KUTOKANA na utafiti wa kisayansi kuonesha kuwa kutofanya tohara kwa wanaume ni moja ya sababu zinazochangia maambukizi ya Ukimwi, wanaume katika mikoa saba nchini wanatarajiwa kufanyiwa tohara kuanzia mwakani kwa sababu inayo idadi kubwa ya wanaume wasiotahiriwa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema itaanza operesheni maalumu kwa kushirikiana na wadau wengine yakiwemo mashirika ya misaada kutoka Marekani, kufanya tohara kwa wanaume hao katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Kagera, Tabora, Shinyanga na Wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Hayo yalibainishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Haji Mponda, jana mjini hapa, katika hotuba yake kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kumkaribisha Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Kitaifa mjini hapa.
Dk. Mponda alisema utafiti uliofanyika na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi, imeonesha kuwa mikoa hiyo inaongoza kwa maambukizi na moja ya sababu ni kuwepo kwa idadi mkubwa ya wanaume wasiofanyiwa tohara.
“Mpango wa Wizara ni kutaka kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU na utafiti umeonesha mikoa hii ina idadi ndogo ya wanaume waliofanyiwa tohara, lakini ina viwango vya juu vya maambukizi,” alisema Waziri huyo.
Hivyo alisema mpango wa Wizara ambao tayari ulianza kwa majaribio katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Kagera, itaendelezwa zaidi katika mikoa iliyoainishwa kuanzia mwakani kwa ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia mashirika yao ya misaada sambamba na marafiki wengine wa maendeleo.
Alisema mpango huo wa kuwafanyia tohara wanaume katika mikoa hiyo umelenga kuwafikia wanaume zaidi ya milioni 2.5 na wanaume wa mikoa hiyo wameonesha kufurahishwa na uamuzi huo wa kuwatahiri.
Katika takwimu zilizotolewa na TACAIDS ya viwango vya maambukizi ya VVU ya mwaka 2003/ 2004, Mkoa wa Iringa ulikuwa na maambukizi ya asilimia 13.4 ambapo kwa mwaka 2007/2008 maambukizi ni asilimia 15.7.
Mkoa wa Mara kwa miaka hiyo, maambukizi yalikuwa ni asilimia 3.5 na kuongezeka mwaka 2007/2008 hadi kufikia asilimia 7.7 wakati Mkoa wa Shinyanga maambukizi yalikuwa ni asilimia 6.5 ambapo kwa mwaka 2007/2008 viwango vya maambukizi ni asilimia 7.4.
Naye Mwandishi Wetu, Flora Mwakasala anaripoti kuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Chiku Galawa ametaka mabango yote ya waganga wa jadi yanayotangaza kuwepo kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume, yaondolewe kwa kuwa ni kichocheo cha ongezeko la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi yaliyofanyika jana kimkoa katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Galawa alisema mabango hayo yamebandikwa mitaani kwa wingi.
“Huu ni utapeli mkubwa, nani kasema watu wanahitaji kuongezewa nguvu za kiume? Jambo hili ni sawa na kuwahamasisha watu waendelee kufanya uasherati na kuongeza maambukizi mapya ya VVU,” alisema.
Alisema kitendo cha watu kuongeza nguvu za kiume kinawashawishi kuendelea kufanya ngono, jambo linalosababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la maambukizi hasa kwa vijana ambao ni taifa la kesho.
“Tutashirikiana na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha mabango yote yaliyobandikwa mitaani na barabarani yanaondolewa,” alisema.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa Mafunzo Taifa wa Chama cha Waganga wa Tiba za Asili, Sadick Kalimaunga alisema kauli hiyo ya Galawa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, si sahihi kwa kuwa kazi yao ni kuwasaidia wanaume wenye matatizo ya upungufu wa nguvu za kiume.
“Sisi hatuchochei maambukizi ya VVU kama wanavyodai bali tunawasaidia wanaume wenye matatizo hayo kudumisha ndoa zao kwa kuwaongezea nguvu za kiume ili waweze kufanya tendo hilo kikamilifu,” alisema.
Aidha, alisema kitendo cha Serikali kuondoa mabango hayo kitasababisha baadhi ya watu wanaohitaji tiba hizo ambazo zilikuwepo tangu enzi kukosa huduma na wengine ndoa zao kuvunjika.
Kwa mujibu wa takwimu, Dar es Salaam ni mkoa unaoshika nafasi ya pili nchini kwa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU cha asilimia 9.3. Iringa inaongozwa kwa kuwa na asilimia 15.7.
No comments:
Post a Comment