KAMA ilivyokuwa Zanzibar, Chama cha Sauti ya Umma (SAU) jana kilikwaa kisiki katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Dar es Salaam fomu zake za urais zilipokataliwa kwa kushindwa kutimiza masharti.
Chama hicho na Democratic Party (DP) vilikumbana na kadhia hiyo baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kupata wadhamini katikam mikoa 10 nchini.
Hivi karibuni, SAU ilitimuliwa katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) baada ya wagombea wake wawili kwenda ofisini hapo kuchukua fomu za kuomba kuidhinishwa kugombea urais.
NEC jana ilipitisha wagombea urais kutoka vyama saba vya siasa kuwania nafasi hiyo kati ya vyama 12 vilivyoomba.
Urejeshaji wa fomu za uteuzi wa kugombea nafasi hiyo ya ukuu wa nchi ulifanyika jana kwa siku nzima na wote kutoka vyama saba kupitishwa huku SAU ikigonga mwamba baada ya kuhakikiwa na kukutwa taarifa za wadhamini wake zilizo sahihi ni za mikoa minne tu ya Tabora; Kilimanjaro; Kusini Pemba na Mjini Magharibi.
DP ilikuwa na matatizo ya wadhamini katika mikoa ya Pwani, Kilimanjaro na Dodoma na kukutwa na wadhamini sahihi katika mikoa saba.
Kutokana na kuenguliwa, SAU ilisema itaifikisha NEC mahakamani kwa madai kuwa walitimiza wadhamini wenye sifa katika mikoa 13 lakini Mchungaji Christopher Mtikila wa DP alisema hatakwenda mahakamani hadi NEC itakapomkabidhi nakala ya fomu za mikoa yenye matatizo. Mgombea mwenza wa Mtikila ni Khamis Msabaha.
Akizungumzia hatua hiyo ya kumwengua Paul Kyara wa SAU na mgombea mwenza Kibwana Said Kibwana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame alisema baada ya kupitia fomu za wadhamini waligundua zilizokuwa na matatizo ni za Pwani; Lindi; Dar es Salaam; Ruvuma; Tanga; Mbeya na Dodoma.
“Mfano, Tanga tuliona kati ya wadhamini wote waliothibitishwa ni 126 na 82 hawakuthibitishwa, wao walitwambia sababu kuu ni wasimamizi wa uchaguzi kukosa na fomu, hivyo NEC imeona hawakukidhi masharti ya kuwa na wadhamini mikoa 10 ambayo minane ni ya Tanzania bara na miwili Zanzibar na kwa masikitiko hawapewi nafasi kugombea,” alisema.
Hata hivyo, Kyara hakusema kitu katika chumba hicho cha mikutano wakati Jaji Makame akitangaza uamuzi wa Tume na alipotoka nje alizungumza na waandishi wa habari na kusema NEC haikuwatendea haki.
“Tatizo ni kwamba baadhi ya mikoa fomu hazikupigwa mihuri na sababu ya kushindikana kuhakiki ni kutopelekewa takwimu na tuliwaeleza makao makuu ya NEC wakasema tuje na fomu hapa wazihakiki na leo (jana) tumekuja saa 6 mchana, lakini wakatuweka chumbani wakatupa soda na saa 9 alasiri wakatuita na kusema hawawezi kuhakiki hadi waende bohari na jioni kuna foleni,” alisema na kuongeza:
“Wakatuweka tena na ilipofika saa 9.45 Kiravu (Rajabu, Mkurugenzi wa NEC), akatuita na kutwambia fomu hazijahakikiwa na tangu tumefika walijua yote, lakini wakachukua Sh milioni moja yetu na baadaye wametuengua na pesa hairudi,” alilalamika.
Awali Kiravu alisema kwa mujibu wa sheria, fedha ya dhamana ya Sh milioni moja inapopelekwa Tume, hairejeshwi isipokuwa kwa chama kilichopata kura zaidi ya asilimia 10.
Urejeshaji huo wa fomu ulianza kwa mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete na mgombea mwenza Dk. Mohamed Gharib Bilal ambao walipata wadhamini mikoa 12 ya Bara na minne Zanzibar.
Walifuatiwa na mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na mwenza Juma Duni Haji ambao walipata wadhamini katika mikoa minane ya Bara na minne Zanzibar.
Wengine waliorejesha na kuthibitishwa, ni Mutamegwa Mugahywa (TLP) na mwenza Abdullah Othman Mgaza; Dk. Wilbroad Slaa (Chadema) na mwenza Said Mzee Said.
Peter Mziray (APPT-Maendeleo) na mwenza Mchenga Rashid Yusuf, Fahmi Dovutwa (UPDP) na mwenza Hamad Mohamed Ibrahim na Hashim Rungwe (NCCR-Mageuzi) na mwenza Ali Omar Juma.
Akizungumza baada ya kurejesha fomu, Dk. Slaa aliahidi kuwa chama chake kitafanya kampeni za kistaarabu na kuongeza: “kampeni zetu zitakuwa za amani kwani hii ni nchi yetu na wote tunapigania Watanzania … kila mpiga kura naomba azingatie kitabu cha Polisi walichotoa”.
Profesa Lipumba aliwataka wananchi kulinda kura zao na kuahidi akishinda nafasi hiyo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa, atakuwa amebadilisha Katiba.
Vyama ambavyo havitashiriki kugombea urais ni Demokrasia Makini ambao hawakurejesha fomu na Jahazi Asilia ambao inaelezwa walikosa wadhamini huku NRA ambayo mgombea wake ni Julius Kiyabo haikurejesha fomu hadi saa 10 jioni muda ambao ulikuwa wa mwisho.
Wagombea waliothibitishwa, walikabidhiwa Sheria ya uchaguzi; sheria ya uchaguzi ya serikali za mitaa; sheria ya gharama za uchaguzi; kanuni za uchaguzi wa rais, wabunge, madiwani na maelekezo kwa vyama vya siasa na wagombea na maadili ya uchaguzi.
Kuanzia jana saa 10 jioni hadi leo saa 10 jioni taarifa za wagombea hao zitabadikwa katika ofisi za Tume, ili watu mbalimbali waweze kukaguliwa na wenye pingamizi kuwasilisha Tume.
Hata hivyo, Jaji Makame alisema kampeni ambazo zinaanza leo zitaendelea kwa chama ambacho kitawekewa pingamizi hadi hapo uamuzi wa Tume utakapotolewa.
No comments:
Post a Comment