Saturday, July 5, 2014

Wanaume wa tarime wakataa ukeketaji




Na Deogratius Temba
WANAUME kutoka katika kata ya Nyamaraga kijiji cha Ng,ereng’ere wilaya ya Tarime Mkoani Mara wamewataka wanaume wote kukataa kuoa wasichana waliokeketwa ili kukomesha kabisa  mila hizo potofu.
Akizungumza katika Tamasha la Jinsia ngazi ya wilaya lililofanyika katika kata hiyo nje kidogo ya mjini wa Tarime linaloongozwa na TGNP Mtandao, Mchungaji wa kanisa la PEFA, Getagasembe,  Roberty Machera  amesema kuwa  suala ya ukeketaji linahitaji jamii nzima ya Tarime, wanaume na wanawake kuunganisha nguvu kupambana nalo.

“ tunahitaji mabadiliko ya haraka, wanaume wakatae kwa nguvu zote  kuwakeketa watoto wao wa kike na kuoa wanawake waliokeketwa ili tuweze kuua kabisa mila hii kandamizi ambayo inaharibu haki ya msingi ya mwanamke” alisema mchungaji Machera
Amesema wanaume wa Tarime wanapaswa kubadilika,  na ndio watakao weza kuondoa kabisa mila hiyo kama wanataipinga na kuungana na  wasichana wao wanaokataa kukeketwa” mimi ni mwanamke mkuria  kama nitasema nakataa binti aliyekeketwa  itakomesha  kabisa kwasababu hata wale wanawake wanaopenda kukeketwa watakataa na kuunganisha nguvu nasi” aliongeza

Kwa upande wake Meneja  wa Idara ya Utafiti, uchambuzi na ushawishi TGNP, Mary Nsemwa  alisema kuwa  wananchi wa Tarime ni lazima kuachana kabisa na mila hiyo na kuondoa dhana ya kufikiri kuwa utajiri wa mali utatokana na kukeketa wasichana na kuwaoza kwa umri mdogo. “achaneni kuwatumia wasichana kama vyombo vya starehe, kujichumia mali,  Tarime ni sehemu yenye utajiri wa ajabu, ardhi nzuri yenye rutuba, maji, madini, misitu, hali ya hewa nzuri, tutumie rasilimali hizo kujipatia utajiri lakini sio  wasichana” alisema Nsemwa
Tamasha hilo linaendeshwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa na Maarifa Nyamaraga, na kushirikisha mashirika mengine kama Oxfam, Kivulini,  na wanaharakati wengine wanaofanya kazi na TGNP kutoka wilaya za Kishapu, Mbeya vijijini, Morogoro Vijijini, na Kinondoni Dar es salaam.

No comments: