck amesema kila siku mahitaji ya warakara huo uliogawanywa katika vijitabu vitatu yamekuwa makubwa na wamekuwa wakiendelea kuchapisha na kusambaza nchi nzima na hivi karibuni walichapa nakala zaidi ya 7,000.

Miongoni mwa walioonekana kutoridhishwa na waraka wa Wakatoliki ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na mwanasiasa mkongwe ambaye amekuwa karibu na watawala kwa muda mrefu, Kingunge Ngombale-Mwiru.

Akijibu maswali ya wananchi moja kwa moja kupitia televisheni na redio, Rais Kikwete alisema matamko ya kidini yanayohusu uchaguzi ujao yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa dini yamemshitua na ameamuru kuanzia sasa asiwepo kiongozi mwingine wa kidini atakayetoa matamko ya namna hiyo.

Lakini kiongozi mmoja wa Kanisa Katoliki, ameliambia Raia Mwema wiki hii kwamba kwa sasa wameamua kufunga mjadala wa suala hilo na watawapuuza wote wanapingana nao kwa kuendelea kuusambaza kwa nguvu nchi nzima.

Akijibu moja ya swali liloulizwa Rais Kikwete alisema hatua hiyo ya viongozi wa kidini ya kutoa matamko ni jambo ambalo sio la kawaida kwani yanawataka Watanzania waende kwenye uchaguzi wakiangalia wagombea wa dini zao na sio Utanzania wao, maelezo ambayo yanapingwa na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini.

Rais Kikwete alibainisha kwamba suala hilo limejadiliwa hata ndani ya vikao vya CCM hususan Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC) iliyokutana mjini Dodoma hivi karibuni akisema:

"Hili tumeliona kwenye kikao cha NEC, tukaona halituweki kwenye mwelekeo mzuri, Taifa hili waasisi wake wamelijenga si kwa kutazamana dini, rangi au kabila bali Utanzania."

Soma zaidi

Thursday, September 24, 2009

Waliomuua albino kunyongwa

MAHAKAMA Kuu Tanzania wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, leo imewahukumu kifo wanaume watatu waliopatikana na hatia ya kumuua mtoto albino wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 14.

Jaji Gabriel Lwakibalira amewahukumu washitakiwa hao kwenda jela na wanyongwe hadi wafe.

Masumbuko Madata (32) mkazi wa Itunga, Emmanuel Masangwa (28) wa Bunyihuna na Charles Kalamuji ‘Charles Masangwa’ (42) wa Nanda, Bukombe , wamepatikana na hatia ya kumvamia, Matatizo Dunia,wilayani Bukombe mkoani Shinyanga wakamkata miguu.

Kwa mujibu wa Jaji Lwakibalira, mahakama imeridhishwa na ushahidi wa mashahidi 15 katika kesi hiyo ya mauaji namba 24 ya mwaka 2009 hivyo washitakiwa hao wanastahili kunyongwa.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban saa moja, Jaji Gabriel Rwakibalila, amesema, mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa kuwa washtakiwa hao watatu walikula njama na kufanya mauaji hayo usiku wa kuamkia Desemba mosi mwaka jana, katika Kijiji cha Bunyihuna, Bukombe.

Jaji Rwakibalila awali alisema ushahidi wa upande wa utetezi uliotolewa mahakamani hapo ulionesha kuwa washtakiwa hawakuwapo, lakini ni utetezi huo huo ulioonesha kuwa ushahidi wao ni wa kweli na ndio waliokula njama na kufanya mauaji hayo.

Amesema, dosari ndogondogo zilizooneshwa na upande wa mashitaka haziharibu mashitaka yaliyokuwa yanawakabili washitakiwa hao.

Baadhi ya dosari ni ushahidi wa idadi ya askari na magari yaliyofika eneo la tukio.

Amesisitiza kwamba, ushahidi wa upande huo unatosha kuwatia hatiani washitakiwa hao na kustahili adhabu hiyo.

Kuhusu ushahidi wa Mkemia Mkuu wa Serikali alisema nao ulionesha kuhusika kwa mshitakiwa wa kwanza, Madata na wa tatu Kalamuji katika mauaji hayo, hasa baada ya kupatikana kwa vinasaba ambavyo damu ya miguu yote miwili ya albino Dunia ilipochukuliwa, iligundulika kuwa na vinasaba hivyo.

Jaji Rwakibalila alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ulionesha jinsi washtakiwa wote watatu walivyoshiriki katika mauaji hayo na ndiyo maana mahakama ikawatia hatiani.

“Mshtakiwa wa kwanza, Masumbuko Madata, mshtakiwa wa pili Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji au Charles Masangwa, nyote kwa pamoja mmepatikana na kosa la mauaji, hivyo mahakama inawahukumu kunyongwa hadi kufa na mnaweza kukata rufaa kama hamridhiki,” alihitimisha kusoma hukumu hiyo.

Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa, upande wa utetezi ulidai kuwa utakata rufaa Mahakama ya Rufaa.

Kesi nyingine za mauaji ya albino zinaendelea katika Mahakama Kuu Kahama na Shinyanga. Wakili kiongozi wa upande wa utetezi, Kamaliza Kayaga, alisema hawakuridhika na hukumu na kwamba kazi yao ni moja ya kukata rufaa.

Hii ni hukumu ya kwanza kutolewa nchini dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya albino tangu kuibuka kwa vitendo hivyo kwa imani za kishirikina na kusababisha vifo vya zaidi ya albino 50 nchini.

Mwanafunzi abakwa, anyongwa Tabora

WATU wasiojulikana wamembaka na kumyonga mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Kanyenye, mkoani Tabora.

Watu hao walimbaka binti huyo, Pili Kapusha, Jumamosi wakati amekwenda kuchota maji kisimani.

Walimvamia, wakambaka, na kisha kumnyonga jirani na kisima cha maji.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Emmson Mmari, amesema, mama mzazi wa binti huyo aliposubiri na kuona mwanawe harudi nyumbani aliamua kwenda kisimani kumfuata.

Kamanda Mmari amesema, alipofika kisimani alikuta ndoo zina maji na wakati anamtafuta alimuona ameuawa na kutupwa kwenye shimo jirani na kisima hicho kwenye kata ya Itetemya.

Amesema, ripoti ya daktari inaonyesha kuwa binti huyo alibakwa kabla ya kunyongwa.

Tuesday, September 22, 2009

Balozi zashituka Sitta kuandamwa

-Wa Sweden aenda hadi ofisi za CCM
-Msekwa aziandikia waraka kuzipoza
-Akiri NEC ilikosea taratibu

BAADHI ya balozi nchini zimefuatilia taarifa za kikao kilichopita cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichotafsiriwa kuwa kililenga kuziba midomo ya wabunge, ili kujiridhisha na usalama wa fedha zao zinazokuja Tanzania kwa njia ya msaada wa kibajeti, Raia Mwema imeambiwa.

Hatua hiyo ya ufuatiliaji, taarifa zinasema, imechagizwa na hoja kwamba kama ni kweli kwamba chama tawala kiliwaonya wabunge wake wapunguze kelele dhidi ya Serikali na hivyo kuua uhuru wa Bunge na mbunge mmoja mmoja wa kuikosoa, basi kazi muhimu ya Bunge na wabunge ya kuisimamia Serikali, itakuwa hatarini.

Taarifa kutoka kwa maofisa wasaidizi wa baadhi ya balozi hizo, zinaeleza ya kuwa baadhi ya mabalozi wamepelekewa waraka maalumu ulioandikwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, kwa lengo la kueleza kwa ufasaha kile kilichojiri katika kikao cha NEC cha mwezi uliopita mjini Dodoma.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mmoja wa balozi zilizopelekewa waraka huo wa Msekwa ni wa Sweden, ambao Balozi wake alifika Ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam kwa ajili ya mazungumzo hayo na masuala mengine ya kisiasa, hatua ambayo imethibitishwa na ubalozi wa Sweden nchini, ingawa pia ubalozi huo umesisitiza kuwa hayo yalikuwa mazungumzo ya kawaida kuhusu masuala ya kisiasa nchini.

‘‘Ni kweli (Balozi Staffan HerrstrĖ†m) alikwenda CCM Lumumba. Na walifanya mazungumzo kuhusu masuala ya kisiasa. Huu ni utaratibu wa kawaida,’’ alisema katibu muhtasi Doris Lema, akikariri majibu ya Balozi kwa maswali ya Raia Mwema juu ya safari yake ya ofisi za CCM.

Katika hatua nyingine, Raia Mwema imefanikiwa kupata nakala ya waraka wa Msekwa kwa balozi kadhaa zinazoifadhili Tanzania ambao, pamoja na mambo mengine, unazungumzia yaliyojitokeza katika kikao hicho cha NEC, akionyesha upungufu katika taratibu za kumjadili Spika Samuel Sitta na kasoro miongoni mwa wabunge wa CCM wanaojitambulisha kuwa ni wapambanaji wa vita dhidi ya ufisadi.

Katika maelezo yake, Msekwa anatoa ufafanuzi katika maeneo makuu matatu aliyoyaweka kwenye mtindo wa maswali, jambo la kwanza likiwa ni “Mjadala kwenye NEC umehoji uendeshaji wa Bunge, hatua ambayo ni uvunjaji wa kifungu cha 100 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?”

Jambo la pili: “Ni sahihi kwa NEC-CCM kujadili mwenendo wa wabunge wake ndani ya Bunge, akiwamo Spika? Kwa maneno mengine, kitendo hicho kinavunja sheria ya mamlaka na haki za Bunge? Pili: “Spika amekabwa kwenye kikao hicho kwa sababu ya kuwa mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya mafisadi? Kabla ya kutoa ufafanuzi wa kina katika maeneo hayo, Msekwa anaeleza; “ jibu kwa kila swali ni hapana.”

Anasema katika waraka huo ya kuwa NEC ina wajibu wa kujadili mwenendo wa viongozi wake ingawa katika kikao cha Dodoma utaratibu wa chama hicho kumlalamikia kiongozi au mwanachama mwingine yeyote haukuzingatiwa.

“Kifungu cha 108 cha Katiba ya CCM kinaeleza majukumu ya jumla ya mikutano ya NEC, na kifungu kidogo chake cha nane kinaeleza kudumisha uangalizi juu ya vitendo vya wanachama na viongozi wa CCM, hii maana yeke ni kudhibiti mwenendo na vitendo vya wanachama na viongozi wake.

“Kuingilia mambo ya Bunge ni makosa, lakini umma unajua kuwa kumekuwa na makundi hasimu miongoni mwa wabunge kuhusu vita dhidi ya ufisadi, wapo wanaopinga ufisadi na wengine wanaopuuza vita hiyo. Spika alikosolewa kwa kushindwa kuendesha mijadala bila kuzingatia maslahi ya chama, na wabunge wamekosolewa kwa kushindwa kutumia kamati ya wabunge wa CCM,” anasema Msekwa.

Hata hivyo, pamoja na kuonyesha kuamini kuwa kulikuwa na nafasi kwa Spika kuendesha mijadala kwa kutazama maslahi ya chama na pia NEC kuwa na wajibu kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho kufuatilia na kuhoji mienendo na vitendo vya wanachama na viongozi wake, Msekwa anasema makosa yalifanyika ndani ya NEC.

“Kitendo hicho cha NEC kinaweza kuwa ni makosa. Ingawa kujadili mwenendo wa Spika na baadhi ya wabunge wengine wa CCM kinaweza kutetewa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, lakini pia kuna makosa yamefanyika na hasa kwa upande wa kuzingatia taratibu na kanuni za chama.

“CCM imekuwa na utaratibu na kanuni nzuri kwa viongozi wake wanaolalamikiwa mwenendo wao kwamba wamekiuka kanuni na maadili ya chama. Sheria na kanuni hizo zinaeleza kuwa kiongozi anayetuhumiwa anapaswa kupelekewa orodha ya tuhuma zake na kupewa fursa ya kuzijibu.

“Na baada ya hapo, Kamati ya Maadili ya CCM inakutana kwa ajili ya kuchambua suala hilo na kufanya uamuzi na pia kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu (NEC). Kwa hiyo inaridhiwa kuwa taratibu za kisheria hazikufuatwa katika suala hili,” anaeleza Msekwa katika waraka wake huo wenye kurasa 11.

Anaongeza:“Ni vizuri ikaeleweka kwamba katika utamaduni wa siasa za vyama vingi umuhimu ni lazima uwekwe na kudhibitiwa ndani ya chama cha siasa, hususan suala la nidhamu. Na uhai wa chama chochote cha siasa ni umoja na nidhamu.’’

Katika hatua nyingine, Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini (UN), Alain Noudehou, amewasifu Rais Jakaya Kikwete na Spika Sitta kwa kazi nzuri ya Rais Kikwete kuruhusu uhuru wa kuzungumza ikiwa ni pamoja na kutoa fursa kwa Watanzania kumuuliza maswali ya papo kwa papo.

Akizungumza, jana, Jumanne, kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Mwakilishi huyo wa UN alimsifia Sitta kwa mpango wake wa kuendesha Bunge vyema katika wajibu wake wa usimamizi wa Serikali.

Source:www.raiamwema.co.tz

Thursday, September 17, 2009

Tanesco kumekucha

OFISI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanza kuchunguza tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ikiwa ni pamoja na kufahamu namna lilivyotumia mkopo wa sh bilioni 280.

Wabunge wametuhumu shirika hilo wakidai kuwa kuna ubadhirifu ukiwamo ukarabati wa nyumba zake kwa gharama kubwa na kupanga kuwauzia wakurugenzi wake kwa bei nafuu.

Ofisi ya CAG imeanza kukagua hesabu za Tanesco ili kufahamu pia kama shirika hilo lilitumia ipasavyo Sh bilioni 280 lilizokopa katika benki za nchini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco, Peter Ngumbulu, alisema jana kuwa, tayari taarifa zote za matumizi zimeshapelekwa kwa CAG kwa ukaguzi huo.

“Mimi nilikuwa safarini lakini kwa mujibu wa taarifa nilizopata, CAG ameshapelekewa nyaraka zote alizozitaka na ameshaanza ukaguzi wa mahesabu,” alisema.

Alipoulizwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika lini alisema “siwezi kufahamu lakini wakishamaliza, taarifa zitatolewa na ni vizuri ukawauliza Tanesco wakueleze kiundani juu ya nyaraka zilizoombwa na CAG”.

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovic Utouh, amekiri kwamba ofisi yake imeanza ukaguzi huo.

“Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco ilitupa kazi hiyo tuifanye na wakatupa hadidu za rejea ambazo tutazifuata, lakini hadidu hizo muulize Mwenyekiti wa Bodi mwenyewe atakueleza.

Kwa mujibu wa Utouh, kazi hiyo ya ukaguzi waliianza wiki mbili zilizopita lakini hakusema itakamilika lini.

Wakati wa mkutano wa 16 wa Bunge uliojadili Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Nishati na Madini, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), alieleza kuwa Tanesco ilitumia Sh bilioni 1.4 kukarabati nyumba zake saba, huku moja ikitumia Sh milioni 600 na ikitarajiwa kuuzwa kwa asilimia 10 ya gharama - Sh milioni 60.

Alizitaja nyumba hizo kuwa ziko Oysterbay na Masaki na thamani ya ukarabati kwenye mabano kuwa ni ya barabara ya Chole (Sh milioni 600); Guinea 24 (Sh milioni 258.4); Laibon 65 (Sh milioni 190); Mawenzi 454 (Sh milioni 138); Guinea 93 (Sh milioni 88.5); Toure Drive 315 (Sh milioni 79) na Uganda Avenue 98 (Sh milioni 73.6).

Mwenyekiti wa Bodi alikiri kutofahamu jinsi Sh bilioni 1.4 zilivyotumika kukarabati na mpango wa kuwauzia nyumba hizo wafanyakazi wake wa ngazi za juu.

Kuhusu mkopo wa Sh bilioni 280 ambao ilikopa kutoka benki za nchini ambazo wabunge walidai zimetumika vibaya, Ngumbulu amesema: “Fedha hizo naamini zimetumika vizuri kama ilivyopangwa kwani hata benki zenyewe ni wakali na wanafuatilia.

“Fedha hizo zimetumika kuliweka sawa shirika kama kulipia madeni yake na ukarabati mbalimbali lakini taarifa za matumizi yake naomba waombe Tanesco”.

Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa kuhusu matumizi ya fedha hizo na taarifa walizompa CAG, alisema: “Tusubiri uchunguzi ukamilike, kwa sasa siwezi kuzungumza lolote, Wizara ya Nishati na Madini itatoa taarifa ya uchunguzi kama ilivyoahidi”.

Wakili awakaanga Mramba na Mgonja

MKATABA uliosainiwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu Daudi Ballali kwa niaba ya BoT na kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Coporation ulikiuka taratibu za manunuzi ya Serikali.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, amedai mahakamani leo kuwa, Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hawakuupitia mkataba huo kabla yakusainiwa.

Manyanda ametoa madai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akisoma maelezo ya awali ya mashitaka ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya sh bilioni 11.7.

Kesi hiyo inawakabili aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gray Mgonja, na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona.

Manyanda alilieleza jopo la makimu wakiongozwa na Hakimu John Utamwa,kuwa, Mkuu wa kitengo cha masuala ya sheria, Godwin Nyelo, alimshauri Yona kutoingia mkataba na kampuni hiyo kwa kuwa ulikuwa unakiuka taratibu za zabuni.

Alidai kuwa, ushauri huo ulipuuzwa, makubaliano ya awali yaliandaliwa na kwamba, vipengele vya 4 na 5 vya mkataba huo vilikuwa vinazungumzia msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Imedaiwa mahakamani kwamba, Mei 26 mwaka 2003 Ofisa udhibiti wa fedha alitoa ushauri kwamba Wizara ipate ushauri kwa TRA ili kuona kama kampuni hiyo ilistahili kusamehewa kodi.

Kwa mujibu wa Manyanda,ofisa huyo alipeleka dokezo hilo kwa Mkurugenzi wa masuala ya ya kisheria Wizara ya Fedha akisisitiza ufanywe uchunguzi mpya kuhusu vipengele vilivyokuwa vikizungumzia msamaha wa kodi.

Mahakama ilielezwa kwamba,wakati ushauri wa TRA ukisubiriwa,yalifanywa marekebisho kwenye mkataba na ulisainiwa Septemba 18,2003.

Manyanda amesema, Balali alisaini mkataba huo kwa niaba ya BoT, Erwin Flores alisaini kwa niaba ya kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Coporation, na kwamba, kipengele cha msamaha wa kodi hakikufutwa.

Manyanda alidai kuwa Mramba alimuandikia Mgonja kuwa utaratibu wa makubaliano kati ya kampuni hiyo na BoT ulikiuka sheria na taratibu za nchi, hivyo akaomba ushauri wa namna ya kuidhinisha msamaha wa kodi.

Imedaiwa kwamba, Wizara ya Nishati na Madini iliandika barua Wizara ya Fedha kupitia kwa Mgonja kwa niaba ya kampuni hiyo ikiiomba msamaha wa kodi.

Mahakama imeelezwa kwamba, Mramba alitoa idhinisho la msamaha wa kodi kwa kusaini katika matangazo ya Serikali baada ya Mgonja kumuomba afanye hivyo.

Wakili amedai kuwa, matangazo hayo yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa TRA ya kuwa kampuni hiyo haikustahili msamaha wa kodi.

Washitakiwa hao wanadaiwa waliruhusu kutolewa kibali cha serikali kilichoisaidia kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Gorvement Bussiness Corporation kutolipa kodi tofauti na mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA).

Inadaiwa kuwa, uamuzi huo uliisababishia serikali hasara ya sh 11,752,350,148.00 kati ya mwaka 2002 na Mei2005.

Wednesday, September 16, 2009

Vigogo wanne wa benki kuu wafikishwa mahakamani


VIGOGO wanne wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na shtaka la Uhujumu Uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh 104 bilioni.

Vigogo hao ambao wote ni wakurugenzi wa BoT wa vitengo tofauti, walifikishwa mahakamani hapo asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Wameshtakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002.

Wakurugenzi hao wanashtakiwa kwa makosa tofauti ikiwamo kosa la tatu linalowahusisha wote wanne ambao ni Mkurugenzi wa Benki ya BoT, Simon Eliezer Jengo, Naibu Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo Kisima Thobias Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Bosco Ndimbo Kimela na Mkurugenzi wa benki, Ally Farijallah Bakari.

Mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Benny Lincon alimwambia hakimu Samuel Maweda kuwa vigogo hao wanne, wakiwa watumishi wa umma walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti na kuisababishia serikali hasara ya Sh104,158,536,146.

“Kwa pamoja na kwa makusudi walishindwa kuchukua tahadhari au kusahau majukumu yao katika mazingira nyeti, kwa udanganyifu walitayarisha nyongeza kwenye mkataba wa 2001 unaohusiana na uchapaji wa noti za benki kwa gharama kubwa ambapo bei ya mkataba huo iliisababishia serikali hasara ya Sh104,158,536,146,” alidai Licon.

Licon aliendelea kuieleza mahakama kuwa mwaka 2004 washtakiwa Jengo na Mkango wakiwa ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam na wakiwa wameajiriwa katika utumishi wa umma katika nyadhifa tofauti ndani ya BoT, kwa pamoja na kwa makusudi, wakiwa na lengo la kuvunja kanuni walitangulia kutoa ofa kwa wasambazaji wa noti za benki.Pauline Richard na Salim Said.

Friday, September 11, 2009

Wazungu wakejeli Serikali ya Kikwete



-Wasema posho zawapofua watendaji
-Wasema inajali wawekezaji kuliko raia

SURA ya Tanzania katika duru za kimataifa imeanza kuchafuka na sasa vyombo vya habari, hususan magazeti barani Ulaya, yameanza kuielezea Tanzania katika tafsiri ambayo ni kinyume cha juhudi za maofisa wa serikali kuinadi kwa madhumuni ya kuvutia zaidi wawekezaji.

Miongoni mwa mambo yanayoandikwa na vyombo hivyo yakiwamo magazeti ya The Guardian, Economist na Financial Times, ni pamoja na urasimu unaokwaza wawekezaji, maofisa wa serikali kupenda posho, serikali kukumbatia wawekezaji dhidi ya wananchi katika baadhi ya maeneo na kusuasua kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki.

Magazeti hayo yamechapisha taarifa kuhusu Tanzania katika matoleo yake ya hivi karibuni kati ya Julai na Septemba mwaka huu likiwamo gazeti la Financial Times lililonukuu maofisa wa kampuni moja ya uwekezaji iliyokusudia kujenga kiwanda cha dawa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari iliyoandikwa na gazeti hilo, inaelezwa kuwa wakati Kamal Kotecha alipoanza mazungumzo ya kujenga kiwanda cha dawa mjini Dar es Salaam ambacho kingezalisha dawa bora na kukuza uchumi, mamlaka zilimhakikishia kwamba dawa hizo zingeidhinishwa ndani ya miezi mitatu.

Leo, zaidi ya mwaka mmoja na nusu na uwekezaji wa dola za Marekani milioni 13, Kotecha bado anasubiri kibali hicho kutoka.

“Huwezi kuwaona maofisa au kupata uamuzi. Siku zote wako katika mikutano,” analalama Kotecha, mfanyabisahara Mhindi ambaye amepata kuishi Jamhuri ya Kongo (DRC) mmiliki wa Zenufa Pharmaceuticals.

Anaongeza: “Unaweza kusema ofisi zetu ziko kwa msajili, kwa kuwa kila siku tuna mtu kati yetu anayekwenda katika ofisi yake (kufuatilia).

“Katika Tanzania, moja ya nchi ya Afrika yenye afueni kidogo katika muundo wa sekta ya utendaji, tatizo si rushwa pekee. Ni aina ya mfumo ambao umekuwa kama taasisi, yaani taratibu za kisheria ambazo huchelewesha muda, ambao umehalalishwa na wafadhili na mashirika ya kimataifa. Lakini pengine chimbuko la hali hii ni utamaduni wa malipo ya posho (per diem)”.

Malipo ya kila siku kwa maofisa wanaohudhuria mikutano na warsha yanayolenga kulipia gharama za safari, chakula na malazi.

Mtumishi mmoja wa Serikali aliimbia kampuni ya Zenufa kisa cha kampuni hiyo kusubiri kibali kwa mwaka na nusu.

Alisema, ya kuwa msajili wa cheo cha chini hupata mshahara wa dola za Marekani 600 (takriban shs 72,000) kwa mwezi lakini akisafiri au akiwa mkutanoni hupata dola 50 (sh zaidi ya 50,000) za Marekani. Msajili mwandamizi hupata mshahara wa dola za Marekani 2,000 au posho ya siku ya dola 200 za Marekani akiwa katika mikutano na kuongeza;

“Ndiyo maana hawashikiki ofisini. Hali hii ni habari ya kawaida. Msomi mmoja alilipwa posho ya kikao kilichofanyika mita chache kutoka ofisini kwake. Alipohoji ni za nini aliambiwa za mafuta, aliposema kwake ni jirani, akaambiwa wasipolipa hakuna atakayehudhuria. ”

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mdudu huyu wa posho haishii serikalini tu bali mashirika yasiyo ya kiserikali nayo yanachangia na hayo hualika wataalamu kutoka serikalini na kuwapa posho nono huku wakwavunja moyo wanaobaki ofisini.

Klaus Leisinger, mkuu wa Novartis Foundation, shirika la misaada la Uswizi alipata mara kadhaa kuomba kufadhili kituo cha mafunzo ya afya (Tanzanian Training Centre for International Health) akajikuta akiambulia patupu.

Anasema: “ Ilikuwa vigumu kuanzisha malengo makubwa kwa kuwa wafanyakazi walikuwa wakilipwa mishahara ambayo ilikuwa lazima ichangiwe na posho za vikao na safari”.

Nalo gazeti la Economist, Septemba 3, mwaka 2009, limeripoti kuhusu kusuasua kwa Tanzania kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki kwamba, Uganda imepata kupitia mapinduzi na hata wakati mgumu wakati wa utawala wa Milton Obote, yote yakijidhihirisha katika umwagaji mkubwa wa damu wakati wa utawala wa Idi Amin, na vipindi virefu vya ukiukwaji wa haki za raia.

Gazeti hilo limeeleza kwamba chini ya Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Tanzania ilichukua siasa ya ujamaa iliyowafanya watu wake wajikokote katika umasikini lakini wakabaki na mshikamano na amani na Kenya ilishamiri kuendana na dunia, lakini yenyewe ikijidhihirisha kwa matendo ya ukosaji amani na rushwa. Sasa Kenya inaweza kuwa isiyo na utulivu kulinganisha na majirani zake.

Kwa mujibu Economist mwaka 1967 Kenya, Tanzania na Uganda ziliunda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa nia kuanzisha shirikisho lakini hakukuwa na maendeleo ya maana kabla ya jumuiya hiyo kuvunjika mwaka 1977, huku baadhi ya Wakenya wakishangilia, wakifurahi kwamba nchi yao ilikuwa ikiwabeba sana wanachama wengine wa jumuiya.

Hata hivyo, mwaka 1999, mpango huo ulifufuliwa na mwaka 2007 ulipanuka kuzijumuisha Burundi na Rwanda na sasa linaeleza gazeti hilo kwamba wengi wana shaka kama Umoja wa aina ya ule wa Ulaya unaweza kufikiwa katika eneo hili hata kama kuna ahadi ya kuwa na sarafu moja ifikapo mwaka 2015 ili kuwezesha muungano wa forodha kufanya kazi.

Hata hivyo linaeleza kwamba matukio ya hivi karibuni yanaashiria kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa na shirikisho lakini Tanzania ndiyo ambayo mara nyingi imekuwa ikikwamisha mambo yasiende katika EAC, ikihofia kufunikwa na Wakenya na Waganda watafuta ardhi na ambao wanaaminika kuwa na elimu zaidi kulinganisha na Watanzania.

Lakini Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, sasa anasema hakuna sababu kwa Watanzanua kuendelea kulialia, bali wajiandae kuingia katika soko la pamoja.

Soko la Mitaji Tanzania, ambalo ni dogo, linaamini katika miaka michache ijayo patakuwa na soko la pamoja la Afrika Mashariki. Kazi si mbioni ya kuanzisha mfumo wa biashara ya pamoja.

Kama Tanzania imekuwa ikibaki nyuma, Uganda imekuwa ikichangamkia sana wazo la kuwa na shirikisho, pamoja na mambo mengine, kwa kuwa Rais Yoweri Museveni ana ndoto ya muda mrefu ya kuustafu akiwa rais wa kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki.

Hata Paul Kagame, Rais wa Rwanda, anaelezwa kwamba anafurahia wazo la kuwa na EAC. Ushirikiano wake wa hivi majuzi na Jamhuri ya Kongo (DRC) unalenga kukuza biashara baina ya nchi hizo kwa kutumia soko kubwa la Afrika Mashariki. Anataka kuwa anasafirisha bidhaa za Kongo, zilizoongezewa thamani Rwanda kupita katika mianya ndani ya EAC.

Na Kongo haina tatizo na maono hayo ya Kagame. China ambayo ndiye mwekezaji mkubwa katika DRC inataka mbao, chuma na madini mengine yasafirishwe kupitia bandari za Afrika Mashariki.

Kwa sababu hiyo, na sababu nyingine, Kenya, kwa upande wake inataka kujenga bandari mpya ya kina kirefu karibu na kisiwa cha Lamu, karibu na mpaka wa Somalia. Kwa ajili hiyo baadhi ya maofisa wa Kenya wanasema mikoko na mazalia ya samaki jirani na mahali itakapojengwa bandari hiyo si masuala ya kuzuia kujengwa kwake.

Wanasema bandari hiyo, kiwanda cha kusafisha mafuta na mji mpya vitawekwa mahali ambako havitavuruga urithi na biashara ya utalii ya Lamu. Matarajio ya baadaye ni kuwa na barabara na reli kwenda Mogadishu, Addis Ababa na Kigali bomba la mafuta likileta mafuta ya Uganda na Sudan Kusini.

Fedha za uwekezaji zitakuja kutoka Kuwait na matajiri wengine kutoka katika nchi za Ghuba, kwa njia hii Afrika Mashariki itaunganishwa kuliko ilivyopata kuwa na soko la pamoja litakuwa na maana zaidi.

Na hakika kwa nini shirikisho la Afrika Mashariki lisipanuke nje ya nchi wanachama wa sasa? Likitazamwa kwa maana ya lugha ya maeneo haya, yaani Kiswahili, malori ya bidhaa yatayokuwa yakitoka katika bandari ya Mombasa na mvutano wa kisumaku unaoufanya mji mkuu Nairobi kuwa kitovu cha shughuli nyingi, Afrika Mashariki inasambaa hadi Ethiopia, inahusisha sehemu za Somalia, sehemu ya mashariki mwa DRC na ukanda kaskazini mwa Msumbiji na na eneo lote la kusini mwa Sudan ambayo inatarajiwa kuwa huru ifikapo mwaka 2011 kama kura za maoni za raia wa eneo hilo zitaamua hivyo.

Kuna watu wapatao milioni 126 katika EAC. Likipanuka watu zaidi ya milioni 120 wataongezeka hiyo ikifanya idadi ya watu zaidi ya mara mbili ya nchi kadhaa ndogondogo katika maeneo mengine ya Afrika, idadi inayotosha kulifanya eneo hilo kuvutia zaidi kwa wawekezaji wa nje na kulifanya kuwa na nguvu zaidi katika majadiliano na dunia nyingine.

Lakini wafanyabiashara wakazi bado wana wasiwasi. Kwao shirikisho linaweza kukwazwa na mgogoro wa kibiashara, mapigano ya kikabila au likabanwa tangu mwanzo na wanasiasa wafanyabiashara wenye uchu na urasimu wa watendaji. Hakika kuna maoni m changanyiko.

Nalo gazeti la The Guardian na The Obsever yote ya Uingereza, yalieleza kuhusu uwekezaji katika mbuga ya Loliondo, kaskazini mwa Tanzania kuwa ni kati ya mifano ya Serikali ya Tanzania kutokana na kuwa na njaa ya “dola za Marekani” inakumbatia zaidi wawekezaji kuliko wananchi wake, na inathamini wanyama wanaovutia watalii wengi kuliko kuthamini wananchi.

Katika machapisho hayo yaliyoandikwa na waandishi waliofika eneo la Loliondo, imewekwa bayana kuwa licha ya malengo ya serikali kujiongezea mapato kutokana na sekta ya utalii, lakini maisha ya wenyeji katika maeneo ya uwekezaji ni duni, na hakuna uhusiano mzuri kati ya wawekezaji na wenyeji.

Kwa mujibu wa habari hizo, wamasai ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiendeleza utamaduni wao wa ufugaji kwenye ardhi yao, kwa vizazi na vizazi, sasa wanatakiwa kuhama maeneo hayo ili kuwapisha wawekezaji mamilionea, kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kitalii.

“Nikiwa katika eneo la umasaini, simu yangu inasoma ujumbe unaonikaribisha katika Jamhuri ya Kiarabu (United Arab Emirates).

“Ni ujumbe unaosema furahia mtandao bora zaidi wa simu na huduma nyingine wa Etisalat," "Furahia uwapo wako hapa Jamhuri ya Uarabuni!"

Ni eneo ambalo wenyeji wamelipachika jina la Uarabuni. Ni eneo yalipo makao makuu ya Shirika la Biashara la Ortelo (OBC), kampuni inayohusika na masuala ya utalii ambayo haijawekwa katika matangazo ya tovuti.

Ilianzishwa mwaka 1993 na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Uarabuni (UAE) yenye uhusiano wa karibu na familia ya kifalme, Dubai.

Ni kampuni ambayo pamoja na mambo mengine ni mahsusi kwa ajili ya kuwapokea masheikh na mamilionea wa kiarabu ambao hufika Kaskazini mwa Tanzania kupumzika, eneo la Loliondo.

Katika habari iliyoandikwa na gazeti la The Obsever la Uingereza, Loliondo inaelezwa kama eneo la kuvutia ambalo “kutokana na njaa ya dola (fedha) kwa serikali ya Tanzania limetolewa kwa wawekezaji wa kigeni.

“Mkakati wa maendeleo wa Tanzania unaeleza kuwa ni lazima idadi ya watalii wanaotembelea nchi hiyo ifikie watalii milioni moja mwaka 2010.

“Ni dhahiri kuwa maofisa wa serikali wanafanya chochote ili kuhakikisha malengo hayo yanatimia. Takriban robo ya eneo la nchi limetengwa kwa ajili ya kile kinachoitwa hifadhi.

Maili chake kutoka kilima kilichopewa jina la “Uarabuni” kuna shughuli nyingine za kijasiriamali zinazoendelea zikihusisha wajasiriamali wa kiarabu.

Kuna eneo la hekari 12,000 lililotengwa kwa ajili ya hoteli na kupiga kambi kwa watalii. Eneo hilo limetolewa kwa mwekezaji ambaye shughuli zake zinaunganishwa kwa jina la kikampuni la Thomson Family Adventures.

Utoaji wa maeneo hayo umekuwa ukilalamikiwa na wenyeji ambao ni wamasai wakidai hawana maeneo ya kulisha na kunywesha mifugo yao.

Lakini mwekezaji huyo amekuwa akikanusha madai ya wenyeji hao akisema; "Wamekuwa wakipewa huduma ya maji ya visima wakati wa kiangazi.” Imeripotiwa kuwa kwa miaka miwili sasa, kumekuwapo na mashambulizi hata ya kutumia risasi kati ya walinzi wa mwekezaji huyo na polisi dhidi ya wenyeji.

Liz McKee, ambaye ni Meneja Mkuu wa shughuli za mwekezaji huyo amenukuliwa akimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa mradi unaokusudiwa kuanzishwa utahifadhi ardhi na wanyama.

Haamini kwamba ni busara kuwaacha wafugaji kuendelea na mfumo wao mkongwe wa maisha uliodumu kwa karne kadhaa.

Hakuna ardhi ya kutosha, sidhani kama wamasai wataendelea na maisha haya ya kufuga kwa kuhama hadi mwisho wa dunia.” Anasema mwanamama huyo mwenye asili ya Uingereza.

McKee ni mtu ambaye aheshimu kwa asilimia 100 utamaduni wa kimasadi na hasa unaohusu tabia dhidi ya wanawake ikiwamo ya kuoa watoto wadogo hata wenye umri wa miaka 12.

Ni wazi kuwa sasa utamaduni imara wa wamasai unaanza kunyongwa kisayansi. Serikali ya Tanzania imekuwa karibu zaidi na wawekezaji wa kitalii, huku wamasai wakilalamika kuhamishwa kwa nguvu kwenye makazi yao ya asili.

Taarifa hizi zinanukuu matamko ya wanaharakati nchini kwamba kati ya miezi ya Julai na Agosti, mamia ya wamasai walichomewa nyumba zao za polisi ikiwa ni majibu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa baadhi ya wamasai kuingiza mifugo yao eneo la mwekezaji wa kiarabu.

"Wamasai wanaonekana kuwa wanahitaji katika kupigwa picha na watalii, kubeba mabegi ya watalii, au hata kuwalinda," anasema Moringe ole Parkipuny, ambaye ni mzee wa kimasai aliyewahi kuwa mbunge na kuongeza kuwa; "Siku hizi wanyama wanakuwa na thamani zaidi kuliko watu."

Hapa, wamasai wanatakiwa kuhama kwa amri ya serikali ili kupisha nyati 25 ambao ni kivutio kwa mamia ya watalii ndani ya mbuga ya Ngorongoro.

Ololosokwan ni mkazi wa umasaini ambaye alituhadithia kuhusu uvumi kuwa Sheikh kutoka Dubai atawasili hivi karibuni katika Shirika la Ortelo.

Kumekuwapo na maelezo kutoka kwa wenyeji kuwa kila wanapokuja wageni maarufu kutoka Uarabuni hutandikiwa zulia jekundu. Mwandishi aliyekuwapo huko alitaka kujua kama anaweza kupiga picha na alipowaeleza nia yake hiyo, alijibiwa; "Watu hukamatwa wanapokaribia eneo hilo.”

Inaelezwa kuwa kampuni ya OBC imepewa leseni ya kuua simba watano kwa msimu. Lakini swali linakuja nani anayehakikisha idadi hiyo? Anahoji mkazi mmoja wa kijiji jirani na Jamhuri ya Kiarabu, Loliondo.

Waandishi wa habari na watu kutoka Mashirika yasiyo ya Serikali (NGOs) wamekuwa wakipigwa marufuku kufika eneo hilo na hata wenyeji wamekuwa wakionywa na polisi kuwa hata kuzungumzia kwa ubaya kuhusu OBC kutawatia kwenye matatizo.

Mfugaji mmoja wa kimasai alieleza kuwa amekwishawahi kuona mtego wa kutega chui wakiwa hai, ikielezwa kuwa wamepewa kibali hicho na serikali.

Inadaiwa kuwa msimu uliopita wa kiangazi, kijana wa kimasai mwenye umri wa miaka 29 alikufa kutokana na ajali, lakini ilidaiwa kuwa kijana huyo alipigwa risasi na baadaye kugongwa kwa gari ili kuzima joto la vurugu ambalo lingeweza kuibuka kutoka kwa wenyeji.

Hata hivyo, kampuni ya OBC imekuwa ikitoa misaada ikiwamo ya mahindi ili kukabili tatizo la njaa lililokuwa likiwakabili wenyeji. Inaelezwa pia kwamba kampuni iliwahi kutoa shilingi milioni 25 lakini baadhi ya wanavijiji walikataa fedha hizo.

"Hatukushirikishwa wakati waarabu wanapewa maeneo haya," anasema Kirando ole Lukeine, mmoja wa wazee wa kimila na kuongeza kuwa; "Kwa hiyo, kijiji chetu hakitaji msaada wowote kutoka kwao.”

Mzee mwingine wa kimasai anasema; “Tunaeleza ni lazima tuitii serikali lakini hizi ni mbinu tu za kutaka kuchukua sehemu nyingine ya ardhi yetu."

