Thursday, July 24, 2014

Katiba mpya ifute viti maalum- wanaharakati




WANAHARAKATI kutoka mashirika mbalimbali nchini wamependekeza katiba mpya ijayo ifute kabisa mfumo wa kuwa na viti maalum na kuweka mwingine utakaotambua uwakilishi sawia wa wanawake na wanaume katika vyombo vya uwakilishi.
Pia wamewataka wajumbe wa Bunge maalum la katiba linalotarajia kuendelea wiki ijayo mjini Dodoma kuhakikisha wanasimamia  kwa umakini vifungu vyote vinavyolinda usawa wa kijinsia katika uwakilishi wa wananchi na mgawanyo wa rasilimali  katika rasimu ya pili ya katiba mpya iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.












Wakizungumza wakati wa Semina ya Maendeleo na Jinsia (GDSS), iliyofanyika katika viwanja vya TGNP Mtandao- Mabibo wanaharakati hao kwa pamoja walisema kuwa mfumo wa sasa wa viti maalum  haufai kwani unawadhalilisha na kuwadhoofisha wanawake kiutendaji na kuwaweka pembezoni zaidi.
Mtoa mada katika jukwaa hilo la wazi lilofanyika katika viwanja vya TGNP Mabibo Jumatano jioni, Mjumbe wa Mtandao wa Wanawake na Katiba na mwanachama mwanzilishi wa TGNP, Aseny Muro alisema kuwa  Tanzania inahitaji kuboresha mfumo wa uwakilishi unaozingatia usawa wa kijinsia katika ngazi zote na wanaopewa nafasi wawe na mamlaka kamili ya maamuzi tofauti na sasa mbavyo wabunge wa viti maalum bado hawana uwezo wa kuamua au kufanya maamuzi katika majimbo wanayotoka   kama walivyo wabunge wa kuchaguliwa.
“Usawa wa jinsia kwenye uwakilishi unatakiwa kuanzia ngazi zote, kuanzia ngazi ya kijiji au mtaa, hadi watendaji wote wa serikali kuu,  kuongeza wabunge pekee pia ahaitasaidia kama watendaji wa serikali ni jinsia moja na ndio wanaofanya maamuzi ya mgawanyo wa rasilimali. Tunataka kuona watendaji wa vijiji, kata, wilaya, mikoa, wizara na idara za serikali  ambao uwiano wao ni sawia kijinsia:” alisema Muro
Aliongeza kuwa kwa hali ilivyo na jinsia mchakato wa Kuandaa katiba mpya unavyokwenda  kuna haja ya kufuta kabisa mfumo wa  viti maalum na kupitisha mfumo wa uwakilishi wa majimbo wa kila jimbo kuwa na Mbunge wa kuchaguliwa mwanamke  na endapo katiba mpya haitapitisha kifungu hicho  viti malum viendelee.
Akizungumza kwa niaba ya wezake wakati wa kuwasilisha  majumuisho ya washiriki, Hancy Obote, alisema kuwa katiba mpya inatakiwa kutamnbua waziwazi uwakilishi wa 50/50 bila kuweka masharti na kuwepo na usawa katika uwakilishi huo.
Alisema kuwa uwakilishi wa 50/50 ukibaki utaongeza sauti za pamoja katika vyombo vya maamuzi serikalini,  lakini viti maalum visiwepo kabisa
“Sisi kwa upande wetu tunaona viti maalum vifutwe kabisa na visiwepo baada ya hii katiba, tunadai kulindwa na kukubaliwa  kama ilivyoainishwa kwenye rasimu ya Pili ya Katiba mpya”alisema
Kwa upande wake Sophia Wambura kutoka Mtandao wa Wanawake na katiba alisema kuwa   kwa mujibu wa takwimu za idadi ya watu za mwaka 2012,  watanzania walio wengi asilimia 51 ni wanawake ili kuwa na taswira  ya utaifa ni lazima kuwa na uwiano wa 50 kwa 50 katika uwakilishi.
Anna Kikwa kutoka TGNP Mtandao alisema kuwa  awali viti maalum vilianzishwa kwa lengo la kuwainua wanawake ili waweze kuingia katika nafasi za maamuzi, wakue na baadaye wagombee, kama Katiba mpya itaingizwa kifungu cha kuwa na mgombea ubunge mwanamke na wakashinda basi viti maalum vinatakiwa kufutwa mara moja.
“ kama rasimu ya pili ya katiba isipopuitishwa au wakikitoa hiki kifungu kinachodai uasawa wa kijinsia kwenye Bunge, basi viti maalum viendelee kubaki katika mfumo ulipo hivi sasa” alisema Kikwa.

No comments: