CHAMA Cha Kijamii (CCK), kinaandaa waraka utakaochambua mapungufu ya Katiba ya sasa ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
CCK watauwasilisha waraka huo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, ili kutoa hoja yao rasmi ya kwa nini Tanzania inahitaji kuwa na Katiba mpya.
Aidha, kimesema kinakusudia kushiriki katika kufungua au kuwa marafiki wa mahakama katika kesi za kikatiba zinazohusiana na masuala ya uchaguzi mkuu kwa madai kuwa si mambo yote yanaweza kumalizika au kubadilishwa kisiasa.
Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda, aliyasema hayo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana ambapo pamoja na mambo mengine, alisema wanaendelea kufuatilia usajili wa kudumu.
Akitanda alisema karibu asilimia kubwa ya matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu yalitokana na kiashirio cha kutokuwepo kwa Katiba mpya yenye kutengeneza mazingira mazuri ya uhusiano kati ya watawala na watawaliwa, na yote yanaweza kusahihishwa vizuri endapo Katiba itaandikwa upya.
“Kama tulivyosema hapo awali kuwa kuna haja ya Katiba mpya, na kwa kuzingatia kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani kuwa hadi hivi sasa hakuna chama chochote kilichotoa madai rasmi ya hoja kuhusu Katiba mpya, sisi kama CCK tukizingatia nafasi iliyopo mbele yetu, tunaandaa waraka utakaochambua mapungufu hayo,” alifafanua Akitanda.
Kuhusu kushirikiana na mahakama katika kesi za kikatiba, alisema wameamua kufanya hivyo wakiamini kuwa mambo mengine katika suala hilo yanahitaji nguvu ya chombo hicho na watachukua njia hiyo wakati wowote wanapoiona njia hiyo ni bora.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Renatus Muabhi, alisema wapo mbioni kufanikisha azma ya kupata usajili wa kudumu ili hatimaye na chenyewe kitoe mchango wake wa kifikra na kiuongozi nchini.
No comments:
Post a Comment