Kumekuwapo na madai kuwa maofisa wa serikali wakiwamo baadhi wanaoshughulikia masuala haya wamekuwa na ukwasi wa kupindukia. Takwimu za rushwa zinaonyesha kuwa Tanzania ambayo mwaka 2008 ilikuwa nchi ya 102 kati ya 180 zilizokithiri kwa rushwa, iliambulia dola za Marekani milioni 9.3 mwaka 2002, kutokana na masuala ya uwindaji kwa leseni.

Hata hivyo, taarifa za waandishi wa kigeni zinaeleza kuwa licha ya mapato hayo hali ya umasikini miongoni mwa wenyeji ni duni.

Mchakato wa kuhamisha wafugaji una historia ndefu nchini Tanzania, ikiwa ni mpango ulioanza mwaka 1959, wakati huo mpango huo ukiendeshwa na serikali ya kikoloni kutoka Uingereza.

Baada ya uhuru, mwaka 1961 hifadhi nyingi za taifa zilianzishwa, uanzishwaji ulioambatana na kuhamisha wenyeji kwenye maeneo husika.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya wananchi ni masikini wa kutupwa, na asilimia 15 ya watoto wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa na umri chini ya miaka mitano.

Hata hivyo, licha ya takwimu hizo mbaya inaelezwa kuwa idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka na hivyo kuongeza mapato ya serikali.

Liz McKee, amekuwa akielezea matarajio yake kama mwekezaji kuwa wenyeji watapata ajira kutokana na kuanza shughuli kwa kampuni anayosimamia, ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwakani.

McKee ndiye aliyemwalika mwandishi wa jarida la The Observer kutembelea kampuni yake na kumhoji meneja mwenyeji, Daniel Yamat.

Hata hivyo, kutokana na maelezo hayo ya kupatiwa ajira, mwandishi kabla ya kufuatilia mwaliko huo alitaka kujua maoni ya mwenyeji, Lesingo Ole Nanyoi, kama yuko tayari kupewa ajira, naye alimjibu; hapa, hilo haliwezekani.

Lesingo ambaye ni baba wa watoto wanne akiwa na wake wawili, wakati mwingine amekuwa akilazimika kuuza ng’ombe wake ili kupata fedha za kuendesha familia yake ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za matibabu.

Source:wwww.raiamwema.co.tz

Thursday, September 10, 2009

Wanawake jamii ya kimasai wasema "Loliondo hatuami ng’o''

Wanawake wakaazi wa wa eneo la Loliondo linalokabiliwa na mgogoro wa ardhi na mwekezaji wa kampuni ya kiwindaji (OBC) wamesisitiza kuwa katu hawataama katika maeneo yao hata kwa mtutu wa bunduki.

Akiongea na waandishi wa habari, kiongozi wa wanawake hao Bi Juliana Tipa alisema kuwa wapotayari kupambana na kikwazo chochote lakini suala la kuhama katu hawaafikiani nalo.

Aliongeza kuwa Tanzania ni nchi huru na wao ni wananchi ambao wanastahili kupewa haki zao ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi na uhuru wa kufanya maamuzi.
Aidha kina mama hao walieleza matatizo wanayokumbana nayo katika maisha yao ya kila siku kuwa ni pamoja na kuishi maisha ya dhiki ambayo yametokana na vitisho na kuchomewa nyumba zao.

Vilevile wamebaibainisha kuwa watoto wao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na wazazi wao kuhamahama na kuokosekana kwa amani katika eneo lao.

Wednesday, September 9, 2009

WANAWAKE wa Kimasai wanaoishi katika wilaya ya Ngorongoro eneo la Loliondo wametoa tamko rasmi la kuiomba Serikali iwaangalie

WANAWAKE wa Kimasai wanaoishi katika wilaya ya Ngorongoro eneo la Loliondo wametoa tamko rasmi la kuiomba Serikali iwape misaada ya dharura ya chakula, mahema na maji pamoja na kupewa maeneo ya kulisha mifugo yao kutokana na opoeresheni kuwahamisha.

Kiongozi wa wanawake hao aliyesoma Tamko hilo Pirias Maingo aliwaambia wanaoshiriki tamasha la 9 la Jinsia Dar es Salaam, lililoandaliwa na Mtandao wa mashirika wateteza wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia (FemAct) Pirias Maingo alisema jana kuwa wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu tangu waanze kuhamishwa kwa nguvu katika eneo hilo.
Pirias alisema wanasikitishwa kwa serikali kutowaonyesha maeneo ya kuishi baada yakuchomewa nyumba zao kupisha shughuli za uwindaji. Alifafanua kuwa wamelazimika kuhamia maeneo ambayo yana ukame , hayana maji hata malisho kwa ajili ya mifugo yao.

Tamko hilo lilitolewa baada ya Mwanamke wa Kimasai Kooya Oletiman, kuzungumza kimasai na kutafsiriwa na Paulina oletipap kuwa wanawake na watoto ndiyo wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na majukumu waliyonayo ya kutunza familia ambapo tangu oparesheni ya kuwahamisha ilipoanza wamekuwa wakihama hama na kukosa mahali pa kujisitiri.
Wanawake hao wapatao 978 kutoka katika vijiji vya Arash,Maaloni, Ololosokwan, Olipiri, Soitsambu, Olorien Piyaya na Malambo wamesema kuwa wametaka pia kampuni ya uwindaji ya OBC iondolewa ktika eneo hili badala yake ardhi ya vijiji ihakikishiwe usalama wake kwa mujibu wa sheria.


Tamasha la Jinsia 2009 linaendelea leo kwa mada mbalimbali ambazo msisitizo wake mkubwa ni rasilimali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni




KIKWETE KUONGEA NA WANANCHI LAIVU LEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, leo, Jumatano, Septemba 9, 2009, atazungumza moja kwa moja na wananchi kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na vyombo vingine vya utangazaji nchini kuanzia saa mbili na nusu usiku.
Mbali na TBC, televisheni nyingine za ITV, TVZ, Mlimani TV, Tumaini TV na Channel Ten zinatarajia kuonyesha mazungumzo hayo.

Rais atatumia aina mpya ya kuwasiliana na wananchi kwa kusikiliza hoja zao, kwa kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao na kupata maoni juu ya mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, Serikali yetu na maendeleo yetu.

Aidha, Rais atasikiliza matarajio ya wananchi katika jitihada zao za kuboresha maisha yao kwa kujiletea maendeleo.

Mazungumzo hayo yatakayochukua muda wa dakika 90 kuanzia saa mbili unusu usiku (saa 2:30 usiku) hadi saa nne kamili usiku.


Aidha mazungumzo hayo yatatangazwa kwenye redio za TBC-Taifa, Sauti ya Tanzania, Zanzibar, Radio Mlimani, Radio Clouds, Radio Tumaini, na Radio Uhuru.

Maswali, maoni, hoja, ushauri utapokelewa moja kwa moja na TBC kupitia simu nambari
+255-22-2772448,
+255-22-2772452
na
+255-22-2772454.

Aidha, maswali, maoni, hoja ama ushauri unaweza kutumwa moja kwa moja TBC kupitia ujumbe mfupi wa SMS kwenye nambari
0788-500019,
0714-591589
na
0764-807683
ama kupitia kwenye barua pepe
swalikwarais@yahoo.com
kuanzia leo.

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inawashauri wananchi kutumia kikamilifu nafasi hiyo ya kuwasiliana moja kwa moja na Rais wao.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

08 Septemba, 2009

Friday, September 4, 2009

Tamasha la ukombozi wa Wanawake kimpinduzi kuzinduliwa wiki ijayo

Kwa mara nyingine Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) & FemAct wanayo furaha kukukaribisha kwenye Tamasha la Jinsia la mwaka
2009 litalojumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali litakalofanyika wiki ijayo tarehe 8/9/2009 mpaka tarehe 11/9/2009 katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania.

Madhumuni ya matamasha ya jinsia ni kuwapa nafasi
wanamtandao na washirika wao kupeana moyo,
kutafakari, kuitathimini hali ya jinsia, kushirikishana
hatua za maendeleo na kupeana mikakati ya utekelezaji.

Unaalikwa na unakaribishwa kushiriki kwa matarajio
utakuwa kiungo muhimu katika kujenga vuvugu la nguvu
za pamoja za kuleta maisha bora kwa wanawake na
wanaume walioko pembezoni.

Kuwepo kwenye tamasha, kushiriki majadiliano,
kuhudhuria vipindi vyote bila kuchomoka chomoka ni
jambo linalotegemewa.

Wote mnakaribishwa!!

Wabunge kutetea msimamo Kamati ya Mzee Mwinyi

-Wakataa viapo vyao kugeuzwa kiini macho
-Wasema wananchi ni makini kuliko vigogo

BAADHI ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameanza kujipanga kutetea msimamo wao wa kutaka mijadala ya ufisadi iendelezwe wazi wazi, na wahusika wachukuliwe hatua badala ya kuwalinda, pindi watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Wabunge hao wameahidi kuwa na msimamo unaowiana na matakwa ya Katiba ya Tanzania, waliyoapa kuilinda na kuitetea. Wamebainisha kuwa, itakuwa fursa nzuri kwao kutetea Katiba kwa mujibu wa viapo vyao, mbele ya kamati hiyo iliyoundwa kwa matakwa ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, ikiwashirikisha Spika wa zamani, Pius Msekwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdurahman Kinana.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kuwa kiu ya wabunge hao kukutana na kamati hiyo imekuwa kubwa na hasa kwa upande wa wabunge wasiopendezwa na juhudi za kutaka kufunika mijadala ya ufisadi badala ya kuwachukulia hatua wahusika.

Wabunge waliozungumza na Raia Mwema bila kutaka kutajwa majina yao kwa madai kuwa wakati wa kuwasilisha hoja hizo bado, wameeleza kuwa tayari kuchambua kwa kina namna ambavyo chama na serikali yao inavyojitenga na wananchi kutokana na kuwapo kwa juhudi za kulinda watuhumiwa wa ufisadi, na kuzima mijadala ya namna hiyo.

