Saturday, July 19, 2014

Tunataka katiba yenye mrengo wa Kijinsia-wanaharakati



 
 mtoa mada mwanachama wa TGNP Aseny Muro akizungumza kwenye GDSS juzi

wanawake kutoka ngazi ya jamii wakifuatilia kwa umakini rasimu ya katiba

Mjadala ukiendelea GDSS

WANAHARAKATI wa masuala ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia  wamelitaka Bunge maalum la katiba kujadili  kwa makini vifungu vya rasimu ya pili ya Katiba ili kuhakikisha inabeba masuala ya jinsia hasa kutambua usawa wa jinisia katika nyanja zote.
Akizungumza wakati wa mjada wa wazi  kuhusu “Kwa nini misingi ya usawa wa jinsia ilindwe katika katiba mpya” mwanachama mwanzilishi wa TGNP Mtandao Aseny Muro, alisema kuwa Wabunge wa Bunge maalum la katiba wanapaswa kutumia muda vizuri kujadili kwa undani na utulivu kifungu kwa kifungu na kuhakikisha katiba mpya inakuwa ya mrengo wa kijinsia.
“kwanza tunawataka kulinda vifungu vyote vya kijinsia ambavyo vimeingizwa kwenye rasimu hii hii pia tunawataka kubeba masuala ya msingi ya kijinsia hasa katika eneo la tunu za taifa,  ibara ya tano imezungumza juu ya Tunu, wahakikishe suala la usawa wa kijinsia liwe ni moja ya tunu za taifa”alisema Muro
Muro alisema kuwa usawa unaozungumzwa sio  mapinduzi ya wanawake dhidi ya wanaume bali ni kudai kuwepo kwa dhana ya usawa wa kijinsia katika mgawanyo wa rasilimali zote, ajira, elimu, na rasilimali za taifa kwa makundi yote yaani wanaume na wanawake walio pembezoni ambao hawapati nafasi au fursa ya kufikia hayo.
Akizungumza katika mjadala huo  uliohudhuriwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam,  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi alisema  lolote ambalo linataka kuendelea ni lazima litambue  maendeleo ya watu wote au makundi yote wanawake na wanaume bila kujali uwezo, hali na nafasi zao.
“taifa huru linaloendelea  linatakiwa kuwa linajali  na kutambua  maendeleo ya wanawake ambao ndio wazalishaji wakubwa.  Na hili litafanikiwa kama suala la usawa wa jinsia litaingizwa kwenye katiba mpya”alisema Liundi
Mwisho
                                                                                           

No comments: