Friday, January 28, 2011

Kizungumkuti Dowans

-Kikwete atofautiana na Ngeleja, Jaji Werema
-Sitta, Mwakyembe waombwa kutoa mwongozo

RAIS Jakaya Kikwete ametofautiana na kauli ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, akikubaliana na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokimbilia kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans, Raia Mwema, imeelezwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya kikao cha wabunge wa CCM, badala yake, Rais ameungana na wabunge hao kutafuta namna ya kuepuka malipo au kuyapunguza kwa kutumia mianya ya kisheria.

Awali, mara baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara kutoa hukumu ikitaka Dowans ilipwe na Tanesco (serikali) shilingi bilioni 94 ikiwa ni faini kwa kuvunja mkataba, AG Werema na Waziri Ngeleja walitoa kauli za kuilipa Dowans endapo tu itasajili hukumu hiyo Mahakama Kuu.

Walitoa uamuzi huo wa kuilipa Dowans bila kueleza nia ya kukata rufaa au mazingira yanayokwamisha ukataji rufaa, huku Waziri Ngeleja akisisitiza kuwa, hatua zozote za kutofanya malipo hayo ni kupoteza muda na kwamba ni kusababisha nchi kutozwa riba.

Uamuzi huo wa Ngeleja na Werema uliungwa mkono na baadhi ya viongozi mashuhuri nchini, akiwamo Jaji Mark Bomani, lakini ukipingwa na wengine wakiwamo wasomi.

Rais atofautiana na Waziri, AG

Sakata hilo la Dowans sasa limechukua sura mpya, likiweka kitendawili hatima ya Waziri Ngeleja pamoja na Mwanasheria Mkuu, Werema.

Wiki hii imependekezwa na wabunge wa CCM katika azimio maalumu kwamba; Serikali isikimbile kulipa na badala yake, mianya ya kisheria ivumbuliwe ili kukwepa malipo au kuyapunguza.

Mapendekezo hayo ni kinyume cha kauli ya Waziri Ngeleja na Jaji Werema. Vitisho vya Ngeleja kwamba kutolipa kwa sasa ni kusababisha nchi kutozwa riba ni kama vimepuuzwa na wabunge hao.

Taarifa za ndani ya kikao cha wabunge wa CCM kilichofanyika kuanzia wiki iliyopita na kilichomalizika Jumatatu, zinaeleza kuwa Rais Kikwete ameungana na wabunge wa chama hicho, ambao pia Ngeleja ni miongoni mwao.

Msimamo huo wa wabunge hao unaungana na mitazamo ya Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe. Kwa nyakati tofauti, tena hadharani viongozi hao walimpinga Ngeleja, kiasi cha kufichua kuwa suala hilo halijajadiliwa kwenye Baraza la Mawaziri.

Hata hivyo, hoja kwamba suala hilo halikuwa limejadiliwa na Baraza la Mawaziri ilipingwa na Ngeleja akisema hakukuwa na haja ya kujadili suala hilo huko kwa kuwa liko wazi mno.

Kauli ya Mwanasheria Mkuu

Wiki hii Raia Mwema liliwasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Werema ili kufahamu mambo mawili katika taswira hii mpya ya Dowans.

Kwanza, madai ya baadhi ya wabunge wa CCM wakati wa mjadala kwamba; amejigeuza msemaji wa Serikali katika baadhi ya masuala badala ya kubaki mshauri.

Kati ya masuala ambayo AG aliyazungumzia kwa vyombo vya habari katika tafsiri inayotajwa kuwa alijigeuza msemaji (mkuu au mwisho) wa Serikali ni suala la Dowans na Katiba mpya. Akisema Dowans italipwa na Katiba mpya hakuna, isipokuwa marekebisho.

Suala la pili katika mawasiliano hayo na AG Werema lilihusu uamuzi wa ofisi yake kutotaka kukata rufaa na badala yake kutaka Dowans ilipwe endapo itasajili tozo (hukumu) yake Mahakama Kuu.

Msingi wa maswali hayo ni uamuzi wa wabunge wa CCM, waliokutana chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, ubungo, jijini Dar es Salaam, Januari 22 hadi 24, mwaka huu.

Akijibu Werema alitoa majibu ya jumla akisema; “Kuhusu hayo ya wabunge wa CCM kwa kweli sikuwapo katika kikao hicho, kwa hiyo bado sijui kumetokea nini au wameazimia nini.