Kwa mujibu wa wabunge hao, tayari matokeo ya hali hiyo ya kuzuia mijadala ya wazi ya ufisadi yamekwishajitokeza katika kampeni za chaguzi ndogo Tarime, Mbeya Vijijini, Busanda na Biharamulo, ambako vyama vya upinzani vimekuwa vikiinadi CCM kuwa ni chama chenye ubia na watuhumiwa wa ufisadi.

“Kwa kadiri unavyozuia wabunge wa CCM kuzungumzia ufisadi kwa kuulani au kutaka wahusika wachukuliwe hatua, ni wazi unapeleka ujumbe kwa umma kuwa chama kama taasisi kinakubaliana na matendo ya watu hao. Hatua hii ni kunufaisha vyama vya upinzani. Ndani ya vyama vya upinzani hakuna kuzuiana kupinga ufisadi.

“Ndiyo inaeleweka kwamba unapozungumzia ufisadi maana yake unagusa watendaji wa chama na serikali ya CCM. Wanachoshindwa kuelewa hapa ni kuwa wanaoguswa ni hao watendaji na si serikali au chama kama taasisi. Kwa hiyo hukibomoi chama au serikali bali unabomoa wanaonufaika na ufisadi na kukiacha chama au serikali salama. Binafsi, napenda ieleweke kuwaandamana watuhumiwa wa ufisadi ili waache si kukiandamana chama, ni kukiimarisha chama,” alisema mbunge mmoja kutoka Tanga.

“Kuna viongozi wetu katika CCM bado wanaamini wananchi ni mbumbumbu, hawawezi kuelewa uchafu wa kifisadi wanaofanya eti wakitaka sote katika CCM tuwalinde, hili haliwezekani. Kutopinga ufisadi hadharani maana yake ni kuimarisha vyama vya upinzani majukwaani,” alisema mbunge mwingine kutoka mkoani Iringa.

Mbunge mwingine kutoka Ruvuma ameiambia Raia Mwema kuwa; “Sitegemei kuona wabunge wenzangu wakikubali kuruhusu viapo walivyokula kuilinda na kuitetea Katiba inayolinda maslahi ya wananchi wote, vikigeuzwa kuwa ni viapo kiini macho. Kama watafanya hivyo Mungu na Watanzania hawatawasamehe.”

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadhi ya wabunge wamedhamiria kuweka bayana vielelezo kadhaa vinavyothibitisha kulinda ufisadi si malengo ya CCM, na hujuma za kuhakikisha mijadala ya ufisadi inafungwa pia ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Tanzania, waliyoapa kuilinda.

Lakini wakati wabunge hao wakijipanga kwa staili hiyo, Raia Mwema imebaini kuwa ingawa wiki tatu zimepita tangu kuundwa kwa kamati hiyo itakayochunguza kile kilichoitwa “uhusiano mbovu” miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawaziri, msingi wake ukitajwa kuwa ni Spika Samuel Sitta kutoa uhuru mkubwa kwa mijadala ya ufisadi bungeni na hivyo kukidhoofisha chama hicho na serikali yake, hakuna taarifa zozote rasmi zilizowasilishwa ofisi ya Bunge kama mdau mkuu, na hasa kuhusu ratiba ya kukutana na wabunge.

Kamati hiyo ambayo inatarajiwa kukutana na wabunge wa CCM pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kusikiliza maoni yao na hata kubaini chanzo cha mpasuko kati yao na serikali, bado haijaweka bayana utaratibu wake wa namna ya kukutana na wawakilishi hao wa wananchi, ingawa taarifa zinaeleza kuwa huenda wakakutana na wabunge katika mkutano ujao wa Bunge, mjini Dodoma.

Mkutano ujao wa Bunge unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Oktoba na kuendelea hadi katikati ya Novemba, mwaka huu. Ni katika mkutano huo ambapo serikali italazimika kuwasilisha taarifa yake kuhusu hatua ilizochukua dhidi ya watendaji wa serikali waliobainishwa na Kamati Teule ya Bunge kuwa wawajibishwe.

Serikali itawasilisha taarifa hiyo kutokana na taarifa yake ya awali kukataliwa na Bunge ikiwekwa bayana kuwa, kilichofanyika katika taarifa hiyo si utekelezaji bali uchunguzi uliolenga kuwasafisha wahusika na si kuzingatia hali halisi inayotawaliwa na matakwa ya sheria.

Katika kikao cha NEC wiki tatu zilizopita, iliripotiwa kuwapo kwa mjadala mkali kuhusu uendeshaji wa Bunge, huku wajumbe wengi wakionekana kuchoshwa na utendaji kazi wa Spika, na hasa uamuzi wake wa kuachia uhuru mpana zaidi wa mijadala ya ufisadi bungeni.

Wajumbe wengi waliochangia katika mkutano huo walimwelezea Spika kama mtu anayestahili kuvuliwa uanachama kwa kuwa utendaji kazi wake unakidhoofisha chama na serikali yake.

Imeripotiwa kuwa kati ya wajumbe hao ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Kingunge Ngombale-Mwiru pamoja na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

Hata hivyo, hoja za wajumbe hao na wengine ambao majina yao hayajaorodheshwa hadharani zilipingwa vikali na wanachama wengine wa CCM nje ya mkutano huo na hata wanataaluma wengine wasio wanachama wa chama hicho.

Wengi waliopinga vitisho vya kumnyang’anya kadi ya CCM Spika Sitta walidai kuwa hatua hiyo ni kuvunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 100, inatamka kuwa masuala ya Bunge hayapaswi kuhojiwa nje ya chombo hicho.

Hata hivyo, licha ya upinzani huo, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati kwa nyakati tofauti walijitokeza hadharani ili kutetea uamuzi huo, na kusisitiza kuwa “wanajeuri ya kumwita na kumhoji Spika.”

Wakati Makamba akitamka kuwa wanajeuri ya kumwita na kumhoji Spika, Chiligati alifafanisha uendeshaji wa midajala bungeni kuwa wakati mwingine ni sawa na kundi la wasanii wachekeshaji.

Kauli hizo za Makamba, Chiligati na hata ile ya Mkuu wa Idara ya Propaganda ya CCM, Hiza Tambwe zilimfanya Spika, Samuel Sitta, akiwa jimboni kwake Urambo Mashariki kulalamika kuwa viongozi hao wamekuwa wakiingilia majukumu ya Kamati ya Mzee Mwinyi.

Kwa mujibu wa Spika, kauli hizo zilikuwa zikiingilia utendaji wa kamati hiyo kwa kuwa tayari zilikuwa zikiegemea zaidi upande mmoja kati ya makundi yanayopaswa kusikilizwa malalamiko yao na kamati Mwinyi.

Uamuzi wa kikao hicho cha NEC uliambatana na matukio mbalimbali ya kisiasa, ikiwamo madai ya Spika kuwa mapokezi yake mkoani Tabora yalihujuiwa na baadhi ya viongozi CCM makao makuu.

Pia baada ya kikao hicho kuliibuka madai mazito ya wajumbe wengi wa NEC kuhongwa fedha na kundi la mafisadi ili kuhakikisha Spika anavuliwa uanachama na pale mkakati huo ulipokwama, taarifa zilieleza kuwa kundi hilo lililotoa fedha limechukizwa na mpango huo kufeli.

Madai ya Spika kuandamwa yalianzia katika mkutano uliopita wa Bunge, ambako alifikia hatua ya kuomba ulinzi serikalini na kuweka bayana kuwa maadui zake kisiasa wamekuwa wakimwandama hadi jimboni kwake ambako fedha nyingi zimemwaga na akiwahimiza wananchi kutumia bila kusita fedha hizo.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba mnipe ulinzi zaidi, hii vita ni ngumu na kubwa sasa. Ulinzi mnaonipa ni dhahiri kuwa hautoshi,” alilalamika Spika Sitta, katika moja ya vikao vya mkutano uliopita wa Bunge.

Kumekuwapo na hali ya kutoridhishwa na mwenendo wa vikao vya NEC, hali ambayo ilianza kujitokeza tangu kikao cha Juni, mwaka jana, mjini Dodoma.

Source:www.raiamwema.co.tz

Thursday, September 3, 2009

Kikwete awapa mafisadi ahueni

-Asaini marekebisho yaliyopitishwa na Bunge kimya kimya
-Ufisadi sasa si uhujumu uchumi
-Kesi za ufisadi kuwa kiini macho?

RAIS Jakaya Kikwete amesaini kuridhia mabadiliko ya sheria zinazohusu rushwa na uhujumu uchumi, hatua ambayo wanaharakati wa vita dhidi ya ufisadi nchini wanaitafsiri kwamba ina lengo la kupunguza makali kesi za uhujumu uchumi na rushwa zinazowakabili baadhi ya vigogo nchini, RAIA MWEMA limeambiwa.

Katika hatua hiyo, inayoashiria kupunguza makali ya sheria zinazotumika kuendesha kesi za uhujumu uchumi na rushwa nchini, kesi ambazo baadhi zinaendelea kusikilizwa mahakamani zikiwahusisha waliowahi kuwa viongozi wa kitaifa, Rais Kikwete, Machi, mwaka huu, alisaini marekebisho hayo ya sheria yaliyopitishwa na Bunge katika kikao chake cha Januari mwaka huu.

Hatua hiyo inatokana na kuwasilishwa bungeni kwa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, ndani yake kikiwamo kipengele kinachoingiza makosa ya rushwa katika Sheria namba 200 ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002 (Economic and Organized Crime Act Cap 200 R.E. 2002).

Kwa kutia saini kwa Rais Kikwete kuridhia marekebisho hayo, rushwa sasa si kosa la kuhujumu uchumi.

Raia Mwema imefahamishwa kwamba mabadiliko hayo ya sheria yaliyopitishwa na Bunge Januari, yalisainiwa na Rais Jakaya Kikwete, Machi 12, mwaka huu na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Machi 20, 2009. Habari kwamba Rais ameridhia marekebisho hayo kwa kutia saini zilifahamika hivi karibuni tu kwa wanaharakati wa vita dhidi ya ufisadi nchini.

Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini kwamba Mabadiliko hayo ya Sheria hiyo yamewashitua wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambao wanasema wakati sheria hiyo inapitishwa walipata nafasi ya kuchangia maoni, hali ambayo haikujirudia wakati wa kuifanyia mabadiliko.

“Tulikuwa tunafikiria Serikali iongeze makali katika sheria ili tuweze kuwadhibiti zaidi mafisadi na wahujumu uchumi, badala yake sasa tunalegeza sheria ili kuwasaidia, ” alihoji mdau wa mapambano dhidi ya ufisadi aliyeko serikalini ambaye anasema ameshitushwa na mabadiliko ya sheria hiyo.

Mabadiliko hayo yamo katika kifungu cha 38 na 39 cha Sheria namba 3 ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2009, kifungu kinachofuta kifungu cha kwanza na cha pili katika jedwali la kwanza la makosa ya uhujumu uchumi kinachoingiza makosa ya rushwa na ufisadi.

Vifungu vilivyofutwa vilikuwa vinasomeka hivi:“Mtu yeyote atakuwa ametenda kosa (la uhujumu uchumi) ikiwa atakuwa ametenda kosa chini ya Sheria ya Kuzuia Rushwa” na “atakuwa ametenda kosa (la uhujumu uchumi) ikiwa atakuwa ametenda kosa la rushwa zaidi ya makosa yanayotajwa katika kifungu cha nne cha Sheria ya Kuzuia Rushwa.”

Kuondolewa kwa vifungu hivyo kunatoa nafuu kubwa kwa watu ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya ufisadi, lakini pia mabadiliko hayo yanawavunja nguvu wapambanaji wa ufisadi ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola vikiongozwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Habari za ndani ya Serikali zinaeleza kwamba hakuna uhakika wa moja kwa moja kwamba TAKUKURU ilishirikishwa katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko sheria hiyo ambayo ndiyo imekuwa kwa muda mrefu msingi wa mashauri mengi inayopeleka mahakamani na kwa ajili hiyo marekebisho hayo yanagusa moja kwa moja utendaji kazi wa kila siku wa taasisi hiyo inayopigana dhidi ya rushwa nchini.

“Kama TAKUKURU wameshirikishwa basi itakuwa ni juu juu sana, lakini ninavyofahamu ni kwamba hawajashirikishwa katika hili bali Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliandaa muswada na kuupeleka bungeni kimya na wabunge wetu bahati mbaya sana hawakugundua hilo,” ameeleza mdau mmoja muhimu wa mapambano dhidi ya rushwa.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Dk. Edward Hosea, hakuweza kupatikana kuzungumzia Mabadiliko hayo ya Sheria yanayoipunguzia ofisi yake ‘makali’ kutokana na kile Raia Mwema ilichoambiwa ya kuwa amekuwa na vikao na kufanya kazi za nje ya ofisi.

Mabadiliko hayo ya Sheria ndogo ndogo yaliwasilishwa bungeni yakiwa na marekebisho katika sheria mbalimbali 11 ikiwamo hiyo ya uhujumu uchumi na inawezekana kwamba wabunge wengi walikosa nafasi ya kupitia sheria zote zilizoguswa na mabadiliko hayo.

Sheria nyingine zilizounganishwa katika muswada huo ambao tayari umekuwa sheria ni pamoja na ya Administrator-General (Powers and Function) Act, ya Usajili wa Vizazi na Vifo, ya Chuo cha Sheria (Law School of Tanzania), Utumishi wa Umma, Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Afya, National Prosecution Service Act, Sheria ya Uchawi, Penal Code, Sheria ya Leseni za Usafirishaji na Sheria ya Ardhi.

Madhumuni ya awali ya kutungwa kwa sheria ya rushwa yalikuwa ni pamoja na kukuza na kuchochea utawala bora na kutokomeza rushwa na ufisadi kwa kutoa msingi wa kitaasisi na kisheria ambao ni muhimu katika mapambano hayo.

Mabadiliko haya yamekuja baada ya hatua kadhaa za Serikali ya Awamu ya Nne iliyofungua, baada ya muda mrefu, kesi kadhaa, zikiwagusa vigogo mbalimbali, karibu zote zikitumia kipengele cha makosa ya uhujumu uchumi ambacho kilisababisha wengi wao kukwama kupata dhamana.

Miongoni mwa walioshitakiwa kwa makosa hayo ni pamoja na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, mawaziri wa zamani, Daniel Yona na Basil Mramba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha kwa muda mrefu, Gray Mgonja.

Mbali ya viongozi hao waandamizi, kuna mlolongo wa watuhumiwa wengine wa ufisadi ambao TAKUKURU imewashitaki kwa kutumia Sheria ya Uhujumu Uchumi, wakiwamo watuhumiwa wa EPA na ujenzi wa majengo pacha ya BoT, wote wakibanwa na sheria hiyo katika kupatiwa dhamana.

Wakati kesi hizo zikifunguliwa hasa baada ya vigogo kuanza kupandishwa kizimbani, baadhi ya watu walisema kwamba kesi hizo zimefikishwa mahakamani kama njia ya kufunika baadhi ya mambo ya ndani ya serikali.

Soma zaidi

Wednesday, September 2, 2009

Watoto wafungwa jela ili kumfurahisha mwekezaji

MWANAFUNZI wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mariwanda B, Juma Sylvester (16), alipaswa kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana. Badala yake, yeye na wenzake wawili Hurushi Wambu (16) na Ndamo Wambu (16) wakafunga mwaka 2008 wakiwa jela.

Watoto hao ambao wana umri chini ya miaka 18, wako jela ya watu wazima wakitumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kuingiza mifugo katika eneo la mwekezaji kampuni ya Grumet wilayani Bunda mkoani Mara.

Vijana hao walitiwa hatiani Agosti 4 mwaka jana, katika mahakama ya wilaya ya Bunda na hakimu wa wilaya hiyo, Richard Maganga baada ya kukiri kosa la kulisha ng’ombe katika eneo hilo lililokodishwa kwa shughuli za uwindaji na uhifadhi kwa kampuni ya Grumet.

Sylvester au Gujoru Girabi, Wambu na Wambu wanatimiza mwaka mmoja gerezani huku mwenzao mmoja Juma Nyakire (15) akipumua baaada ya Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kumfutia kesi iliyokuwa inamkabili kama hiyo, Agosti 5 mwaka huu.

Nyakire mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kunzugu wilayani Bunda mkoani Mara pia alifungwa miaka mitatu Januari 2 mwaka huu, katika kesi namba 381/2008 kwa kuingiza mifugo eneo la hifadhi huku watoto wenzake wenye kesi namba 212/2008 na 282/2008 wakiendelea kusota jela.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mariwanda B, David Barijera anasema kufungwa kwa mwanafunzi wake, Juma Silivesta kumemfanya ashindwe kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka jana.

"Kijana huyu alikuwa tayari kapewa namba ya mtihani ambayo ni PS/090/137/013 lakini hakufanya na alikuwa kati ya wanafunzi bora, lakini hiki kitendo cha kufungwa mwanafunzi wetu kimetusikitisha sana," anasema Barijera.

Unaweza usiamini unaposoma taarifa hii lakini hii ni hali halisi ambayo serikali ya awamu ya nne imelifikisha taifa hili. Sasa wawekezaji, kama alivyosema Mbunge ya Jimbo la Kyela Dk. Harrison Mwakyembe wanaonewa aibu na Serikali kama wakwe hata pale inapodhihirika wazi wamekosea .

Wakati taarifa ya matukio haya ikitolewa kwa wanasheria wa kituo cha haki na binaadamu (LHRC) mkoani Arusha , wakili wa shirika la kutetea wafugaji Pingos Forum na waandishi wa habari ilikuwa vigumu kuamini lakini baadaye yote yaliyoelezwa yalithibitika kuwa ni ukweli.

Watoto wadogo watatu, ambao walipaswa kulindwa na sheria zilizopo, wanatumikia kifungo huku kampuni ya Grumet ikiendelea na shughuli zake za kuvuna wanyama pori katika pori hilo la akiba ya Grumet.

Baada ya kuvuna wanyama pori, mwekezaji huvilipa vijiji saba vya wilayani Bunda jumla ya Sh 1.8milioni kila mwaka. Vijiji hivyo ni vile vinavyopakana na pori la akiba la Grumet.Mwenyekiti wa kijiji cha Mariwanda, Samson Kisung'uda anasema wakati watoto wao wanafungwa hawaoni manufaa ya mwekezaji huyu kwani hata hizo Sh 1.8milioni huwa hawazipati kwa wakati."Hadi sasa mwezi Agosti hajatupa hizo fedha.

Bajeti ya kijiji tayari imepita, mwaka jana alitoa mwezi wa 11 baada ya kulalamika sana serikalini na mwaka 2004 hakutoa kabisa hatujui nchi hii inakwenda wapi?"anahoji Kisung'uda.
Awali eneo hilo lenye mgogoro, katika mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji, lilitengwa kama eneo la malisho, lakini hivi karibuni liliingizwa kinyemela katika eneo la pori la akiba la Grumet jambo ambalo linawafanya wafugaji wa kijiji hicho kukosa eneo la malisho.

"Katika hili eneo Mto Rubana unapita na miaka yote tumekuwa tukipeleka mifugo kunywa maji sasa baada ya mipaka ya pori kuingizwa hadi sehemu ya kijiji ndio sababu kila mara wafugaji na wananchi wanakamatwa kwa madai ya kuingiza mifugo kwenye pori," analalamika Kisung'uda.
Eneo hilo ndiko walikoshikwa watoto hao wanaotumikia kifungo na akina mama wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara wakienda kuchukua kuni za kupikia.

Kutokana na matukio hayo kijiji kimechoka. Mwenyekiti huyo anasema hawaoni manufaa ya mwekezaji huyo kwani serikali imeficha mkataba wake. Wanaitaka serikali iuweke wazi mkataba huo na ieleweke wazi kiasi cha fedha anazotoa kwa vijiji saba vinavyozunguka eneo alilokodishiwa na serikali ni za kisheria au msaada tu.

Diwani wa kata ya Hunyali, Sumera Kiharata ambaye vijiji vyake vinne vinapakana na mwekezaji huyo, anasema hata yeye kama diwani na mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Bunda hajui mkataba na mwekezaji huyo na serikali unasemaje.

