WAZIRI wa zamani katika Serikali ya Tanzania, Joseph Mungai jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa mjini Iringa , kujibu mashitaka ya kutoa rushwa wakati wa kinyang’anyiro cha kura ya maoni katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mungai anakabiliwa na mashitaka 15 ya utoaji rushwa kwa wapiga kura wa CCM wa kata ya Ihalimba katika jimbo la Mufindi Kaskazini.
Imedaiwa kuwa mwanasiasa huyo alitoa rushwa wakati akitafuta ridhaa ya wapiga kura wa CCM wa jimbo la Mufindi Kaskazini ili wamchague kwa mara nyingine kugombea ubunge wa jimbo hilo ambalo ameliongoza kwa miaka mingi.
Katika kura hizo za maoni, Mungai alishika nafasi ya pili kwa Kupata kura 3,430 dhidi ya kura 6,386 zilizompa ushindi Mahamud Mgimwa katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na wagombea sita.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inamuunganisha pia Moses Masasi aliyetajwa kwamba ni Mhasibu na Fidel Cholela ambaye ni Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM kata ya Mafinga.
Mungai alikana mashitaka na kurudishwa rumande na watuhumiwa hao wengine kusubiri taratibu za dhama ambapo walihitajika wadhamini wawili kwa kila mmoja.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Mary Senapee, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Prisca Mpeka, alidai kuwa Mungai na wenzake walitoa rushwa kwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kata ya Ihalimba waliokuwa na kikao Julai 8, mwaka huu kwenye ofisi ya CCM ya kata ya Ihalimba, ili wampigie kura ya maoni.
Alidai kwamba Mungai na watuhumiwa hao wanadaiwa kutoa Sh 10,000 kwa Obadia Mtokoma ambaye ni Mwenyekiti wa CCM wa tawi la kijiji cha Vikula na Katibu wa Uchumi na Fedha wa tawi la CCM la kijiji cha Vikula, Konjeta Kiyeyeu ambaye pia alihongwa Sh 10,000.
Wengine kwa mujibu wa Mpeka na kiasi cha fedha walichopewa kwenye mabano, ni pamoja na Katibu wa CCM wa Kata ya Ihalimba, Aldo Lugusi (Sh 10,000), Mwenyekiti wa CCM wa Ihalimba, Ezekiel Mhewa (Sh 10,000) na Katibu wa Fedha na Uchumi wa CCM Ihalimba, Tulaigwa Kisinda (Sh 10,000).
Wengine ni Jiston Mhagama (Sh 10,000), Maria Kihongozi (Sh 20,000), Lurent Mdaligwa (Sh 5,000), Victory Kalinga (Sh 20,000), Francis Chonya (Sh 2,000) na Alfred Kisinga (Sh 2,000).
Waliohongwa wengine kwa mujibu wa mashitaka, ni Issac Tewele (Sh 2,000), Sosten Kigahe (Sh 10,000), Raphael Lutomo (Sh 10,000) na Andrew Mkiwa (Sh 20,000). Wanakabiliwa na jumla ya mashitaka 15 ya rushwa.
Pamoja na kukana mashitaka hayo, watuhumiwa hao walishindwa kukamilisha kipengele cha dhamana mara moja, na hadi tunakwenda mitamboni walikuwa bado rumande wakisubiri kukamilisha kipengele hicho.
Akitoa masharti ya dhamana kwa watuhumiwa hao, Senapee alisema kila mtuhumiwa anatakiwa kuwa na wadhamini wawili, na kila mmoja akiwa na Sh milioni tano na mmoja wao lazima awe mkazi wa hapa.
Mpeka alisema pia kuwa mwana CCM mwingine Fredrick Mwakalebela, ambaye naye anatuhumiwa kujihusisha na rushwa wakati wa kampeni hizo Iringa Mjini, atafikishwa mahakamani Agosti 17 mwaka huu, baada ya kushindwa kutokea jana kwa kilichoelezwa kwamba ana udhuru.
Wakati huo huo, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Iringa, Donasian Kessy aliwaambia waandishi wa habari kwamba katika kesi inayomkabili Mungai wana CCM wanaotuhumiwa kupokea rushwa hizo, watafikishwa mahakamani hapo kama mashahidi kwa sababu ndio walioisadia Takukuru kupata taarifa hiyo.
Kessy alisema pamoja na washitakiwa hao kufikishwa mahakamani alisema suala la kuwaengua kushiriki uchaguzi ni la Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye kabla ya kufanya hivyo ni lazima ajiridhishe na tuhuma.
Alisema pamoja na kwamba Takukuru inatambua kuwa katika kesi hizo kuna kushinda au kushindwa, endapo watashindwa hilo halitakuwa kosa la chombo hicho cha Dola.
No comments:
Post a Comment