“Lakini kwa sababu chama (CCM) ndicho kinaongoza Serikali basi yakiletwa kwetu (ofisi ya Mwanasheria Mkuu) tutayashughulikia.”

Hatima ya Sitta, Mwakyembe

Kwa mujibu wa mwenendo wa kikao cha wabunge hao wa CCM, hali ya mjadala wa Dowans ilionekana kukera wengi katika malipo yanayopaswa kufanywa kwa kampuni hiyo.

Inadaiwa na baadhi ya watoa habari kuwa; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete walikuwa wakiongoza mjadala huo katika mwelekeo wa kutokuridhika na hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Inaelezwa kuwa Rais Kikwete wakati wa mjadala huo alionekana kuwapa nafasi Sitta na Mwakyembe kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu mianya ya kukwepa malipo hayo, akitumia lugha ya “watoe mwongozo.”

Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge lililoshiriki mijadala ya Richmond na Dowans, wakati Mwakyembe akiwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond na kusababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, wanatajwa kujenga hoja zao kwa kuegemea zaidi uhalali wa Dowans ambayo kimsingi imetokana na kampuni ya mfukoni ya Richmond.

Sitta na Mwakyembe ambao ni wanasheria kitaaluma kwa sehemu kubwa wanatajwa kufanikiwa kuwashawishi wabunge hao kuridhia azimio la kusaka fursa za kisheria ili kutolipa mabilioni hayo kwa Dowans.

Wengine wanaotajwa kuwapo katika harakati hizo kiasi cha kujitolea kupambana kisheria ili Dowans ama isilipwe au malipo yapunguzwe ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.

Mkono aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi dhidi ya kesi iliyofunguliwa na Kampuni ya City Water, iliyoshindwa kutekeleza mkataba wake wa kusambaza hudumu ya maji safi Dar es Salaam na mkataba wake kuvunjwa, baada ya uamuzi wa Baraza la Mawaziri, chini ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Mbali na Mkono, mwingine aliyeshiriki kuzungumzia suala la malipo kwa Dowans katika wigo wa kisheria ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge, ambaye wakati wa Awamu ya Tatu, nchi iliingia mikataba mingi yenye utata.

Pinda ajaribu kufukia mashimo

Hata hivyo, katika kumuondolea ‘kiwingu’ Waziri Ngeleja, Waziri Mkuu Pinda ameeleza kuwa; kitendo cha kupishana kauli kati ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Ngeleja, kilitokana na ugeni katika kazi za uwaziri.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda bado inatajwa kuwa tata kwa kuzingatia rekodi za uzoefu katika uwaziri kati ya Ngeleja na Sitta.

Utata wa kauli Pinda unaibuka kwa kuzingatia ukweli kuwa Sitta ni mzoefu katika utendaji wa Serikali na amewahi kuwa waziri na wizara mbalimbali.

Kati ya Wizara alizopata kuongoza ni Ujenzi na ile iliyokuwa Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba (sasa ni Wizara ya Katiba na Sheria).

Kwa upande wake, Waziri Ngeleja amekuwa katika nafasi hiyo kwa takriban miaka minne sasa, kuanzia Februari, mwaka 2008.

Chiligati katika tuhuma nzito

Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, John Chiligati, ambaye pia ni Mbunge, naye yuko katika wakati mgumu.

Anadaiwa kutia chumvi hasa mtazamo au hisia binafsi tamko la kikao cha Kamati Kuu kuhusu sakata la Dowans. Chumvi anayotajwa kuikoleza Chiligati ni kutokana na kudai kwake kuwa Kamati Kuu “imebariki” malipo kwa Dowans.

“Suala hilo limewekwa wazi na Mwenyekiti kwamba haukuwa uamuzi wa Kamati Kuu kubariki malipo kwa Dowans, isipokuwa Kamati Kuu ilishauriwa kuruhusu michakato ya kisheria kuchukua nafasi na si kutoa uamuzi wa kulipa,” kilisema chanzo cha habari katika kikao hicho.

Kauli ya Msekwa kuhusu Kamati Kuu

Gazeti hili liliwasiliana na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, kufahamu kilichojiri kwenye Kamati Kuu, hadi ielezwe kulikuwa na upotoshaji.

Msekwa alijibu; “Achana na uamuzi wa Kamati Kuu, umekwishapitwa na wakati. Uamuzi wa sasa wa wabunge wa CCM ndiyo uamuzi wa Chama.

“Kama ilivyopendekezwa zichukuliwe hatua za kisheria na si kuchukua hatua za kulipa, huo ndiyo msimamo wa sasa wa chama.”

