HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), imezingatia maoni ya wanachama wake kwa kuwateua wagombea wa ubunge walioongoza kura za maoni.
Hata hivyo katika baadhi ya majimbo wameachwa walioongoza kwa sababu mbalimbali zikiwemo tuhuma za rushwa na ukosefu wa maadili.
Akitangaza majina ya wagombea hao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, John Chiligati alisema sehemu chache chama hicho kiliamua kuteua wagombea ambao hawakushinda kura za maoni.
Uamuzi huo wa kufuata kura za maoni, umekilazimu chama hicho kuwaacha baadhi ya mawaziri wake akiwemo Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala aliyekuwa akitetea kiti chake cha Nkenge na Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga (Ubungo).
Wengine ni Naibu Waziri Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza (Mkinga); Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera (Korogwe Mjini) na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. James Wanyancha (Serengeti).
Mbali na mawaziri hao, chama hicho kimejikuta kikilazimika kuwaacha wakongwe wake wa siasa akiwemo Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela.
Hata hivyo, imewaengua pia washindi wa kura za maoni wakiwemo Thomas Nyimbo (Njombe Magharibi); Athuman Ramole (Moshi Mjini); Hussein Bashe (Nzega) na Frederick Mwakalebela aliyeongoza kwa Jimbo la Iringa Mjini, kwa sababu za kuonekana kukosa maadili.
Chiligati alisema jana alfajiri mjini hapa kuwa suala la Mwakalebela aliyeongoza Jimbo la Iringa Mjini, halifanani na washindi wengine wa kura za maoni walioteuliwa wakiwemo Basil Mramba (Rombo) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), licha ya kuwa na kesi mahakamani kama yeye.
“Suala kwa Mwakalebela ni maadili tu, katika mchakato huu, kakamatwa kwa tuhuma za rushwa na Takukuru wamesema wanayo sababu ya kumpeleka mahakamani.
“Lakini alikuwa ndiyo kwanza kaingia katika mchezo wenyewe na katika mchezo huu huu kabla ya dakika tisini, akapigiwa filimbi kuwa amecheza faulo,” alisema Chiligati.
Kuhusu tofauti ya Mramba, Chenge na Mwakalebela, Chiligati alisema, “kisheria wote ni watuhumiwa na hawakukutwa na
hatia, lakini kimaadili ni tofauti…Mramba anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka, tuliita wanasheria wakasema hiyo kesi haimuondolei sifa ya kuwa mgombea.”
Hata hivyo, alikiri Mramba alipitishwa baada ya kufanyika mjadala kati ya wajumbe hao wa NEC. “Katika Mkoa wa Shinyanga, Jimbo la Bariadi Magharibi aliteuliwa Chenge kutetea nafasi yake, anayo kesi ya trafiki, haimkoseshi haki ya kuwa mgombea,” alisema Chiligati.
NEC pia imelazimika kuwapoka washindi wengine wa kura za maoni ‘haki’ ya kuwa wagombea kutokana na mmoja kuonekana kuwa hauziki licha ya kushinda kura za maoni, na mwingine kupokwa kwa kuwa alikuwa katika mapumziko baada ya kutumikia adhabu ya chama hicho.
Mgombea aliyeshinda kura za maoni katika Jimbo la Moshi Mjini na kuonekana kuwa hana sifa, ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiusa, Athuman Ramole aliyepata kura 1,554 na kufuatiwa na Mwenyekiti wa Wazazi Kilimanjaro, Thomas Ngawaiya (1,539) na Justine Salakana (1,152).
Katika jimbo hilo, NEC imemteua Salakana aliyeshindwa kura za maoni, lakini kwa kigezo kuwa amewahi kuwa Mbunge wa Rombo kwa tiketi ya Chadema, sifa ambayo mshindi wa kwanza hana, lakini wa pili anayo, ila tofauti yake amewahi kuwa Mbunge wa Vunjo kwa tiketi ya TLP.
Sifa nyingine aliyonayo Salakana ambayo wenzake hawana, ni kuwahi kuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Utalii Kilimanjaro.
Ingawa Chiligati hakufafanua kwa nini sifa hizo, ziwe muhimu kuliko kura za maoni, lakini duru za kisiasa zilieleza kuwa wamezingatia historia ya jimbo hilo kuwa mikononi mwa upinzani tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.
Mbunge wake ni Philemon Ndesamburo wa Chadema. Pili ni nguvu za Mbunge anayemaliza muda wake, Ndesamburo ambaye ni wa Chadema anakotoka Salakana na mfanyabiashara wa utalii anayeongozwa na mteule huyo wa CCM.
Katika Jimbo la Njombe Magharibi, mshindi wa kura za maoni Nyimbo amepokwa nafasi ya uteuzi kwa kuwa aliwahi kufungiwa mwaka mmoja asigombee chochote katika chama hicho. Chiligati alisema pamoja na kuwa muda wa adhabu hiyo umekwisha na kuwa ameshinda kura za maoni, wameona wamuangalie kwanza mwenendo wake na hivyo ameteuliwa Gerson Hosea.
Kwa upande wa Viti Maalumu, NEC imewabeba wagombea wote walioongoza kwa kushika nafasi ya kwanza ambao baadhi ya sura mpya ni Vicky Kamata (Geita); Namalok Sokoine (Arusha); Betty Machangu (Kilimanjaro) na Ummy Mwalimu (Tanga).
Pia kwa upande wa Walemavu, wameteuliwa wabunge wawili wa zamani, Al-Shaymaa Kwegir na Margaret Mkanga, wakati kwa upande wa mashirika yasiyo ya kiserikali ni wabunge wawili wa zamani, Rita Mlaki wa Kawe na Anna Abdallah wa Viti Maalumu.
Katika Viti Maalumu, walioshika nafasi ya pili wamo wabunge wengi wa zamani akiwemo Margaret Sitta; Dk. Christine Ishengoma; Devotha Likokola; Rosemary Kirigini na Dk. Maua Abeid Daftari.
Aidha, kutoka katika kapu, nafasi 18 wapo baadhi ya wabunge wa zamani walioanguka katika kura mikoani kama Janeth Masaburi; Aziza Sleyum Ally; Esther Nyawazwa na Florence Kyendesya; na wanawake maarufu kama Asha Baraka; Sifa Swai na Rukia Masasi.
No comments:
Post a Comment