Tuesday, January 25, 2011

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA




TAARIFA YA WIZARA KULAANI MAUAJI YA WATOTO WANNE (4) YALIYOTOKEA WILAYA YA KARATU, ARUSHA.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imesikitishwa na kuwepo kwa taarifa za mauaji ya kutisha ya watoto katika familia mbalimbali nchini ambapo baadhi ya wazazi wamekuwa wakiripotiwa kuhusika na mauaji ya watoto hao.

Hivi karibuni ilitaarifiwa kuwa baba mzazi Samweli Daudi aliwauwa watoto wake wawili kwa kuwakata mapanga hadi kufa katika kijiji cha Mwenei wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambaye anaye aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kubaini kuwa amewaua wanaye. Katika tukio hilo watoto Kulwa Daudi (5) na Abel Daudi (4) waliopoteza maisha yao. Watoto wengine wawili Elizaberth Kashirima (1), Dotto Kahabi (5) na mzee Daudi Kahabi (50) walijeruhiwa na wanaendelea na matibabu.

Tukio lingine la aina hiyo lilitokea januari 4 mwaka huu katika kijiji cha Makere mkoani Kigoma ambapo mwanakijiji Filbert Kafonogo aliwauawa watoto wake watatu kwa kuwakata mapanga naye akajinyonga kwa kamba. Ilielezwa kwamba alifika uamuzi huo baada ya kutuhumiwa na familia yake kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa watoto wake wa kuzaa.

Ukatili mwingine wa kutisha ni wa mauaji ya watoto wanne wa familia moja, waliouawa kwa kukatwa na shoka kisogoni kitendo kilichofanywa na baba yao mzazi, ambaye naye alijinyonga hadi kufa baada ya mauaji ya watoto hao. Taarifa inaeleza kuwa Evans Damian (43) ambaye ni baba wa watoto hao alikuwa na ugomvi wa kifamilia kwa muda mrefu na kusababisha kumfukuza mkewe na kisha akafanya mauaji hayo dhidi ya watoto wake wanne.

Wizara inakemea vikali mauaji ya watoto hao ambao ni Theophil Evans (10) mwanafunzi wa darasa la tatu, Ritha Evans (8), na watoto wawili mapacha Dibimo Evans (4) na Theodory Evans (4) wote wanafunzi wa darasa la awali katika wilaya ya Karatu. Taarifa kutoka kijijini zinaeleza kuwa, kabla ya tukio hilo la marehemu Evans alimuua nyani na kunywa damu yake.

Aidha, kitendo cha mauaji haya dhidi ya watoto wasio na hatia ni cha kikatili na kinapotokea katika ngazi ya familia kinarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukiukwaji wa Haki na Ustawi wa Mtoto. Mauaji haya yamewakosesha watoto hao haki yao ya msingi ya kuishi kitendo kinachopingana na katiba ya nchi yetu pamoja na mikataba ya Kimataifa ya Haki na Ustawi wa Mtoto ambayo nchi yetu imeridhia.

Hivyo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inahimiza jamii kubadilika na kuhakikisha kuwa familia ambayo ndiyo kitovu cha jamii yote panakuwa ni mahala salama penye upendo, amani na mshikamano miongoni mwa wanafamilia; na kuwapatia watoto haki zao za msingi ikiwemo haki ya kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kuendelezwa. Ni vema wanafamilia wakawa wavumilivu na kuchua maamuzi yenye kuzingatia maslahi ya watoto ili kuepusha maafa.

Aidha, Wizara inatoa wito kwa wanajamii kubaini matukio yasiyo ya kawaida yanayotendwa na baadhi ya wanafamilia na kuyafuatilia kwa karibu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika vyombo husika ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea na kuhatarisha uhai na usalama wa jamii.

Wizara inatoa rambirambi kwa mama, ndugu na jamaa wa watoto waliouawa maana maisha yao yamekatishwa kwa kupokonywa haki yao ya kuishi katika umri mdogo kutokana na kufanyiwa mauaji hayo ya kikatili. Wizara inawaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki cha majonzi mazito.



Hussein A. Kattanga

KAIMU KATIBU MKUU

24 Januari, 2011

No comments: