SERIKALI imekuwa ikipoteza Sh bilioni 300 kwa mwaka kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuchakachua mafuta ya taa na dizeli na petroli.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha Wafanyabiashara wa Mafuta Tanzania (TAOMAC) pamoja na Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kusafirishia Mizigo (TATOA), wametaka bei ya mafuta ya taa irekebishwe ili Taifa liepukane na tatizo hilo.
Aidha, wamesema kutokana na kazi ya uchakachuaji wa mafuta, zaidi ya magari 60 yaliyopeleka mizigo Rwanda yamerudishwa nchini, jambo ambalo linaisababishia nchi fedheha kubwa.
Mwenyekiti wa TATOA, Seif Seif amewaambia waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuwa, uchakachuaji unawaneemesha mafisadi wachache huku uchumi wa nchi ukididimia.
Seif alisema, Tanzania imekosa sifa ya uaminifu kwa nchi jirani zinazopitisha mizigo yake nchini ambapo inaonesha wazi jitihada zilizofanywa na Rais Jakaya Kikwete za kuzunguka nchi jirani kuomba wapitishe mizigo yao nchini, hazina matunda.
“Kazi ya uchakachuaji wa mafuta ni ugonjwa mbaya kuliko Ukimwi, unaipatia nchi fedheha huku mitambo ya injini ya vifaa vya usafiri ikiharibika ama kushindwa kufanya kazi kabisa, hali ambayo inatishia uchumi wa nchi,” alisema Seif.
Alisema nchini Rwanda, magari ya mafuta 29 yakiwa na petroli yalikataliwa kuingizwa nchini humo huku magari 31 yaliyokuwa na dizeli, kusafishwa na kutakiwa kulipiwa gharama za usafishaji.
Kwa Burundi, alisema magari 80 ya dizeli pamoja na petroli yalikamatwa na walikubali kuyasafisha ingawaje gharama zake zitalipwa na wamiliki wa magari.
Seif alisema serikali inapata hasara kubwa kutoka kwenye kodi ya mafuta ya taa, ambapo kila lita moja ya mafuta ya taa inayochukua nafasi ya dizeli hupotea Sh 462 na kwa lita ya petroli ni Sh 487.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taomac, Salum Bisarara alisema biashara ya kuchakachua mafuta ni ya hatari kuliko dawa za kulevya, na kwamba imekuwa ngumu kuikabili kutoka kwa mamlaka zilizopewa kazi hiyo.
“Hii ni biashara mbaya kuliko ile ya cocaine, na inawahusisha watu wachache ambao wanataka wafaidike nayo. Imekuwa ngumu kwa sababu nani atamfunga paka kengele,” alisema Bisarara.
Alisema licha ya juhudi za Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta (Ewura) kutaka kuweka alama katika mafuta ili kudhibiti uhalifu huo, bado litaendelea kwa sababu linawahusisha watu walio tayari kutumia fedha kuhakikisha tatizo linaendelea.
Alisema Tanzania inapoteza Sh bilioni 300 kwa mwaka kutokana na kodi inayopotea ambayo ni Sh bilioni 25 kwa mwezi, fedha ambazo alisema zingesaidia kuboresha maisha ya Watanzania.
Alipinga dhana ya kuwa kuongeza ushuru wa mafuta ya taa kuwataathiri wananchi wengi walalahoi, akisema “mafuta hayo ya taa mengi kwa sasa hayafiki viiijini, je, tunamzungumzia mwananchi yupi wakati hali hii inawanufaisha wachache.”
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mhazini wa TATOA, Zacharia Hans Pope, alisema ipo kampuni inayotoa mafuta ya taa lita 38,000 kila siku bandarini, na kuhoji mafuta hayo yanakwenda wapi. Haikutaja jina.
Hans Pope alisema tatizo la uchakachuaji ni kubwa na litaisababisha madhara makubwa nchi kuliko yale la kuendelea na ushuru mdogo wa sasa wa mafuta ya taa, ambao ndio mwanya unaotumiwa na watu wanaoendesha biashara ya uchakachuaji mafuta.
Kwa mujibu wa Bisarara, hivi karibuni walikuwa na kikao na wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini, na wote wameitaka serikali ipandishe ushuru wa mafuta ya taa.
1 comment:
Kutoa nafuu ya kodi kwenye mafuta ya taa kwa ajili ya watu wachache kutokuwa waaminifu ni kuwaumiza zaidi ya 80% ya watanzania wanatumia nishati hii kwa kupikia na taa vijijini.
EWURA wanatakiwa watekeleze wajibu kusayansi zaidi. Kama magari ya raisi yanauwezo wa kutambua petrol iliyochanganywa na mafuta ya taa, jee, EWURA haina vifaa vya kutambua hilo?
Ikumbukwe kuwa kwa kila Shs 100 katika nishati ya umeme na maji, mwanachi analipa Shs 2 EWURA sasa kama pesa wanazo kwa nini washindwe kithibiti tatizo?
Post a Comment