Monday, December 13, 2010

Chadema wamtambua Kikwete

JAKAYA Kikwete aliwaambia viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwamba hawana mwingine wa kumlilia kwa masuala yao, isipokuwa yeye; na kwamba watakwenda na kurudi kwake kwa sababu yeye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Novemba 18, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma wakati akihutubia Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 10,na sasa aliyoyasema yametimia.

Baadhi ya wabunge wa Chadema walitoka katika ukumbi wa Bunge wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe walitoka nje mara tu Rais Kikwete alipoanza hotuba yake, sasa wamekubali yaishe. Wanamtambua ndiye Rais halali wa Tanzania.

Lakini katika kauli iliyowalenga moja kwa moja wabunge wa Chadema wakati akimalizia hotuba yake bungeni, Rais Kikwete alisema wabunge hao hawana wa kumlilia zaidi yake, kwani yeye ndiye Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Watakwenda watarudi, hawana mwingine wa kumlilia kwa yao, isipokuwa Serikali ya CCM ambayo mimi ndiye Rais wake; Dk. Mohammed Gharib Bilal ndiye Makamu wake. Serikali ambayo Dk. Ali Mohammed Shein ndiye Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais na Balozi Seif Ali Idd ni Makamu wa Pili wa Rais,” alisema Rais Kikwete, Novemba 18, mwaka huu na kushangiliwa na wabunge.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho katika siku za karibuni, kilitangaza kutomtambua Rais Jakaya Kikwete, kimebadili msimamo.

Kimekubaliana kwamba Kikwete ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kinatarajiwa siku yoyote kuanzia leo kutangaza maazimio ya Kamati Kuu iliyokutana mwishoni mwa wiki Dar es Salaam, ambayo moja ya maazimio yake, ni kumtambua kiongozi huyo wa nchi.

Kamati Kuu ya Chadema pia imeamua kusitisha uamuzi wa wabunge wa chama hicho kwa kumvua nafasi ya Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, mbunge mwenzao, Kabwe Zitto wa Kigoma Kaskazini.

Baada ya Rais Kikwete kutangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, Chadema ilikataa kumtambua, ikidai alichaguliwa kutokana na uchaguzi uliokuwa na udanganyifu.

Novemba 18, mwaka huu, wakati akianza hotuba ya kulihutubia Bunge jipya mjini Dodoma, baadhi ya wabunge wa Chadema waliokuwa ndani ya ukumbi wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, walitoka nje ya ukumbi huo.

Lakini sasa, vyanzo vya habari kutoka ndani ya Kamati Kuu ya Chadema, vimeliarifu gazeti hili kuwa wamekubaliana kumtambua Rais Kikwete baada ya mjadala mzito na baada ya kupima athari za kutomtambua Rais Kikwete aliyeshinda kwa zaidi ya asilimia 60.

Kuhusu suala la Zitto, chanzo hicho cha habari, kilieleza kuwa wajumbe wakongwe wa Kamati Kuu walimtetea na kueleza kuwa mbunge huyo machachari hakupewa nafasi ya kujitetea.

Wabunge wa Chadema walikutana Bagamoyo wiki iliyopita na kupiga kura ya kutokuwa na imani na Zitto, wakimtuhumu kwa kwenda kinyume cha msimamo wa chama hicho wa kumsusa Rais Kikwete bungeni.

Zitto hakupatikana kuzungumzia hatua hiyo mpya ya chama chake jana, kwa sababu simu yake iliita bila kupokewa, ikiwa ni siku moja baada ya kutoka Hospitali ya Aga Khan ambako alikuwa amelazwa tangu Alhamisi iliyopita, kwa kusumbuliwa na maumivu ya tumbo, ikidaiwa alikula chakula chenye sumu.

Kutokana na kuchafuka kwa hali ya hewa ndani ya chama hicho, Kamati Kuu iliamua pia kuunda kamati maalumu ya watu wanne ikiongozwa na Profesa Mwesiga Baregu, kwa nia ya kurejesha amani kundini.

Kamati hiyo kwa maudhui, inafanana na ile iliyoundwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juni mwaka huu, ikiongozwa na Rais mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi kupatanisha makundi hasimu yaliyokuwa yameibuka ndani ya wabunge wake.

Alipoulizwa kuhusu kamati hiyo, Profesa Baregu alithibitisha na kueleza kuwa Kamati yake imepewa jukumu la kuhakikisha amani inarejea katika chama hicho.

“Ndiyo, kuna kamati maalumu inayowahusisha wajumbe wakongwe wa Kamati Kuu iliyoundwa kwa ajili ya kuhakikisha umoja na amani zinarejea katika chama,” alisema Profesa Baregu.

Alisema kurejeshwa kwa umoja na amani katika chama hicho, pia kutahakikisha umma haupotei imani yao kwa chama hicho cha upinzani.

“Tutazungumza na wanachama ambao wana malalamiko au wana matatizo, ili kumaliza tofauti zao na kurejesha tena mshikamano, amani na upendo katika chama…hatutaki kupoteza imani ya umma kwetu,” alieleza Profesa Baregu.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Shida Salim ambaye ni mama mzazi wa Zitto, Kitila Mkumbo ambaye ndiye Katibu na mjumbe mwingine aliyetajwa kwa jina la Shilungushela.

Katibu Mkuu wa Chadema, alikataa kuzungumzia maazimio hayo jana alipotafutwa kwa simu, lakini akaeleza kuwa watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho.

No comments: