ILE siku ya hukumu kwa wanachama 11 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaowania uteuzi wa kugombea urais wa Zanzibar, imetimia.
Leo Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na Halmashauri Kuu (NEC) vinakutana hapa kufanya uteuzi na kisha kupiga kura ya kuchagua mgombea huyo miongoni mwa 11 waliojitokeza.
Awali, Kamati Kuu ilikuwa ikutane jana, lakini sasa itakutana leo kwanza kabla ya kupeleka majina au jina la mgombea mmoja kupigiwa kura NEC.
Tayari Dodoma imepambwa na rangi za kijani na njano zinazotumiwa na chama hicho tawala, huku kambi mbalimbali zikiwamba ngoma upande wao, katika mbio za nani atasimamishwa na CCM kuwania kumrithi Rais Amani Abeid Karume.
Wanachama 11 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo wakiwamo vigogo kadhaa ambao ni Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, Naibu wake ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma Shamuhuna na Waziri Kiongozi mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Pia wamo mawaziri Haroun Ali Suleiman, Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohammed Aboud, Mohammed Yussuf Mshamba, Balozi Ali Abeid Karume, Hamad Bakari Mshindo, Mohammed Raza na Omar Sheha Mussa.
Miongoni mwao, Dk. Shein, Nahodha na Dk. Bilal wanapewa nafasi kubwa ya kuteuliwa na CCM leo kusimama dhidi ya Maalim Seif Sharrif Hamad wa CUF katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 31 mwaka huu.
Dk. Shein anaelezwa kuwa mwanasiasa mwenye kufuata siasa za ustaarabu, muungwana na anayetenda kazi zake bila kuwa na makundi na anatazamiwa kuwa kiungo kikubwa kati ya Pemba na Unguja, hasa baada ya maridhiano ya kisiasa visiwani.
Hata hivyo, tangu ajitose kuwania uteuzi huo, amekuwa akiandamwa na ‘makombora’ kutoka kwa baadhi ya wapinzani wake, waliofikia hatua ya kumwaga vipeperushi Unguja wakimtuhumu kwa mambo kadhaa.
Hata jana jioni, uvumi ulikuwa unaenezwa mjini hapa kuwa Dk. Shein alikuwa ameandika barua ya kujitoa na kuelekeza nguvu zake kumsaidia Nahodha.
Lakini wanaomtetea wanaamini hali hiyo imefanyika kwa sababu mgombea huyo ni tishio miongoni mwa wenzake na ana nafasi kubwa ya kuibuka mshindi leo.
Baadhi ya wasaidizi wa Dk. Shein walithibitisha kuenezwa kwa uvumi wa kujitoa tangu juzi, lakini akaeleza kuwa habari hizo hazikuwa na ukweli wowote.
Mwingine ni Nahodha ambaye kwa umri wake wa miaka 48, anaonekana kuwa chaguo la vijana, kama ambavyo mwenyewe amesema anataka kuleta mabadiliko Zanzibar na kuifanya kuwa kama Dubai.
Huyu naye anaonekana kuwa miongoni mwa wagombea wenye nguvu katika kumrithi Rais Karume na kwa turufu yake ya ujana, na pengine kuwa kwake karibu kama msaidizi wa Rais, ni karata yake nyingine.
Dk. Bilal ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi chini ya Dk. Salmin Amour Juma ‘Komandoo,’ ni mgombea mwingine mwenye nguvu miongoni mwa waliojitokeza.
Alijaribu bila mafanikio kutaka kumrithi Komandoo na akabwagwa na Karume na akajaribu tena mwaka 2005 bila mafanikio, lakini tangu wakati huo, ndoto za kutaka kuwa rais wa Zanzibar hazijafutika kwake.
Alitajwa kuwa mtu wa karibu wa Dk. Salmin, lakini yamekuwapo madai mapya hapa na Zanzibar, kuwa wawili hao sasa hawako pamoja katika mbio za mwaka huu za kuingia Ikulu.
Dk. Salmin alitua hapa juzi akifuatana na Nahodha na haijawekwa bayana kama turufu yake ni kwa mwanasiasa huyo kijana, lakini uwepo wake katika vikao hivi viwili vya leo, ni ishara kuwa amekuja na siri moyoni.
Wagombea wengine wanane waliosalia katika kinyang’anyiro hicho, hawapewi nafasi kubwa ya kuteuliwa, kwa sababu mbalimbali, ingawa katika siasa, lolote linaweza kutokea.
Chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, vikao hivyo vinatarajiwa hadi kufikia majira ya jioni leo, vitakuwa vimetoa jina la mgombea na la mgombea mwenza wa Jamhuri ya Muungano.
Rais Kikwete ndiye mgombea pekee wa CCM katika urais wa Muungano na kwa mujibu wa Katiba ya Chama hicho, atapigiwa kura katika Mkutano Mkuu utakaofanyika kwa siku mbili kuanzia kesho.
Katika suala la mgombea mwenza, bado ni siri kubwa kwa Rais Kikwete mwenyewe, ingawa yamekuwapo majina kadhaa yanayotajwa kwa nafasi hiyo.
Majina ya wanasiasa kama Zakia Meghji, Dk. Salim Ahmed Salim, Muhammed Seif Khatib na hata Dk. Shein na Nahodha, yamehusishwa na nafasi hiyo, ingawa ukweli wa mambo utakuwa hadharani majira yoyote leo.
Katika maandalizi ya vikao hivyo, Rais Kikwete jana alitembelea Kizota ambako Mkutano Mkuu utafanyika kesho na keshokutwa, na maandalizi yalikuwa yanaelekea hatua za mwisho kukamilika.
Rais Kikwete alitembelea eneo hilo muda mfupi baada ya kutua mjini hapa na alikuwa Kizota na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Katibu Mkuu wa CCM Yusuf Makamba na watendaji wengine wa CCM na Serikali.
No comments:
Post a Comment