Saturday, July 19, 2014

KAIRUKI ASHAURI WANANCHI KUZITUMIA ASASI ZA MSAADA WA KISHERIA



Serikali imewataka wananchi kuwatumia wasaidizi wa kisheria (paralegals) katika kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria wanayokabiliana nayo na kuepuka kupeleka mahakamani migogoro ambayo inaweza kusuluhishwa nje ya Mahakama.

Wasaidizi wa kisheria ni watu ambao hawana sifa za kuwa mawakili lakini kutokana na uzoefu na ujuzi wao wanaweza kufanya kazi za usaidizi wa kisheria na hivyo kushiriki katika kutatua migogogoro mbalimbali katika jamii.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Julai 18, 2014), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Angellah Jamsine Kairuki amesema kwa kufanya hivyo, wananchi watakuwa wanashiriki moja kwa moja katika kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.

“Nichukue fursa hii kuwasihi wananchi wanaokabiliwa na migogoro mbalimbali kuwatumia vyema wasaidizi wa kisheria katika utatuzi wa migogoro,” amesema Naibu Waziri Kairuki katika mkutano wake wa majumuisho ya ziara ya siku tano jijini Dar es Salaam ambapo alizitembelea taasisi 13 zinazotoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Angellah Jasmine Kairuki akiongea na waandishi wa habari katika mkutano wa majumuisho ya ziara yake ya siku tano katika taasisi zinazotoa msaada wa kisheria jijini Dar es Salaam. Ziara hiyo imemalizika leo (Ijumaa, Julai 18, 2014). Wengine ni Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria (LAS) Dkt. Hellen Kijo-Bisimba (kulia) na Bi. Theodosia Muhulo
Taasisi hizo alizotembelea Naibu Waziri Kairuki ni pamoja na Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Envirocare, Kamati ya Msaada wa Kisheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-LAC), Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST),  Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).

Taasisi nyingine zilizotembelewa ni Kituo kinachoshughulikia Maslahi ya Wanawake na Watoto (TWCWC), Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wajane na Watoto (CWCA), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Nyumba ya Amani na Ofisi ya Mfuko wa Huduma za Kisheria (LAF).

Mafanikio na changamoto
Katika mkutano huo, Naibu Waziri Kairuki amesema ameshuhudia mafanikio mengi katika ziara yake yakiwemo kuanzishwa kwa kada ya wasaidizi wa kisheria ambao wanawafikia wananchi wengi kwa ukaribu katika maeneo yao na kuwapa msaada wa kisheria.

“Wasadizi hawa wameweza kutatua migogoro mingi katika jamii zetu bila kufikisha nashauri mahakamani na hivyo kupunguza uwezekano wa mlundikano wa mashauri mahakamani,’ amesema.

Ametaja mafanikio mengine aliyokutana nayo kuwa ni pamoja na asasi hizo kushiriki katika mapambano dhidi ya ukimwi, ukatili wa kijinsia na kingono pamoja na baadhi ya taasisi kuanza kutumia huduma za kisasa katika kutoa huduma zikiwemo simu za mkononi.

“Baadhi ya taasisi kama TAWLA wanatoa huduma kupitia namba 0800751010 (Vodacom) na namba 110017 (TTCL) wakati WLA wanatoa huduma kupitia namba 0800780100 ….hii ni kazi nzuri,” amesema.

Kuhusu changamoto alizokutana nazo katika ziara yake, Naibu Waziri Kairuki amesema amepokea malalamiko ya ucheleweshaji wa kesi mahakamani na malalamiko ya rushwa katika vyombo vinavyojihusisha na utoaji wa haki. Changamoto nyingine ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu nafasi ya wasaidizi wa kisheria katika utatuzi wa migogoro.

Chombo cha mpito (LAS) kuratibu utoaji msaada wa kisheria

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kairuki, kutokana na mchango mkubwa wa taasisi zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeunda chombo cha mpito kinachoratibu shughuli ya utoaji huduma za msaada wa kisheria nchini kinachofahamika kama Sekretariaeti ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid Secretariat).

“Kupitia sekretarieti hii, wadau wanaotoa msaada wa kisheria wanapata ruzuku kutoka Serikalini ili kuweza kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo,” amesema Naibu Waziri Kairuki katika mkutano uliohudhuriwa pia na Wajumbe wa Bodi ya Sekretarieti hiyo wakiwemo Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, Bi. Theodosia Muhulo na Bw. Gideon Mandes.

Naibu Waziri ameongeza kuwa tangu Sekretarieti hiyo iundwe mwezi Agosti, 2012 hadi mwishoni mwaka wa fedha uliopita (Juni, 2014), Serikali na wadau wa maendeleo walikuwa wametoa zaidi ya Tshs 1.55 bilioni kwa taasisi 20 zinazotoa huduma za msaada wa kisheria nchini.

“Na kimsingi asilimia 97 ya fedha za kuendesha LAS zinatolewa na Serikali na asilimia tatu inatoka kwa wafadhili,” amefafanua Naibu Waziri Kairuki ambaye ni mwanasheria kitaaluma na kuongeza kuwa kutokana na uwezeshaji huo, mafanikio kadhaa yamepatikana kama alivyoshuhudia katika ziara yake.

Kairuki ameongeza kuwa kupitia fedha hizi, Sekretarieti imeweza kuwafikia na kutambua walipo watoa huduma za msaada wa kisheria na kuanzisha kanzidata (database) inayoonyesha hudua wanazotoa na mahali walipo.

“Hii ni hatua kubwa sana ikizangatiwa kuwa awali taasisi hizo zilitoa huduma bila kutambuliwa au kutambuana jambo lililowanyima fursa ya kubadilishana uzoefu na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao,” amsema.

Akiongea katika mkutano huo, Kwa upande wake, Bi. Muhulo ambaye pia ni Mkurugenzi wa WLAC ameipongeza ziara ya Naibu Waziri na kusema imeboresha mahusiano baina ya watoa huduma za msaada wa kisheria na Seriali na kusisitiza ushirikiano huo ni muhimu katika utoaji wa huduma bora za kisheria.

Kwa upande wake, Dkt. Kijo-Bisimba ambaye pia ni Mkurugenzi wa LHRC amesema taasisi zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi zimefurahishwa na hatua ya Naibu Waziri Kairuki kuzitembelea, kukutana na watumishi na wananchi wanaopata msaada wa kisheria badala ya kusikia huduma hizo kupiti vyombo vya habari.

“Tumefurahishwa sana na kututembelea…wengine wanasikia tu kutoka kwenye vyombo vya habari lakini yeye ametembelea hadi sehemu tunazotoa huduma za msaada,” amesema Dkt. Kijo-Bisimba na kushauri kuwa wakati umefika kwa kutungwa kwa sheria itakayowatambua wasaidizi wa kisheria na kuratibu utendaji wao kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mandes ambaye pia Wakili wa Kujitegemea ameishukuru Serikali kwa kuonyesha utayari wa kutunga sheria itakayoratibu wasaidizi wa kisheria (paralegals) na kushauri kuongezwa kwa kasi ili sheria hiyo ipatikane haraka.
Akifafanua kuhusu utungwaji wa sheria itakayoratibu wasaidizi wa sheria, Naibu Waziri amesema maandalizi ya kutungwa kwa sheria hiyo yamefikia hatua nzuri Serikalini kabla ya kupelekwa bungeni.
Mwisho.

No comments: