BAADHI ya wabunge wametilia shaka upatikanaji wa fedha za bajeti wa sh trilioni 11.6 huku wengine wakiipongeza kuwa imeonyesha mwelekeo wa kujitegemea.
Sambamba na hilo, wabunge wameonyesha wasiwasi na nguvu za kampuni za madini na kuhofia mikataba yao inaweza kuwa juu ya bunge baada ya Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, kuongeza maneno yaliyokuwa yamesahaulika katika bajeti yakielezea kusamehe kodi wawekezaji katika madini.
Wakitoa maoni yao baada ya kuwasilishwa bajeti hiyo ya mwaka 2010/2011, baadhi ya wabunge walielezea wasiwasi wao wa kuipata fedha hiyo ya bajeti kutokana na wafadhili kuonyesha hawana msimamo wa kutoa fedha walizoahidi.
Mbunge wa kuteuliwa, Ismail Jussa alisema “tuna uhakika gani kama wafadhili watatoa fedha wakati walishaonyesha mwelekeo wa kupunguza mchango wao katika bajeti”, alihoji.
Naye Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed(CUF) alisema ushahidi wa mwaka jana umeonyesha makusanyo ya ndani hayakufikia lengo lililokusudiwa hivyo hata mwaka huu kuna uwezekano wa lengo la makusanyo ya ndani kutotimia na hivyo bajeti kutotekelezeka kama ilivyokusudiwa.
Alisema bajeti ya mwaka ujao imeonyesha kuwajali zaidi watu wa kipato cha kati na cha juu na kufafanua “tumeona ushuru wa pikipiki imeongezwa hii inamaanisha tumewaongezea gharama watu wa chini kwani wao ndiyo wapanda pikipiki lakini kodi nyingi zimepunguzwa kwa mazao ya viwandani lakini mkulima hajazungumziwa hapo”.
Msemaji huyo wa kambi ya upinzani alisema kuwa kitendo cha serikali kukopa kwenye mabenki ya biashara ni kuwaongezea wananchi mzigo kwani riba itakayolipwa itatokana na kodi za wananchi.
Mbunge wa Bariadi Mashariki , John Cheyo(UDP) alisema bado serikali inaonekana kusuasua kupata mapato kutokana na rasilimali za nchi kama madini na bajeti hiyo imeonyesha kuwa mikataba ya madini imeiondolea serikali haki ya kisheria ya kupata maendeleo.
Kwa upande wa Mbunge Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto alisema kitendo cha kuondoshwa kodi ya mafuta kwa upande wa migodini kunaweza kuifanya migodi kuzalisha umeme wenyewe na kutonunua Tanesco hivyo fedha zao hazitaingia nchini.
Alisema bajeti hiyo ambayo hataiunga mkono imeua matumaini ya kuwainua wananchi na kufafanua “kipaumbele cha miundombinu utaona fedha zimewekwa nyingi kujenga barabara lakini robo ya fedha zote itaishia kulipa riba ya wakandarasi waliocheleweshewa kuanza miradi ya ujenzi na nusu yake italipa madeni yao ya nyuma pia sasa hapo barabara ngapi zitajengwa? Hakuna kitu”.
Hata hivyo Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni alisema kuna haja ya kupunguzwa fedha za matumizi ya kawaida. Bajeti inaonyesha matumizi ya kawaida ni sh trilioni 7.8 ikiwa ni ongezeko kutoka trilioni sita za mwaka unaomalizika wa bajeti.
Hoja hiyo pia ilizungumziwa na mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa ambaye alisema bajeti ni ya matumizi na si ya maendeleo kwa kuwa kati y ash. Trilioni 11 ni sh. trilioni 3 tu zinazokwenda katika maendeleo.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba(CCM) alipongeza bajeti aliyoiita imeonyesha nchi imeanza kujitegemea na kupongeza pia kuondoshwa kodi kwa mabasi yaendayo kasi kwani yatasaidia kuondoa foleni jijini Dar es Salaam ambayo imekuwa ikirudisha nyuma
uchumi wa nchi.
Mbunge wa Maswa, john Shibuda alisema bejti hiyo imeonyesha ni nyenzo ya kujitegemea na itaweza kupunguza kuwa ombaomba kwani imeonyesha kuimarisha makusanyo ya ndani.
No comments:
Post a Comment