ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, amewataka Watanzania kutomchagua kiongozi muongo na muoga katika kutekeleza na kusimamia ukweli kwa mambo anayoyaamini katika kuliletea taifa maendeleo.
Askofu Shao aliyasema hayo wakati akiwasilisha salamu za mkuu wa kanisa hilo nchini, Dk. Alex Malasusa kwa waumini wa kanisa hilo katika Usharika wa Moshi Mjini ikiwa ni sehemu ya Ibada ya Jumapili.
Alisema kila inapofika wakati wa uchaguzi, watu wa kada mbalimbali hujinadi mbele ya wananchi kuomba kura huku wakitoa ahadi tofauti kwa wapiga kura ili hali wakijua kuwa ahadi hizo ni za uongo.
“Ninazungumza na viongozi wanaotafuta kura kwa wananchi baadaye katika uchaguzi mkuu mwaka huu, nawasihi msiogope kutoa ahadi za kweli, simamieni ahadi za kweli….acheni kigugumizi katika hili, mtahukumiwa kutokana na matendo yenu,” amesema.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza ahadi zao na kuacha tabia ya kuangalia nyuma, bali wasimame katika mtazamo wa baadaye; lengo kuu likiwa kuleta chachu ya maendeleo kwa wananchi wao.
“Mnaposimama kuomba kura kwa wananchi mnazungumza na kutoa ahadi nyingi za kuvutia, ukichaguliwa na baadaye kuulizwa ulichoahidi, unakosa jibu….tekelezeni ahadi zenu leo, hiyo kesho ni ya manyani,” alisema.
Akizungumzia suala la maendeleo, Askofu Shao alitoa changamoto kwa viongozi waliopo madarakani kuhakikisha wanasimamia vyema rasilimali zilizopo ili kuwaletea wananchi maendeleo badala ya kufanya masuala kwa faida yao.
Alisema pamoja na kwamba Tanzania ni nchi yenye rasilimali nyingi, lakini bado ni masikini kutokana na mifumo iliyopo ambayo haitoi kipaumbele kwa masuala yanayolenga kumkomboa mwananchi wa kawaida.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa kidini aliwataka viongozi kumrudia Mungu na kuhakikisha wanatenda masuala ambayo yameamrishwa katika maandiko matakatifu kuliko kufuata masuala ya kidunia zaidi.
No comments:
Post a Comment