Tuesday, June 22, 2010

Mbio za urais zaanza, Kikwete wa kwanza

RAIS Jakaya Kikwete amechukua fomu ya kuwania kugombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka mitano ijayo katika sherehe zilizopambwa na shamrashamra na vijembe vya Katibu Mkuu wa Chama hicho, Yusuf Makamba.

Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, alikabidhiwa fomu yake saa 5.38 asubuhi makao makuu ya CCM mjini hapa na Msimamizi wa Uchaguzi wa CCM, Makamba aliyetabiri kuwa Mwenyekiti wake, anaweza kuwa mgombea pekee wa chama hicho.

Makamba alisema kabla na baada ya kumkabidhi Rais Kikwete fomu kuwa anaweza kuwa mgombea pekee baada ya mwanachama mwingine aliyetangaza nia, Mbunge wa Maswa, John Shibuda, kujiondoa katika mchakato huo.

“Hili ni tukio kubwa na ndiyo tumeanza safari ya kwenda Ikulu,” Makamba aliuambia mkusanyiko wa wana-CCM wakiwamo wabunge, mawaziri, wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM, wenyeviti wa mikoa na wananchi wengine.

“Ipo dalili kuwa utakuwa peke yako, tutakutuma wewe, ipo dalili wengine hawatakuja,” alisema Makamba akimweleza Rais Kikwete kabla ya kueleza kuwa Shibuda alishaondoa nia yake na kutokana na hilo, mbunge huyo wa Maswa aliyekuwa kwenye shughuli ya jana, aliitwa mbele ya meza kuu na kupeana mkono na Rais Kikwete.

Makamba hakuishia hapo kwa vijembe na kauli zake zilizosisimua uchukuaji huo wa fomu, kwani kabla ya Rais Kikwete kutoa hotuba yake, alitumia muda mwingi kujitetea katika rafu zilizoanza kuchezwa katika majimbo ya wabunge wa CCM, ambazo zililalamikiwa hivi karibuni katika kikao cha wabunge wa CCM kabla ya Bunge la Bajeti kuanza ambalo ni la mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Mtendaji huyo wa CCM licha ya kukiri kupokea malalamiko ya wabunge hao, lakini alisema si yeye wala Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Pius Msekwa au Rais Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa CCM anayewatia kiburi wanachama hao waliotangaza nia, hivyo taratibu za chama zitachukua mkondo wake na asilaumiwe yeye.

“Chonde chonde akina Msekwa chukueni hatua…nami mwenzenu niokoeni, wapo waliotusaidia wameandika malalamiko, tuyafanyie kazi. Yapo kwa Msekwa, nimekupa (akimwambia Msekwa), wewe ni Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Maadili, yafanyie kazi. Mna haki ya kulalamika, kwani mkomamanga wenye makomamanga ndio unaopigwa mawe,” alisema Makamba. Lakini aliwataka wanaolalamika, wamtendee haki kwa sababu naye ni binadamu.

“Ni vizuri mkayasema haya tarehe 23 (kesho) wakati wa kikao cha NEC, pale ndipo mahali pake, Mwenyekiti atakuwapo, kule (bungeni) hapana.

Nami nikiulizwa, nitasema, Msekwa usikasirike,” aliongeza Makamba na kuwafanya waliohudhuria kuangua vicheko. Pia aliomba apewe nafasi ya kuzungumza katika Mkutano Mkuu wa CCM mwezi ujao kwa kumkaribisha Mwenyekiti, kwani ana ya kuzungumza kwa sababu ratiba iliyopangwa sasa, imemwengua.

Rais amekubali awekwe, ndio utaratibu. Mara baada ya Makamba kumaliza kuzungumza, alimpa nafasi Rais Kikwete aliyezitaja sababu zilizomfanya awanie tena nafasi hiyo kuwa ni ushawishi wa Watanzania wengi; kufanya vizuri kwa Serikali yake katika miaka mitano iliyopita na Katiba kumruhusu kuwania tena urais.

“Ushawishi wa Watanzania wengi, wana-CCM na wasiokuwa wana-CCM, wanawake kwa wanaume, vijana kwa wazee wa mikoa yote na wilaya zetu zote kwa kunitaka nigombee tena.

“Pili, nimeridhika kwamba katika miaka mitano hii, pamoja na kukabiliana na changamoto nyingi, Serikali chini ya uongozi wangu imefanya kazi nzuri ya kusukuma maendeleo ya Taifa letu na kuimarisha umoja, amani na utulivu katika nchi yetu.

“Na tatu, Katiba inaniruhusu, kwani naweza kuwa Rais kwa vipindi viwili mfululizo.

Nimemaliza kimoja, hivyo naweza kuomba kupata kipindi kingine cha pili,” alisema Rais Kikwete ambaye kabla ya hotuba yake, kadi yake ilihakikiwa na Makamba kuona kama ni mwanachama hai na kisha akalipa papo hapo Sh milioni moja za kuchukulia fomu na hatimaye kukabidhiwa.

Rais Kikwete alisema mwaka 2005 walimpa ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM na sasa anaiomba tena na kuahidi kuwa akiteuliwa, atafanya hivyo kwa dhati na hasa kama wana-CCM wakishikamana kama 2005, watapata ushindi mkubwa au kuzidi huo.

Alisema Watanzania na wana-CCM ni mashahidi kwa kiasi gani amekuwa mwaminifu kwa ahadi ya kutekeleza mipango na programu mbalimbali za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, aliyosema imetekelezwa kwa umakini mkubwa na matokeo yake yanaonekana pembe zote.

Aliueleza mkusanyiko huo, kwamba amefarijika kuona kwamba wao, pamoja na wana-CCM wenzake wengine nchini, wanamwamini kwamba anafaa kuendelea kuliongoza Taifa kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

“Hayo yote ndiyo yaliyonishawishi nami kushawishika kujitokeza kuomba tena kupewa nafasi ya kuliongoza Taifa letu. Safari ile nilisema mkinichagua nitafanya kazi kwa Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya na matokeo yake tumeyaona.

“Safari hii nasema mkinichagua nitawatumikia Watanzania kwa Ari Zaidi, Nguvu Zaidi na Kasi Zaidi katika dhamira yetu ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Kwa pamoja, tuzidi kusonga mbele,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na watu waliokuwapo.

Aliahidi kuwa akipewa nafasi ya kuwa mgombea wa CCM Oktoba mwaka huu, hatawaangusha na atatumia bidii yake yote kufanya kampeni ya kukipigania chama hicho tawala ili kipate ushindi mkubwa.

Awali, kabla ya shughuli ya kukabidhi fomu kwa mgombea huyo, Makamba alisema dalili za kuomba dua ya kuwa Rais Kikwete awe mgombea pekee zilizotolewa na watu kadhaa akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi, zimesikika.

Mbali na Ndejembi, shughuli hiyo ya kuchukua fomu ilihudhuriwa pia na wazee wengine wa CCM wakiwamo Peter Kisumo, Balozi Job Lusinde na Isaac Mwisongo.

Wabunge John Malecela (Mtera) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa zamani wa CCM, Dk. Abdallah Kigoda (Handeni) na Waziri Profesa Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki) ambao pia waliwania urais 2005, ni miongoni mwa waliokuwapo jana.

Familia ya Rais Kikwete ikiongozwa na mkewe Mama Salma Kikwete na wanawe saba, wavulana wanne wakiongozwa na kaka yao, Ridhiwani Kikwete na wasichana watatu, pia walimsindikiza baba yao, kama ilivyokuwa kwa kaka yake Kikwete, Suleiman Kikwete ambaye aliongozana na mkewe, kushuhudia mwanzo wa safari ya mpendwa wao kuomba ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.

No comments: