Serikali imewataka wananchi
kuwatumia wasaidizi wa kisheria (paralegals) katika kutatua migogoro mbalimbali
ya kisheria wanayokabiliana nayo na kuepuka kupeleka mahakamani migogoro ambayo
inaweza kusuluhishwa nje ya Mahakama.
Wasaidizi wa kisheria ni
watu ambao hawana sifa za kuwa mawakili lakini kutokana na uzoefu na ujuzi wao
wanaweza kufanya kazi za usaidizi wa kisheria na hivyo kushiriki katika kutatua
migogogoro mbalimbali katika jamii.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam leo (Ijumaa, Julai 18, 2014), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria
Mheshimiwa Angellah Jamsine Kairuki amesema kwa kufanya hivyo, wananchi
watakuwa wanashiriki moja kwa moja katika kupunguza mlundikano wa mashauri
mahakamani.
“Nichukue fursa hii kuwasihi
wananchi wanaokabiliwa na migogoro mbalimbali kuwatumia vyema wasaidizi wa
kisheria katika utatuzi wa migogoro,” amesema Naibu Waziri Kairuki katika
mkutano wake wa majumuisho ya ziara ya siku tano jijini Dar es Salaam ambapo
alizitembelea taasisi 13 zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi
wasio na uwezo.
Taasisi hizo alizotembelea
Naibu Waziri Kairuki ni pamoja na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS),
Envirocare, Kamati ya Msaada wa Kisheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM-LAC), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST),
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Kituo cha Msaada wa
Kisheria kwa Wanawake (WLAC).
Taasisi nyingine
zilizotembelewa ni Kituo kinachoshughulikia Maslahi ya Wanawake na Watoto
(TWCWC), Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wajane na Watoto (CWCA), Chama cha
Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo
Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Nyumba ya Amani na Ofisi ya Mfuko wa Huduma za
Kisheria (LAF).
Mafanikio na
changamoto
Katika mkutano huo, Naibu
Waziri Kairuki amesema ameshuhudia mafanikio mengi katika ziara yake yakiwemo
kuanzishwa kwa kada ya wasaidizi wa kisheria ambao wanawafikia wananchi wengi
kwa ukaribu katika maeneo yao na kuwapa msaada wa kisheria.
“Wasadizi hawa wameweza
kutatua migogoro mingi katika jamii zetu bila kufikisha nashauri mahakamani na
hivyo kupunguza uwezekano wa mlundikano wa mashauri mahakamani,’ amesema.
Ametaja mafanikio mengine
aliyokutana nayo kuwa ni pamoja na asasi hizo kushiriki katika mapambano dhidi
ya ukimwi, ukatili wa kijinsia na kingono pamoja na baadhi ya taasisi kuanza
kutumia huduma za kisasa katika kutoa huduma zikiwemo simu za mkononi.
“Baadhi ya taasisi kama
TAWLA wanatoa huduma kupitia namba 0800751010 (Vodacom) na namba 110017 (TTCL)
wakati WLA wanatoa huduma kupitia namba 0800780100 ….hii ni kazi nzuri,”
amesema.
Kuhusu changamoto
alizokutana nazo katika ziara yake, Naibu Waziri Kairuki amesema amepokea
malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi mahakamani na malalamiko ya rushwa katika
vyombo vinavyojihusisha na utoaji wa haki. Changamoto nyingine ni pamoja na
uelewa mdogo wa wananchi kuhusu nafasi ya wasaidizi wa kisheria katika utatuzi
wa migogoro.
Chombo cha mpito
(LAS) kuratibu utoaji msaada wa kisheria
Kwa mujibu wa Naibu Waziri
Kairuki, kutokana na mchango mkubwa wa taasisi zinazotoa msaada wa kisheria kwa
wananchi, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeunda chombo cha
mpito kinachoratibu shughuli ya utoaji huduma za msaada wa kisheria nchini
kinachofahamika kama Sekretariaeti ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid
Secretariat).
“Kupitia sekretarieti hii,
wadau wanaotoa msaada wa kisheria wanapata ruzuku kutoka Serikalini ili kuweza
kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo,” amesema Naibu
Waziri Kairuki katika mkutano uliohudhuriwa pia na Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti
hiyo wakiwemo Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, Bi. Theodosia Muhulo na Bw. Gideon
Mandes.
Naibu Waziri ameongeza kuwa
tangu Sekretarieti hiyo iundwe mwezi Agosti, 2012 hadi mwishoni mwaka wa fedha
uliopita (Juni, 2014), Serikali na wadau wa maendeleo walikuwa wametoa zaidi ya
Tshs 1.55 bilioni kwa taasisi 20 zinazotoa huduma za msaada wa kisheria nchini.
“Na kimsingi asilimia 97 ya
fedha za kuendesha LAS zinatolewa na Serikali na asilimia tatu inatoka kwa
wafadhili,” amefafanua Naibu Waziri Kairuki ambaye ni mwanasheria kitaaluma na
kuongeza kuwa kutokana na uwezeshaji huo, mafanikio kadhaa yamepatikana kama
alivyoshuhudia katika ziara yake.
Kairuki ameongeza kuwa
kupitia fedha hizi, Sekretarieti imeweza kuwafikia na kutambua walipo watoa
huduma za msaada wa kisheria na kuanzisha kanzidata (database) inayoonyesha
hudua wanazotoa na mahali walipo.
“Hii ni hatua kubwa sana
ikizangatiwa kuwa awali taasisi hizo zilitoa huduma bila kutambuliwa au
kutambuana jambo lililowanyima fursa ya kubadilishana uzoefu na kushirikiana
katika kutekeleza majukumu yao,” amsema.
Akiongea katika mkutano huo,
Kwa upande wake, Bi. Muhulo ambaye pia ni Mkurugenzi wa WLAC ameipongeza ziara
ya Naibu Waziri na kusema imeboresha mahusiano baina ya watoa huduma za msaada
wa kisheria na Seriali na kusisitiza ushirikiano huo ni muhimu katika utoaji wa
huduma bora za kisheria.
Kwa upande wake, Dkt.
Kijo-Bisimba ambaye pia ni Mkurugenzi wa LHRC amesema taasisi zinazotoa msaada
wa kisheria kwa wananchi zimefurahishwa na hatua ya Naibu Waziri Kairuki
kuzitembelea, kukutana na watumishi na wananchi wanaopata msaada wa kisheria
badala ya kusikia huduma hizo kupiti vyombo vya habari.
“Tumefurahishwa sana na
kututembelea…wengine wanasikia tu kutoka kwenye vyombo vya habari lakini yeye
ametembelea hadi sehemu tunazotoa huduma za msaada,” amesema Dkt. Kijo-Bisimba
na kushauri kuwa wakati umefika kwa kutungwa kwa sheria itakayowatambua
wasaidizi wa kisheria na kuratibu utendaji wao kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza katika mkutano
huo uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mandes ambaye
pia Wakili wa Kujitegemea ameishukuru Serikali kwa kuonyesha utayari wa kutunga
sheria itakayoratibu wasaidizi wa kisheria (paralegals) na kushauri kuongezwa
kwa kasi ili sheria hiyo ipatikane haraka.
Akifafanua kuhusu utungwaji
wa sheria itakayoratibu wasaidizi wa sheria, Naibu Waziri amesema maandalizi ya
kutungwa kwa sheria hiyo yamefikia hatua nzuri Serikalini kabla ya kupelekwa
bungeni.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment