Wednesday, August 25, 2010

Tendwa aongeza siku za kujaza gharama za uchaguzi


Msajili wa vyama vya siasa- John Tendwa

Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ameongeza muda wa siku kumi kwa wagombea kuwasilisha fomu za gharama za uchaguzi watakazotumia wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kwamba watakaoshindwa kufanya hivyo ndani ya muda huo wa ziada, atawafuta kwenye kinyang’anyiro hicho.

Muda wa kurejesha fomu za tamko la gharama za uchaguzi zitakazotumika unaishia kesho, lakini Tendwa ameuongeza hadi Septemba 6 baada ya baadhi ya vyama vya siasa kulalamika kuwa wagombea wake hawajapewa fomu hizo na wakurugenzi wa halmashauri, ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi huo.

Msajili huyo alithibitisha kuwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi wamekuwa wakiwakatalia kuwapa fomu hizo wagombea wa ubunge na udiwani wa vyama vya siasa wanapokwenda kuziomba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema wakurugenzi hao hawana sababu yoyote ya kuwanyima wagombea fomu hizo kwani tayari zilishapelekwa kwa wingi katika kila ofisi ya halmashauri kwa ajili ya kuzigawa.

Alisema hata vyama vya siasa havipaswi kulalamika kwani navyo vilishapatiwa fomu hizo muda mrefu hivyo viliwajibika kuwa vimeshawapatia wagombea wao wajaze na kuzirejesha katika ofisi ya msajili kwa wakati.

“Sitaongeza muda tena na mgombea yeyote atakayeshindwa kuwasilisha fomu inayoelezea gharama atakazotumia katika kampeni ajue nitamwondoa na hatagombea maana sheria inanipa mamlaka ya kufanya hivyo, nimeamua kuongeza muda baada ya kuridhika kuwa baadhi ya sehemu fomu zilikuwa hazijafika,” alisema Tendwa.

Alisema hata wagombea ambao wamepita bila kupingwa wanapaswa kujaza fomu hizo na kuziwasilisha kwa ofisi ya msajili kama sheria inavyosema.

“Hata Waziri Mkuu nimemwambia leo (jana) kuwa kupita bila kupingwa si sababu ya kutojaza fomu ya gharama za uchaguzi atakazotumia, nimemwambia kuwa Sheria inamtaka ajaze na aiwasilishe kwangu, na wabunge wengine ambao hawakupingwa nimewaeleza hivyo hivyo,” alisema Tendwa.

Alisema siku kumi alizoongeza sio nyingi hivyo vyama vya siasa vinapaswa kufanya haraka kuwapa wagombea wao fomu hizo wazijaze na kisha kuzirejesha ili wasipoteze sifa za kugombea.

Alisema wagombea wanaweza kutumia zaidi ya gharama walizojaza katika fomu, lakini baadaye watawajibika kuelezea matumizi ya nyongeza yalivyofanyika.

“Kuna vitu vingi ambavyo vinaweza kutokea bila kutarajia kama mfumuko wa bei, watu wakakuta njia mbovu wakakwama wakatumia fedha zaidi, kinachotakiwa ni kuelezea matumizi yaliyozidi basi, lakini mgombea hakatazwi kutumia zaidi ya alichoandika kwenye fomu,” alisema.

Kuhusu malalamiko ya Chadema kuwa wagombea wake wamenyimwa fomu za kujaza gharama hizo, Tendwa alisema ofisi yake ilishatoa fomu hizo kwa chama hicho siku nyingi hivyo anashangaa malalamiko yanatoka wapi.

Alisema wajibu wa kuwapa wagombea fomu za kujaza ni la vyama vya siasa kwa kuwa vyenyewe ndivyo vinawania madaraka na si ofisi yake.

Katika fomu hizo, wagombea wanatakiwa wajaze matarajio ya mapato yao na gharama wanazotarajia kuzitumia wakati wa kampeni.

Sheria inawataka wagombea hao kujaza fomu hizo ndani ya siku saba baada ya kuthibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kugombea.

No comments: