WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliposema atahakikisha watu waliojenga kwenye maeneo ya wazi na yasiyoruhusiwa wavunje wenyewe majengo yaliyopo, hakuwa anatania na wale waliokuwa wakimvimbishia kichwa, watakuwa wamekosea.
Hali hiyo ilidhihirika jana jioni wakati tingatinga la Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam, lilipofanya kazi ya kuvunja maeneo ambayo yameanza kujengwa majengo kinyume cha utaratibu na ambayo inaaminika kuwa ni ya wazi au hayaruhusiwi majengo hayo.
Jana majengo mawili katika Jiji la Dar es Salaam, kiwanja kilichopo karibu na Hoteli ya Palm Beach, ambacho ndio kwanza kilikuwa kimepandishwa ukuta pamoja na ukuta mwingine uliojengwa jirani na Hospitali ya Aga Khan katika Barabara ya Ocean Road, vilivunjwa jana jioni na askari wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Licha ya mmiliki wa kiwanja cha jirani na Hoteli ya Palm Beach, Taher Muccadam kutoa notisi ya siku saba kwa Waziri Profesa Tibaijuka amuombe radhi na kumlipa fidia ya Sh bilioni mbili kwa madai kwamba alimvunjia heshima kwa jamii vinginevyo atamfikisha mahakamani, agizo hilo limepuuzwa.
Badala yake, umma wa wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa wakirejea majumbani mwao jana jioni, walishuhudia tingatinga la Manispaa ya Ilala, lenye namba SM 3937, chini ya ulinzi mkali, likifanya kazi ya kuangusha ukuta huo saa moja jioni kabla ya kuhamia ukuta wa jirani na Aga Khan nusu saa baadaye.
Kazi hizo mbili zilifanywa na tingatinga hilo chini ya ulinzi wa askari zaidi ya 50 waliokuwa katika magari mengine manne, Isuzu; Toyota Land Cruiser Hard Top, Toyota Double Cabin na Toyota Nissan Patrol yenye namba za usajili SM 3096, SM 4360 na STJ 5662, mali ya Manispaa ya Ilala.
Mara baada ya kazi hiyo kukamilika katika eneo la Palm Beach, wananchi waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, baadhi yao walisikika wakisema, “huyu ndiye Waziri, siyo viongozi wababaishaji. Watu wanamtisha eti wana vibali kutoka Ikulu, yeye aliwambia hatishiki na vibali vyao.”
Mwingine alisema, “huyu mama (Profesa Tibaijuka) hana mchezo, kama fedha anazo za kutosha, hasumbuliwi na vijisenti…tunahitaji viongozi wenye kusimamia sheria nchini mwetu.”
Mmoja wa viongozi waliosimamia kazi hiyo, hakutaja kutaja jina lake wala kueleza hatua hiyo imefikiwa na nani, akisema, “hatupo hapa kuongea na vyombo vya habari. Kazi mnaiona.”
Kiwanja hicho cha Palm Beach ambacho ni namba 1006 ni kati ya viwanja ambavyo Profesa Tibaijuka alidai kuwa ni cha wazi na kwamba hakiruhusiwi kuwa makazi.
Hivi karibuni, Profesa Tibaijuka akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam aliwataka wananchi waliopora viwanja na maeneo ya wazi nchini na kujenga, wajisalimishe kwa mazungumzo, kwa sababu huenda wakaokoa hata matofali kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.
No comments:
Post a Comment