Monday, June 21, 2010

Suala la mgombea binafsi: Mtikila kwenda kimataifa

BAADA ya Mahakama ya Rufani mwishoni mwa wiki kuliachia Bunge kutoa uamuzi kuhusu kuruhusiwa ama kutoruhusiwa kwa mgombea binafsi, Mchungaji Christopher Mtikila aliyefungua kesi hiyo awali katika Mahakama Kuu amesema hakuridhishwa na uamuzi huo na baada ya wiki moja kuanzia jana, atalipeleka suala hilo katika mahakama za kimataifa.

Sambamba na hatua hiyo, Mtikila ametangaza nia ya kugombea urais kupitia chama chake cha DP na kueleza atatangaza siku ya kuchukua fomu.

Mtikila aliyasema hayo jana, Dar es Salaam katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Rufani kwa suala la mgombea binafsi na nia yake ya kuwania urais mwaka huu huku akisisitiza kuwa anachukua hatua hiyo kutetea wananchi na si kwa maslahi yake.

“Kama nilivyosema awali, Mahakama imeonesha udhaifu mkubwa na udhalilishaji wa idara hiyo inayotekeleza haki za binadamu duniani kote, ni wazi kuwa wananchi hawajaridhishwa, sasa wanasheria wangu na wengine wanajiandaa, ikiwa tayari tutapeleka katika mahakama za kimataifa,” alisema Mtikila.

Alizitaja mahakama hizo kuwa ni Mahakama ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Umoja wa Afrika na kuitaka Mahakama ya Rufani kupitia upya rufani hiyo kwani imedhalilisha idara hiyo.

Mchungaji Mtikila alisema amewapa nafasi mawakili na wanasheria wengine walioko upande wake kuchambua uamuzi huo na kupitia sheria za kimataifa hivyo baada ya wiki moja, watakuwa tayari huku akijigamba kuwa hatua hizo zikishindikana, hatosita kuingia msituni.

Alisema ingawa hukumu hiyo imekuwa ya kihistoria kwa kutolewa na majaji saba, lakini imependelea upande mmoja wa serikali na ndiyo maana ameamua kwa kushirikiana na wanasheria wengine, kulishughulikia kimataifa.

Uamuzi huo umetolewa baada ya serikali kukata rufani kupinga uamuzi wa Mahakama kuu aliompa ushindi Mtikila ambaye anataka mgombea binafsi aruhusiwe.

Kesi kuhusu mgombea binafsi ilifunguliwa kwa mara ya kwanza na Mtikila katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na Mahakama hiyo kupitia kwa Jaji Kahwa Lugakingira ikaruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi.

No comments: