MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa amewaambia viongozi wa Chama Cha Jamii (CCJ), waende tu mahakamani kwa kuwa ni sehemu yao ya kutafuta haki.
Aidha, amesema ana wasiwasi kama Msemaji wa Chama hicho, Fred Mpendazoe, kama jina lake halimo kwenye orodha ya fomu za majina na pia kama ana kadi ya chama hicho; kama ilivyokuwa kwa viongozi wakuu wa chama hicho kilichosajiliwa kwa muda Machi mwaka huu.
Tendwa aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa anasonga mbele na kazi ya uhakiki kwa mikoa iliyopangwa kwa mujibu wa ratiba.
Hatua ya kwenda mahakamani kwa CCJ imetolewa na Mpendazoe juzi akidai kutokuwa na imani na utendaji wa Msajili huyo pindi alipoanza kazi ya uhakiki wa wanachama wa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kuwa uhakiki sio sahihi na una mizengwe.
“Mahakama ni sehemu ya kila mmoja kutafuta haki, mimi nimetenda haki na kila mmoja ameshuhudia hilo, sasa kama kwa kuwa wanatafuta haki waende tu mahakamani,” alisema Tendwa kutokana na kauli ya chama hicho ambacho kimekuwa kikiilazimisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukipatia usajili wa kudumu haraka ili kishiriki uchaguzi mkuu.
Tendwa alisema keshokutwa yeye na timu yake ya watu wanne akiwemo Naibu Msajili, watakuwa Zanzibar katika Mkoa wa Mjini Magharibi kwa ajili ya uhakiki kwa kuwa tamko la kusitisha ni fikra zilizokuja baada ya ratiba kupangwa na kazi kuanza.
Alisema tangu awali walishakubaliana na viongozi wa CCJ kuwa miezi sita itatosha kujipanga na kuhakikisha wanakamilisha vyema kazi ya uhakiki, lakini kinyume cha matarajio hayo, walikwenda ofisini kwake kwa kujiamini kuwa wako tayari kwa uhakiki.
“Chama kupata usajili wa kudumu sio kazi rahisi na matakwa yanayotakiwa yasipofanikishwa, inawezekana kuona kama ni ndoto kuupata usajili…kama ni haki, nimetenda kwa sehemu yangu,” alisisitiza Tendwa.
Alisema kilichopangwa ndio hicho hicho na kwamba ofisi yake hairudii kufanya uhakiki katika maeneo ambayo hawakuonesha mwelekeo na ieleweke kuwa duru ya kwanza ya uhakiki itamalizikia Zanzibar.
Aidha, alisema viongozi wa CCJ hawana umakini na kazi hiyo, hivyo huenda Msemaji wake, Mpendazoe hana kadi wala jina lake halipo kwenye fomu kama ilivyokuwa kwa viongozi wakuu, Mwenyekiti Richard Kiyabo na Katibu Mkuu, Renatus Mwabhi, ambapo hawakuwa na kadi na hata majina yao kutokuwepo katika fomu.
“Wakati nahakiki Mkoa wa Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CCJ, alikuwa na kadi, lakini jina halikuwepo kwenye fomu wakati Mwenyekiti yeye alikuwa hana kadi wala jina halikuwepo kwenye fomu...sasa iweje kwa Mpendazoe?” Alihoji Tendwa.
Kazi ya uhakiki kwa chama hicho kwa Mkoa wa Dar es Salaam ilipangwa Juni 3, katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke ambako vurugu zilitawala wakati Msajili alipotangaza wanachama halali walikuwa 13, kati ya wanachama 7,000 waliodaiwa kuwepo kwa mkoa huo; hatua iliyofuatiwa na viongozi wa CCJ kutangaza kusitisha kazi ya uhakiki kwa nchi nzima.
No comments:
Post a Comment