"Hapa tuna mgogoro wa muda mrefu na jambo hili la kukamatwa watoto na kunyanyaswa wananchi tumelifikisha hadi vikao vya chama na serikali lakini inaonekana hakuna ufumbuzi kwani hata halmashauri ya wilaya haijui mkataba wa mwekezaji na serikali," anasema Kiharata.
Pamoja na malalamiko ya viongozi hao wa kata na kijiji, mkuu wa wilaya ya Bunda, Chiku Gawallawa anasema mwekezaji huyo, licha ya kuchelewesha fedha za vijiji na kukamata watoto, ana manufaa makubwa katika wilaya hiyo.

"Ni kweli kuna ucheleweshaji wa fedha, hilo tutalisukuma lakini huyu mwekezaji ni muhimu sana kwa wilaya nzima na hizo fedha za mwaka 2004 ambazo hawakupata vijiji zilitumika katika miradi mingine ya maendeleo," anasema Gallawa.

Kuhusu watoto waliokamatwa, Gallawa anasema walikubali kutumika kama ngao, pale wafugaji wanapovamia eneo la mwekezaji na kuingiza mifugo kwa kisingizio cha kufuata maji Mto Rubana.
"Ni kweli kuna watoto walishikwa kwa kuingiza mifugo eneo la pori la akiba la Grumet siku hiyo wananchi wengi walijitokeza kutaka kufanya vurugu na ili kujilinda waliwatanguliza mbele watoto kama ngao. Ila nadhani watoto walikwishaachiwa," anasema mkuu huyo wa wilaya bila kuwa na uhakika juu ya mahali waliko watoto hao.

Migogoro, mkuu huyo wa wilaya anakiri kwamba imekuwa mingi katika wilaya hiyo kutokana na kuwepo wafugaji ambao ni wahamiaji haramu, hatua ambayo inalazimisha kuendesha operesheni ya kuwaondoa wafugaji hao.

Anasema mifugo mingi imevamia wilaya hiyo hatua ambayo inasababisha kukosekana kwa eneo la malisho hadi kufikia wananchi kung’ang’ania kuchungia mifugo eneo la pori la akiba la Grumet.
Mkuu wa wilaya inaelekea hajui kitu maana taarifa yake hiyo inapingana na taarifa ya meneja wa pori la akiba la Grumet, Mathias Rwegasira anayesema wilaya hiyo inayozungukwa na mapori ya akiba na hifadhi ya taifa ya Serengeti, inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa malisho ya mifugo.

Anasema tangu pori hilo lilipotangazwa rasmi mwaka 1994 kumekuwa na migogoro ya mipaka hasa katika kijiji cha Mariwanda kutokana na wananchi kudai kuna eneo lao la asili na malisho limeingizwa katika eneo la pori la akiba.

"Huwa wanakuja ofisini wanaomba kibali kwenda katika eneo hilo ili kufanya mambo yao ya asili na tumekuwa tukiwapa kibali lakini tatizo kubwa ni kuingiza mifugo," anasema Rwegasira.
Meneja huyo anasema kampuni ya Grumet ina mkataba na serikali kuwinda kitalii na kuhifadhi eneo la ukubwa wa hekta za mraba 400 katika pori la Grumet na nyingine 500 pori la Ikirongo huku eneo la Ikoma sasa kumeanzishwa hifadhi za jamii (Wildlife Management Area-WMA).
Wananchi wa Bunda ambao wanaishi katika vijiji vinavyopakana na mwekezaji, wanasema wao hawapingi uwekezaji ila mazingira ambayo serikali inayaweka kwa kuwakumbatia sana hata wawekezaji wanapokiuka sheria ndicho wanacholalamikia.

Hata hivyo, Rwegasira anakiri kuwepo malalamiko ya wananchi juu ya mwekezaji huyo, lakini anasema miaka ya hivi karibuni wamejitahidi sana kuyapunguza kwani awali askari wa mwekezaji walikuwa wakilalamikiwa sana.“Hata kamati ya bunge ilifika hapa na kuulizia masuala haya ila tunajitahidi kuyashughulikia na sasa matatizo yanapungua kwani awali askari wa mwekezaji walijipa madaraka makubwa na hivyo kusuguana na wananchi," anasema.

Kuhusu kukamatwa na kufungwa watoto watatu, Rwegasira anasema yeye hana taarifa hizo japo kuwa alikiri kuwahi kusikia malalamiko alipotembelea vijiji vinavyozunguka pori hilo.Wakati Gallawa na Rwegasira hawajui hatima ya watoto hao, Mkuu wa gereza la kilimo la Serengeti, Deogratius Rwanga anakiri gereza lake kuwa na watoto wawili kati ya hao watatu na siku hiyo walikuwa wameondoka asubuhi kwenda machungani.

"Ni kweli tuna hao vijana hapa ila muda huu wapo machungaji," anasema Rwanga. Hii ndiyo hali halisi ya wilaya ya Bunda ambayo inaacha maswali mengi ni kipi kipaumbele cha serikali kati ya wananchi wake na wawekezaji.

*Mwandishi wa makala haya mwenye makazi yake mkoa wa Arusha anapatikana 0754296503 Email mussasiwa@gmail.com

Jamani naomba habari hizi muzifwatilie kwa kina na tujue mwisho na hatima ya watoto hao walio jela. Tunasema vijana Taifa la Kesho, sasa tukiwaweka vijana jela ndio watakuwa Taifa la Kesho kweli?

Habari hii nimeipata kutoka http://michuzijr.blogspot.com

Tuesday, September 1, 2009

EPA yazaa deni jipya

SERIKALI imetakiwa kuilipa Benki Kuu Tanzania (BOT) deni la sh bilioni 135 lililosababishwa na hasara iliyotokana na matatizo ya uendeshaji wa Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), iliyokuwa katika benki hiyo.

Serikali imekubali kubeba mzigo huo lakini imekiri kushindwa kulilipa kwa mara moja hivyo imeamua kuanza kulipa deni hilo taratibu huku ikichajiwa riba ya asilimia 8.5 mpaka mwaka 2028.

Taarifa za kuaminika zimebainisha kuwa benki hiyo imepata hasara hiyo baada ya kulazimika kuwalipa waliokuwa wakidai fedha zao zilizohifadhiwa katika akaunti hiyo kwa vipindi tofauti vilivyokuwa na viwango tofauti vya ubadilishanaji wa fedha za kigeni kati ya mwaka 1985 na Juni 30, mwaka jana.

Kukiri kwa Serikali kwamba hasara hiyo italipwa, kumeifanya benki hiyo itarajie kujipatia pato litokanalo na riba hiyo la Sh bilioni 10.8 kwa mwaka, ambayo ni tofauti na malipo ya deni hilo.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, BoT imepeleka taarifa kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, ikimkumbusha kuwa jukumu la uendeshaji wa EPA iliyokuwa NBC, lilikuwa la Serikali na hivyo hasara yake haistahili kubebwa na benki hiyo.

BoT imemkumbusha Mkulo kuwa mwaka 1985, benki hiyo ilipewa dhamana ya kusimamia akaunti hiyo kwa niaba ya Serikali na hivyo ikalazimika kuihamishia akaunti hiyo kutoka NBC kwenda BoT. Taarifa hiyo ambayo 'HabariLeo' inayo, iliendelea kueleza kuwa akaunti hiyo wakati ikihamishiwa BoT, ilikuwa na Sh bilioni 6.6 tu.

Ilibainisha kuwa malipo mbalimbali kwa waliokuwa wakidai kwa fedha za kigeni kutoka katika akaunti hiyo, yaliendelea kufanyika kati ya mwaka 1985 hadi Juni 30, mwaka jana wakati ambao akaunti hiyo ilisimamishwa.

Taarifa hiyo iliendelea kumbainishia Mkulo kuwa katika kipindi hicho, kulikuwa na tofauti za viwango vya ubadilishanaji fedha za kigeni na za Tanzania.

Ilikumbusha pia kwamba kwa kuwa malipo yalitolewa kwa fedha za kigeni kwa wadai ambao walikuwa ni wa kigeni, tofauti za viwango vya kubadilishana fedha za kati ya mwaka 1985 na mwaka jana, ziliisababishia benki hiyo hasara ya Sh bilioni 135.

HabariLeo ilizungumza na Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye alifafanua kuwa deni hilo limetokana na ucheleweshaji wa malipo ya wadai ambao walipaswa kulipwa kwa fedha za kigeni na mabadiliko ya viwango vya kubadilisha fedha hizo za kigeni.

Profesa Ndulu alifafanua, kwamba wafanyabiashara wa Tanzania katika miaka ya 1980 walilipa fedha za ndani NBC iliyokuwa ya Serikali na kuruhusiwa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, ambapo NBC ilipaswa kutafuta fedha za kigeni na kulipa waliowauzia Watanzania bidhaa.

Alibainisha kuwa wakati huo fedha hizo za kigeni zilikuwa zikipatikana BoT na katika benki ya NBC pekee ambayo ilikuwa ikimilikiwa na Serikali. Kwa mujibu wa Profesa Ndulu, kutokana na upatikanaji mdogo wa fedha hizo za kigeni, malipo kwa waliowauzia Watanzania bidhaa, yalicheleweshwa huku kiwango cha kubadilisha fedha kikipanda kutokana na kushuka kwa thamani ya sarafu.

“Kwa mfano, BoT ilipochukua EPA, ilichukua fedha zilizohifadhiwa kwa kiwango cha ubadilishanaji wa Sh 7.14 kwa dola, lakini wakati wa kulipa deni, ililipa kwa kiwango cha Sh 1,000 kwa dola na Serikali ikasema itafidia tofauti,” alisema Ndulu.

Alibainisha kuwa tofauti ya Sh 7.14 waliyoichukua kutoka NBC na kujikuta ikilipa Sh 1,000 kwa waliokuwa wakiidai NBC, ndiyo hasara waliyoipata. Alisisitiza iwapo Serikali ingekataa kulipa deni hilo, Sh bilioni 69 zilizorejeshwa na wafanyabiashara waliodanganya kuwa sehemu ya wadai, wasingeziruhusu zitumike kwenye kilimo na badala yake wangezitumia kufidia sehemu ya hasara hiyo.