KAMPUNI kubwa ya ulinzi ya Ulaya, BAE Systems, imekubali kuilipa Serikali ya Tanzania fidia ya Sh bilioni 67.29 (pauni milioni 30) kama walivyokubaliana na Taasisi ya Kuchunguza Makosa makubwa ya jinai ya Uingereza, SFO, ikiwa ni sehemu ya kumaliza shauri lililokuwa linawakabili mahakamani.
Kauli hiyo imetolewa baada ya kampuni hiyo kuhukumiwa kulipa faini ya pauni 500,000 au dola za Marekani 775,000, sawa na Sh bilioni 1.12 baada ya kukiri kosa la ‘kushindwa kuweka kwa usahihi kumbukumbu za manunuzi.’
Viwango vya ubadilishaji kwa siku ya jana kwa mujibu wa Benki Kuu ni pauni moja sawa na Sh 2,243 wakati dola moja ni Sh 1,442.
Kampuni hiyo imesema kwamba kwa sasa inaangalia utaratibu wa malipo hayo ikiwa ni sehemu ya fedha zilizolipwa na Serikali ya Tanzania kununua rada hiyo ya kisasa.
Mpango huo ulikuwa na thamani ya dola milioni 40 sawa na pauni milioni 28. Mahakama ilitoa hukumu hiyo kwa kuzingatia shauri la kutoweka taarifa vyema.
Suala la kutoa mlungula ambalo awali lilitawala uchunguzi wa SFO halikufikishwa mahakamani.
Jaji David Bean alisema itakuwa ni kuukataa ukweli kufikiri kuwa wakala wa BAE nchini Tanzania, Shailesh Vithlani, alilipwa mamilioni ya dola eti kwa sababu tu anajua kuunganisha vyema masuala ya biashara.
BAE ilikubali kwamba inawezekana kwamba sehemu ya dola milioni 12.4 (waliyomlipa Vithlani) ilitumika kwa ajili kuisaidia kupata zabuni hiyo.
Hata hivyo waendesha mashtaka wamesema kwamba ni vigumu sana kuweza kujua Vithlani alifanya nini na fedha hizo na wala kuthibitisha kwamba sehemu ya fedha hizo zilitumika vibaya.
Kwa mujibu wa maelezo fedha hizo zililipwa kwa kampuni za Vithlani za British Virgin Islands na Kampuni ya Merlin iliyosajiliwa Tanzania.
Kampuni ya BAE imesema kwamba imefurahishwa na shauri hilo kumalizwa na kwamba inaandaa utaratibu wa kuilipa Tanzania fedha zake.
Hukumu hiyo iliyotolewa jana na Jaji David Bean mjini London inahitimisha miezi sita ya uchunguzi wa kina wa shauri hilo.
BAE ilikiri kosa hilo la kushindwa kutunza vyema kumbukumbu za manunuzi mwezi uliopita katika mpango wake na Taasisi ya Kuchunguza Makosa makubwa ya jinai ya Uingereza, SFO.
Kampuni hiyo iliridhia Februari kulipa pauni milioni 30 kama sehemu ya fidia na waendesha mashitaka walisema wangekubaliana na BAE ikiwa wangelipa faini hiyo na kutuma ‘chenji’ kwa Serikali ya Tanzania.
Kampuni hiyo ilikuwa katika uchunguzi nchini Uingereza kuanzia Novemba, 2004 kwa tuhuma za kutoa rushwa ili kushinda zabuni za manunuzi katika nchi sita ikiwamo Tanzania na Jamhuri ya Czech.
Februari mwaka huu BAE ilikubali kulipa karibu dola za Marekani milioni 450 kama fidia ili kumaliza shauri hilo baina yake na SFO na waendesha mashitaka wa Marekani.
Hata hivyo, BAE ililipa dola za Marekani milioni 400 kwa Marekani na kukiri kosa la kutoweka taarifa sahihi ya manunuzi hayo. Kampuni hiyo ilikanusha kutoa rushwa.
“Jukumu langu ni kufikisha kesi mahakamani na kuhakikisha kuwa Jaji anatoa adhabu stahili,” alisema Mkurugenzi wa SFO, Richard Aderman baada ya hukumu.
Alisema ana uhakika kuwa BAE itatekeleza makubaliano yaliyofikiwa ya kuilipa Serikali ya Tanzania ‘chenji’ ya pauni milioni 30 (zaidi ya Sh bilioni 60), baada ya kulipa faini nchini Uingereza.
Wakili aliyekuwa akiitetea BAE, Arno Chakrabarti, alikataa kusema chochote baada ya hukumu hiyo.
Shauri hilo la rada lililoelezwa kufanywa na mfanyabiashara Shailesh Vithlani ambaye alihusika katika mpango huo kuinufaisha BAE, pia limemhusisha aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wahusika wa kashfa hiyo.
No comments:
Post a Comment