MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imesema kuruhusiwa ama kutoruhusiwa kwa mgombea binafsi, si suala la kisheria, hivyo haliwezi kuamuliwa na Mahakama hiyo, bali chombo sahihi chenye uamuzi ni Bunge.
Jopo la majaji saba katika uamuzi uliosomwa jana na Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, lilisema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuamuru kuruhusiwa kwa mgombea huyo, kwa kuwa suala hilo si la kisheria, bali ni la kisiasa zaidi.
Uamuzi huo unatokana na Serikali kukata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyompa ushindi Mchungaji Christopher Mtikila, anayetaka mgombea binafsi aruhusiwe.
Jaji Mkuu alisema Bunge ndilo lenye mamlaka ya kurekebisha sheria na si Mahakama, hivyo suala la mgombea binafsi linatakiwa lishughulikiwe na chombo hicho ambacho kimepewa mamlaka kikatiba ya kurekebisha Katiba yenyewe.
Katika uamuzi wake huo, Mahakama hiyo ilisema uamuzi wa kuanzisha mgombea binafsi utatokana na matakwa ya nchi na mahitaji ya wakati pia historia ya nchi kisiasa.
“Hoja hii sisi tunaona si ya kisheria, ndiyo maana tunasema Mahakama haina mamlaka ya kuruhusu mgombea binafsi, bali ni suala la kisiasa,” alisema Jaji Mkuu katika uamuzi ambao umeweka pembeni uamuzi wa Mahakama Kuu kwa vipindi viwili tofauti ukiruhusu mgombea binafsi.
Majaji wengine katika jopo hilo ni Eusebio Munuo, Januari Msofe, Nathania Kimaro, Mbarouk Salim, Bernard Luanda na Sauda Mjasiri.
Upande wa Serikali uliwakilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju, wakati Mchungaji Mtikila akiwakilishwa na Wakili wa Kujitegemea, Richard Rweyongeza.
Jaji Ramadhani alisema ni suala la uamuzi wa jamii husika kupitia wawakilishi wao, ambao ni wabunge, na wakiona kuna haja ya mgombea huru, wataamua kupitia kwao.
Katika uamuzi huo uliosomwa kwa saa moja na nusu, Jaji Ramadhani alisema pia kuwa Mahakama haina mamlaka ya kutamka kuwa vifungu vya Katiba vinakiuka Katiba yenyewe, kama ilivyofanya Mahakama Kuu.
Alisema inachoweza kufanya Mahakama baada ya kuona kuna vifungu vinavyosigana na vifungu vingine kwenye Katiba, ni kuvioanisha na si kufuta baadhi ya vifungu vya Katiba kama ilivyokuwa kwenye uamuzi wa Mahakama Kuu.
Alisema Mahakama inafanya hivyo kwa vile marekebisho ya Katiba yanayofanywa na Bunge ni tofauti na utungaji wa sheria zingine. Alisema marekebisho ya Katiba yanahitaji theluthi mbili ya wabunge wa Bara na Zanzibar.
Jaji Ramadhani alisema yapo mambo mengi kwenye Katiba ambayo yameanisha masharti mbalimbali yanayowataka wagombea wa uongozi wa kisiasa kuyazingatia.
Alitoa mfano wa mambo hayo kuwa ni mtu kuwa na umri wa miaka 21 kugombea ubunge, umri wa miaka 40 kugombea urais na lazima awe raia wa kuzaliwa.
“Itatokea mtu siku moja atakuja kuhoji kwa nini awe na miaka hiyo au kwa nini awe raia wa kuzaliwa … hizi ni busara tu zilizowekwa na watunga sheria kutokana na mahitaji ya nchi kwa wakati huo,” alisema Jaji Ramadhani.
Historia ya kesi ya mgombea binafsi ilifunguliwa kwa mara ya kwanza na Mchungaji Mtikila katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na Mahakama hiyo kupitia kwa Jaji Kahwa Lugakingira, ikaruhusu mgombea binafsi mara baada ya vyama vingi kuanza mwaka 1992.
Baada ya Serikali kubwagwa, ilikwenda bungeni na kufanya marekebisho ya sheria na kuvifanya vifungu vilivyotajwa na Mahakama kuwa vinatoa fursa ya kuwapo mgombea binafsi, vikaondolewa na kutamka kuwa mtu anaruhusiwa kugombea kupitia vyama vya siasa.
Baada ya marekebisho hayo, Mtikila alifungua tena kesi Mahakama Kuu kwa maelezo kuwa marekebisho hayo yanakiuka haki za binadamu na yako kinyume cha Katiba.
Safari hiyo jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi Amir Manento likatamka kuwa vifungu vilivyorekebishwa na Bunge vinakiuka Katiba yenyewe.
Majaji hao wakaenda mbali zaidi na kumwagiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa mazingira kuanzia hukumu hiyo ilipotolewa hadi uchaguzi wa Oktoba kuwe na sheria inayoruhusu mgombea binafsi.
Baada ya hukumu hiyo, Serikali haikuridhika ikakata rufani ambayo jana majaji hao walibainisha kuwa suala hilo si la kuamuliwa na Mahakama, bali Bunge.
Jaji Ramadhani alisema uamuzi huo umetolewa baada ya kuzingatia hoja za mkata rufani na mkatiwa rufani na zilizowasilishwa na Marafiki wa Mahakama; wahadhiri waandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Palamagamba Kabudi, Profesa Jwani Mwakyusa, Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar, Othman Masoud na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Rajab Kiravu.
Katika kuchambua hoja mbalimbali Mahakama ilikataa hoja ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la kikatiba.
Lakini ilikubaliana naye kuwa Mahakama kamwe haiwezi kujitwisha majukumu ya Bunge ya kurekebisha Katiba wala kufuta vifungu vya Katiba husika.
Lakini majaji hao walikubaliana na Wakili Rweyongeza, kuwa Bunge lina mipaka yake katika kutunga sheria, kwani haliwezi kutunga sheria bila kuzingatia misingi ya Katiba yenyewe.
Akielezea uamuzi huo, Wakili Rweyongeza alisema ni mzuri, kwani umekubaliana na hoja zao licha ya kuwa tofauti na matarajio yao.
“Suala la kwenda mbele zaidi ni la mlalamikaji, sisi kazi yetu tuliyopewa imeishia hapa, hatuwezi kuendelea zaidi ya hapa,” alisema Rweyongeza.
Kwa upande wake, Mchungaji Mtikila alisema hukumu hiyo ni aibu kwa Idara ya Mahakama nchini; kwa kile alichosema ni wa kisiasa ambao haukuzingatia misingi ya sheria.
“Sikushangaa walipomwita Mkurugenzi wa NEC na kada wa CCM Kabudi kuja hapa kuishauri Mahakama … lakini sitachoka, nitakwenda kushauriana na wanasheria wangu, kuona ni sehemu gani tunaweza kwenda ili haki ipatikane.
“Haki itakayopatikana si ya Mchungaji Mtikila, itakuwa ni haki ya raia wote wa nchi hii, ambao wanahitaji mabadiliko ya kweli,” alisema.
Alidai Mahakama ya Rufani imetoa uamuzi ili kumfurahisha Rais Jakaya Kikwete ambaye chama chake, CCM, kinaogopa wagombea binafsi, kwani wanajua kuna watu watajitokeza na watawabwaga wa CCM.
No comments:
Post a Comment