BAJETI ya Serikali ilipitishwa juzi jioni huku matumizi kadhaa, yakiwamo ya Ikulu, yakiwa yamepanda kutoka Sh. bilioni 7.23 hadi bilioni 8.8, yakigusa posho, safari za nje, ununuzi vinywaji na vitafunio kwa ajili ya kukirimu wageni na matengenezo ya magari ambayo hivi karibuni yalikumbwa na matatizo wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa katika ziara jijini Dar es Salaam.
Ongezeko la matumizi hayo linakwenda sambamba na ongezeko la bajeti Sh. trilioni 9.5 hadi Sh trilioni 11.1.
Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo viwango vya fedha vilivyotengwa katika bajeti inayokwisha vimepunguzwa katika bajeti ya sasa ya mwaka wa fedha 2010/2011. Miongoni mwa maeneo hayo ni safari za ndani ya nchi ambazo fungu lake limekatwa kutoka Sh. milioni 732.4 hadi Sh. milioni 668.4 zinazokadiriwa kutumika mwaka mpya wa fedha.
Fungu hilo la safari za ndani limeonyesha mwelekeo wa kupungua mwaka hadi mwaka na kwa Mwaka wa Bajeti wa 2008/2009 lilikuwa na Sh. 839,807,283.
Katika eneo la matengenezo ya magari, ambayo hivi karibuni yalizua mtafaruku baada ya kung’oka matairi, mwaka jana zilitengwa Sh. milioni 120 ambazo katika mwaka huu wa bajeti zimepanda hadi Sh. milioni 167.4.
Fungu kwa ajili ya posho limeongezeka kutoka Sh. milioni 611.9 hadi milioni 713.9 wakati matumizi kwa ajili ya mafuta na vimiminika vingine vya magari yameongezwa kutoka Sh. milioni 344.9 hadi milioni 389.8.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo ya Serikali iliyopitishwa na Bunge Jumatatu, bajeti kwa ajili ya matumizi ya kukirimu wageni ikiwamo ununuzi wa vinywaji, vitafunio na huduma nyingine aina hiyo Ikulu yameongezeka kutoka Sh. milioni 444.4 za mwaka unaokwisha wa bajeti hadi Sh milioni 566.44.
Ununuzi wa mashuka, nguo, viatu na huduma (za utunzaji wake) umetengewa fungu la nyongeza kutoka Sh. milioni 116.4 hadi milioni 160.
Kwa upande wa safari za nje makadirio yaliyopitishwa na Bunge mwaka huu yanaonyesha kuwa yamepanda kutoka Sh milioni 115. 9 za mwaka unaokwisha hadi milioni 164 . Mwaka wa bajeti wa 2008/2009, safari hizo ziliidhinishiwa Sh. milioni 77.8.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kiwango kinachopitishwa cha matumizi ya Serikali wakati mwingine hutumika na kumalizika kabla ya wakati uliopangwa na matokeo yake ni ongezeko la matumizi ambayo yanalazimika kuidhinishwa kwa hati ya dharura na Bunge.
Ofisi ya Makamu wa Rais fungu lake la matumizi limeongezeka kutoka Sh 4,492,974,000 za mwaka unaokwisha wa bajeti hadi Sh bilioni 4,542,109,000 zikigusa matengenezo ya magari kutoka milioni 144 hadi milioni 168.
Hata hivyo, katika hali inayozua maswali mengi ofisi hiyo ya Makamu wa Rais katika bajeti mbili mfululizo Bunge limekuwa likipitisha fedha kwa ajili ya ukarabati wa mabomba ya maji na mfumo wa umeme.
Mwaka jana na mwaka huu wa bajeti eneo hilo limetengewa kiwango kinacholingana ambacho ni Sh milioni 20, wakati mwaka juzi zilitengwa Sh milioni 17.
Matumizi haya ya Serikali yameongezeka wakati kukiwa na maelezo miongoni mwa waziri kuwa Tanzania imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mtikisiko wa uchumi duniani, ulioanzia Marekani, Ulaya na baadaye kuathiri nchi za Afrika.
Lakini pia matumizi hayo yanapanda katika wakati ambao wananchi wamekuwa wakilalamika na kuitaka Serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na wakati huo kuwekeza zaidi katika maeneo ya miradi ya maendeleo inatajwa kuwa uwekezaji wake kutoka serikalini umekuwa dhaifu na kwamba kwa kiasi kikubwa miradi hiyo inategemea fedha za wahisani.
Katika bajeti ya mwaka huu, nchi wahisani zimepunguza kiwango cha msaada wao kwa serikali ya Tanzania hali iliyolazimu Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Uchumi kuingia katika mazungumzo na Benki binafsi ya Stanbic, ili ikopeshwe kiwango cha fedha kufidia pengo la wafadhili. Serikali imepanga kukopa Stanbic Sh bilioni 346 katika lugha inayoelezwa na serikali kuwa ni kwa “masharti nafuu” ili kuhakikisha matumizi yake yanatimia.
Source:raimwema.co.tz
No comments:
Post a Comment