UVCCM walia na Dowans

Katika hali isiyotarajiwa, wakati Kamati Kuu ikikutana Ikulu, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi ulikutana na waandishi wa habari, Hoteli ya Peacok, Dar es Salaam.

Hawa walitoa tamko wakisema Dowans isilipwe lakini kama kuna ulazima wa kulipa basi, wasibebeshwe mzigo huo Watanzania wote, bali walipe wanasiasa waliolifikisha hapo Taifa.

Taarifa za uhakika zinabainisha kuwa hatua hiyo imewakera baadhi ya viongozi wa sekretariati ya CCM na mmoja wa viongozi wa Serikali anatajwa kuanza kuwanunia vijana hao, akisema wamemuhujumu.

Katika utaratibu usio rasmi, vijana hao wanadaiwa kufokewa na baadhi ya viongozi wa sekretariati ya CCM inayoongozwa na Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, lakini wamekuwa wakiweka msimamo wao wazi kuwa; “Ni jumuiya huru katika kutoa mitazamo yake kuhusu hali ya kisiasa na mwenendo wa Taifa.”

Upinzani wamezea mate Dowans

Uamuzi wa hivi karibu wa wabunge wa CCM umetanguliwa na nia ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, aliyeweka bayana tangu kutolewa hukumu hiyo ya Dowans kwamba; atawasilisha suala hilo bungeni.

Kwa mujibu wa Kafulila, alipanga kuhoji nchi imefikishwaje hapo kuilipa kampuni hiyo ambayo kimsingi imetokana na kampuni ya mfukoni ya Richmond.

Kafulila alikuwa tayari kuliomba Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani ya Waziri wa Nishati na Madini, Ngeleja au na serikali nzima.

Kama ilivyo kwa Kafulila wa NCCR-Mageuzi, CHADEMA kwa upande wao walikuwa wakitazama suala hilo kwa ukaribu na taarifa zinabainisha wamepanga kulifikisha Bungeni wao binafsi au kwa kumuunga mkono Kafulila.

Hata hivyo, kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa suala hilo halitafikishwa bungeni kwa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kujadili siasa wakati suala ni la kisheria zaidi, ni kama inakwamisha ndoto za wanasiasa hao wa upinzani nchini.

Mtiririko wa sinema ya Dowans

Suala la Dowans limekuwa likichua sura tofauti kila kukicha. Mara baada ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa kibiashara kutolewa, Desemba mwaka jana, vyombo vya habari vimeonyesha wakati fulani mwelekeo wa ushabiki.

Lakini wakati baadhi ya vyombo vya habari vikiwa katika ushabiki, huku wasomi na wanasiasa mashuhuri wakiwa katika mgongano wa maoni, wananchi wa kawaida walionyesha kutokubali kulipa deni hilo.

Msimamo huo wa wananchi wa kawaida umebebwa na asasi za kiraia ambazo zimefungua kesi katika Mahakama Kuu kuitaka Mahakama hiyo kutoridhia hukumu ya Mahakama ya Kimataifa, kuilipa Dowans mabilioni hayo.

Mahakama ilipokea ombi hilo la asasi za kiraia. Katika hatua nyingine, kwa kuwa Dowans walipaswa kuwasilisha hukumu hiyo ili ipate nguvu za kisheria nchini, wanadaiwa kutofanya hivyo.

Badala ya kuwasilisha hukumu hiyo ambayo imejumuisha uovu wa kampuni ya Richmond ndani yake, Dowans wanadaiwa kuwasilisha viambatanishi tu mahakamani hayo. Mahakama kwa sasa inasubiri hukumu hiyo kutoka mikononi mwa Dowans.

Hisia za wananchi mitaani

Kutokana na uamuzi wa Shirika la Umeme Tanzania kupandisha bei za umeme, kumekuwapo na hisia miongoni mwa wananchi kuwa, ongezeko hilo la bei linalenga kukusanya fedha za kuilipa Dowans Sh bilioni 94.

Hisia hizi zimewahi kupingwa na Waziri Ngeleja katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema mwezi huu, bali hali iko hivyo kutokana na Tanesco kutaka kujimudu kiuendeshaji.

1 comment:

Anonymous said...

Hi there.
This is my first visit to your blog! We are a team of volunteers and starting a
new initiative in a community in the same niche.
Your blog provided us useful information to work
on. You have done a extraordinary job!

Keep updated and take a look at my web page
at Learn about Offshore Banks for additional info.