Saturday, July 19, 2014

Matokeo ya Kidato cha Sita: Pigo kubwa kwa masikini hasa wanawake nchini



Matokeo ya Kidato cha Sita:
Pigo kubwa kwa masikini hasa wanawake nchini
Na Deogratius Temba
WATANZANIA wanafuatilia kwa karibu masuala mbalimbali yanayowahusu ikiwa ni sehemu ya kudai mabadiliko  ya mfumo wa uchumi, sera sheria  na bajeti ili kuhakikisha kuwa raslimali za Taifa zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote wanawake na wanaume  hususani wale waliotupwa pembezoni. Jukumu hili ni kuhakikisha kuwa tunaisukuma serikali kutimiza wajibu wake kwa kuboresha huduma za kijamii ili makundi yote yaweze kunufaika kwa kiwango kizuri.
                                                                                                                            
Suala la elimu bora ni la msingi ndio maana kwenye wadau wa elimu  wanadai na kulilia kila mara  upatikanaji wa elimu bora ambayo  ni sanjari na vifaa, chakula,  mabweni hasa ya wasichana, walimu wenye ujuzi na  mazingira rafiki ya kufundishia wanafunzi wote wa Kitanzania  wanawake na wanaume.

Matokeo ya mitihani ya  kidato cha sita uliofanyika Mwezi Mei 2014, yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa(NECTA) yametutia wasiwasi juu ya mustakhabali wa elimu nchini kutokana na kiwango cha ufaulu kwa wasichana kushuka kwa kiasi kikubwa kulinganisha na mwaka jana 2013. Kutokana na matokeo haya kunahitajika uwanjibikaji wa dhati kwa watendaji wa Wizara ya Elimu na Tamisemi ili kuboresha kiwango cha elimu.

 Jambo la kushangaza tena kusukitisha ni kiwango cha ufaulu. Haiajawahi tokea Tanzania matokeo kama haya na bila shaka hayatatokea, wengine tumeitafsiri hii kama ni sehemu ya kutekeleza mpango wa Matokeo makubwa sasa ambao kweli matokeo yamekuwa makubwa. Tujiulize kama tunapanua magoli ili wachezaji wafunge kwa wingi tunategemea nini?  Wingi wa shule na vyuo vikuu unatupofusha tunasahau ubora wa elimu yetu?

Pamoja na kwamba matokeo  ya jumla yameonesha kupanda kwa kiwango cha ufaulu, tumekuwa na wasi wasi juu ya ubora wa ufaulu kutokana na kuendelea kuwepo kwa tatizo la uhaba wa vifaa vya kufundishia katika shule za msingi, sekondari na hata vyuo vya elimu ya Kati. Matokeo yameonesha kuwa ufaulu umetoka asilimia 87.85% mwaka 2013 hadi 95.98% mwaka huu. Ni ajabu kwasababu tukumbuke kuwa hata haya matokoe ya 2013 tulilalamika kuwa yaliongezwa ili kupata idadi kubwa ya wahitimu watakaojiunga na vyuo vikuu.  

Matokeo ya mwaka huu yanatokana na wahitimu waliofanya mtihani 40,695  ambapo  kati yao 38,905(95.98%)wamefaulu kwa daraja la I hadi IV, wakati mwaka 2013 waliofanya mtihani ni 50,611 na waliofaulu mwaka jana walikuwa 44,366 (87.85%), uchambuzi unaonesha kuwa idadi ya watahiniwa imepungua mwaka huu lakini idadi ya waliofaulu imeongezeka, lakini suala la msingi ni ubora wa ufaulu na  uwiano wa wahitimu na waliofaulu kijinsia.

Jambo la kushangaza ni kwamba matokeo hayataji jumla ya wahitimu kijinsia ili uweze kulinganisha na waliofaulu. Jambo la kujiuliza wakati takwimu za sensa ya watu na makazi zimeonesha kuwa   wanawake Vijana ni wengi kuliko wanaume zaidi ya asilimia 50 ya watu wote, lakini wasichana wanaohitimu elimu za juu wanazidi kushuka.  Tujiulize wapo wapi wasichana wengine mbona hawaonekani kwenye elimu za juu? Tumewaacha wapi?  Jumla ya watahiniwa wote  waliofaulu wasichana ni 12,085,  wavulana wakiwa ni 26,825, ya watahiniwa wote. Jumla ya watahiniwa 30,225(85.73%) wamefaulu kwa kiwango cha daraja la I hadi III wakiwemo wasichana 9,954,  na wavulana ni 20,271 (83.5%) ya wavulana wote. Tunaona jinsi ambavyo hakuna uasawa katiika udahili wa kidato cha tano na ndivyo itakavyokuwa kwenye elimu ya chuo kikuu, na baadaye kwenye nafasi za ajira kwasbabu hatutakuwa na wanawake wamama waliosoma.

Mbaya zaidi kwetu wanajamii ni kwamba, katika matokeo ya mwaka huu, wavulana wameonesha kuongoza kwa ufaulu  wengi wakiwa wameongoza kwenye masomo ya sayansi huku wasichana wakiongoza kwenye masomo ya Biashara na lugha/sanaa.  Kwetu sisi hili tunaona kuwa ni tatizo linalotokana na kukosekana kwa nia ya dhati ya kuwekeza kwenye shule za serikali ambazo ndiko wanakosoma watoto wa masikini.  Shule za serikali ndizo za watanzania masikini  lakini hazifaulishi au hakuna ubora wa elimu inayotakiwa. Shule nyingi za serikali hazina madawati ya kutosha, vitabu, walimu wa sayansi, maabara, mabweni na vifaa vingine muhimu.

Kutokana na takwimu hizi inasikitisha kuona idadi kidogo ya wasichana waliofaulu au kufikia mwisho wa masomo ya kidato cha sita. Hatuwezi kujivunia ufaulu wakati wasichana  watakaojiunga na elimu ya chuko kikuu ni 9,954 kati ya watahiniwa  40,695.  Tofauti ya wavulana na wasichana ni kubwa na kamwe hatuwezi kupigania usawa wa kijinsia kwa kuchana kwa kiasi hiki kwenye elimu.

 Kutokana na utafiti wa kiraghibishi  uliofanywa na TGNP Mtandao Mbeya Vijijini, Kishapu na Morogoro mwanzoni mwa mwaka huu 2014  ulionekana wazi kwamba maeneo mengi hasa  ya vijijini wanafunzi wengi hasa wasichana hawana makazi  rafiki na salama yaani mabweni, vifaa vya kusomea, walimu na maji, miundombinu mibovu na kupelekea wengi wao kupata ujauzito na kuacha masomo

Kundi kubwa la wasichana linalohitimu darasa la saba halifiki kidato cha sita kwababu hakuna nia ya dhati ya kuwajengena mazingira ya kufika kiadato cha nne salama, mfano kijiji cha Usoha njia panda kata ya Tembela, Mbeya Vijijini, wasichana 14 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2010  katika shule ya sekondari Ikhoho ni watatu pekee waliohitimu wengine wamepata ujauzito na kucha masomo. Hapo  watoto wa matajiri na viongozi wapo shule za binafsi tena za bweni. Hapa kuna usawa wa Kijinsia? Je tujivunie ufaulu huu wa kibaguzi ambao maelfu wanaostahil kuwepo shuleni wameachwa? Tutafakari!



No comments: