TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imekamilisha uchunguzi wa kesi tano za ufisadi ndani ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); huku ikikamilisha uchunguzi kama huo ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Raia Mwema limethibitisha.
Habari za uhakika ndani ya TAKUKURU zilizothibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk. Edward Hosea, zimeeleza kwamba kwa sasa majalada matano yamekwishafikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kupata kibali cha kuwafikisha mahakamani wahusika.
Akizungumza na Raia Mwema katika mahojiano maalumu, hivi karibuni, Dk. Hosea alisema kuwa sehemu ya kwanza ya uchunguzi ndani ya NBC imekamilika na majalada matano yamepelekwa kwa DPP kupata kibali cha kuwashitaki wahusika, ambao baadhi ni maofisa waandamizi wa NBC na wafanyabiashara walioshirikiana nao katika wizi wa takriban Sh bilioni 4.
“Ni kweli tunashughulikia tuhuma za ufisadi ndani ya NBC na TRA na tayari kuna majalada matano tumeyafikisha kwa DPP kupata kibali cha kuwafikisha mahakamani wahusika,” alisema Dk.Hosea bila kutaja majina na idadi ya wahusika.
Wakati uchunguzi wa tuhuma za ufisadi dhidi ya wahusika ukiendelea ndani ya NBC na TRA, uongozi wa taasisi hizo mbili umekwisha kuchukua hatua dhidi ya wahusika kupisha uchunguzi dhidi yao.
Ndani ya NBC habari zimethibitisha kwamba maofisa waandamizi wanne (majina tunayahifadhi kwa sasa) wamekwisha kuchukuliwa hatua kufuatia matukio hayo ya ufisadi. Raia Mwema limethibitisha, hata hivyo, kwamba baadhi ya maofisa waandamizi wanaendelea na kazi licha ya kutajwa kuhusika katika ufisadi huo kwa kiasi kikubwa.
Uchunguzi wa Raia Mwema umethibitisha kuwapo mvutano mkali ndani ya NBC kabla ya wenye hisa wakuu wa benki hiyo - benki ya ABSA ya Afrika Kusini, kuingilia kati kutaka kuchukuliwa hatua madhubuti dhidi ya watumishi walioshiriki katika upotevu wa mabilioni ya fedha ndani ya benki hiyo.
Mvutano huo umeelezwa kusababishwa na kuhusika kwa vigogo wa juu wa benki hiyo kabla ya mabadiliko yaliyofanywa hivi karibuni kwa kuingia kwa Mkurugenzi mpya Lawrence Mafuru, ambaye alianza kazi rasmi Juni mosi, mwaka huu, kuchukua nafasi ya raia wa Afrika Kusini, Christo de Vries aliyeondolewa.
Uongozi wa NBC kwa kushirikiana na uongozi wa wafanyakazi, umekwisharidhia kusimamishwa kazi kwa maofisa wandamizi watatu na ofisa mmoja wa ngazi ya chini kuhusiana na kuhusika na upotevu wa zaidi ya Sh bilioni 4 kupitia akaunti hewa zilizofunguliwa katika matawi ya benki hiyo Dar es Salaam.
Uchunguzi dhidi ya ufisadi ndani ya NBC ulihusisha nyaraka za kughushi kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo za NBC yenyewe, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), TRA na za Benki ya CRDB Limited; nyaraka zilizoghushiwa kufanikisha uhalifu huo ambao uliitikisa benki hiyo katika siku za karibuni.
Uchunguzi wa awali ulihusisha pia makachero kutoka kwa wamiliki wa hisa kubwa za benki hiyo, taasisi kubwa ya fedha Afrika Kusini ya ABSA Group Limited, ambao kwa kiasi kikubwa walihakikisha wanasafisha uozo ndani ya benki hiyo.
Habari zaidi zinaeleza kwamba maofisa wanaotuhumiwa kushiriki wizi huo wamekuwa na tabia ya kupoteza hati za dhamana zinazotumiwa na baadhi ya wateja kuchukua mikopo na kusababisha benki hiyo kupata hasara kubwa kwa kushindwa kukamata mali za wateja wanaoshindwa kulipa madeni.
Katika tukio moja wapo la wizi ndani ya NBC, baadhi ya maofisa wa benki hiyo tawi la Corporate walituhumiwa kuhusika na akaunti hewa iliyochotewa kiasi cha Sh milioni 900 ikihusisha akaunti namba 011103033038 iliyodaiwa kumilikiwa na kampuni moja (jina tunalihifadhi kwa sasa).
Benki ya NBC Limited ilibinafsishwa mwaka 2000 baada ya kuendeshwa kwa miaka mingi kama shirika la umma. Ni kati ya mashirika ya umma yaliyozua utata mkubwa wakati wa kubinafsishwa kutokana na kile ambacho hadi leo wengine wanasema iliuzwa kwa bei ya kutupa.
Wakati ABSA Group Limited ya Afrika Kusini inamiliki hisa 55 ndani ya NBC, Serikali ya Tanzania inamiliki hisa 30 na Shirika la Kimataifa la Fedha (International Finance Corporation) linamiliki hisa 15.
Kwa upande wa TRA, tayari bodi ya mamlaka hiyo imeamua kuwachukulia hatua maofisa wake waandamizi kupisha uchunguzi dhidi yao; huku TAKUKURU ikiendelea kukamilisha uchunguzi dhidi yao.
Maofisa wa Idara ya Ushuru wa Forodha waliosimamishwa na Bodi ya TRA kwa tuhuma za ama kushiriki au kufumbia macho vitendo vya ukwepaji kodi, wameamriwa wajieleze huku hatua zaidi zikichukuliwa kwa maofisa wengine wa chini.
Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Dk. Marceline Chijoriga, alilieleza Raia Mwema ya kuwa, aliyekuwa Naibu Kamishna wa Ushuru wa Forodha, Generose Bateyunga, ameondolewa katika nafasi yake kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomhusu pamoja na wahusika wengine.
“Wapo wahusika ambao ni wafanyakazi wa TRA lakini waajiriwa wa Bodi, hawa ni makamishna na naibu makamishna na hata mameneja, lakini wapo pia wahusika wengine ambao ni walioajiriwa na Menejimenti ya TRA.
“Sasa kwa taratibu za kazi, mimi ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi, nashughulikia hawa ambao mikataba yao ya ajira wamepewa na Bodi na Menejimenti inashughulikia wengine. Hatua tulizokwishakuchukua hadi sasa ni kuitaka Menejimenti imwondoe Kamishna (Naibu) wa Forodha Bateyunga impangie kazi nyingine tofauti wakati uchunguzi unaendelea.”
Akizungumzia uchunguzi ndani ya TRA, Dk. Edward Hosea alisema ofisi yake inafanya uchunguzi mkali kuhusiana na suala la ukwepaji kodi ndani ya TRA na kwamba hatua madhubuti zitachukuliwa.
“Suala la TRA tunalo na tunalifanyia kazi kwa karibu sana. Wakati muafaka tutawaeleza hatua tutakazochukua dhidi ya wahusika... Watu wajue tu tuko kazini wakati wote na hasa kwa mambo ya msingi kama hayo yanayogusa uchumi wa Taifa,” alisema Dk. Hosea katika mahojiano yake na Raia Mwema.
Hatua hizo za Bodi ya TRA na Takukuru zinafuatia taarifa za raia wema ambazo hatimaye zilichapishwa na Raia Mwema zikihusu ufisadi wa kutisha ndani ya Idara ya Forodha ambako, pamoja na mambo mengine, imeelezwa ya kuwa familia moja ya Dar es Salaam inayomiliki kampuni inayojihusisha na biashara ya bidhaa za nyumbani imekuwa ikiendesha uwakala wa forodha kwa ama yenyewe kukwepa kodi au kuwasaidia wafanyabiashara wengine kukwepa kodi huku ikijiwekea kinga kwa wanasiasa.
Taarifa za awali zilizoifikia Raia Mwema na kuandikwa kwa kirefu katika matoleo yake mawili ya nyuma zinaonyesha kuwa biashara hiyo ya uwakala wa ukwepaji kodi imekuwa ikiipotezea Serikali mapato ya mabilioni ya shilingi ambazo zilistahili kukusanywa kutoka kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbalimbali kutoka China na Dubai ambako kampuni hiyo imefungua ofisi “kurahisisha” shughuli zake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mtandao wa kampuni hii ni mkubwa, unajumuisha baadhi ya watendaji wa TRA, wakubwa kwa wadogo na umevuka mipaka hadi Hong Kong na Guanzhou, China na Dubai. Ofisi za nje ya Tanzania hutumika kupokea mizigo inayoingia nchini.
Imeelezwa kwamba mwagizaji wa mali yoyote kama nguo, hardware au vifa vya umeme hufanya manunuzi kwenye maeneo hayo na hupewa gharama zote za kufikisha mzigo Dar es Salaam pamoja na ushuru wa forodha na gharama nyinginezo hadi kweye bohari yao iliyopo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa hizo mwagizaji anakabidhi mzigo ofisini China na anakabidhiwa mali yake Dar es Salaam baada ya siku kadhaa kati ya wiki tano hadi sita.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini viwango vya gharama zao kwa baadhi ya mali ni kama ifuatavyo:
Kusafirisha na kutoa bandarini vifaa vya ujenzi hutoza dola za Marekani 350.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za nguo ni dola za Marekani 450.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Kusafirisha na kutoa bandarini bidhaa za umeme kama swichi, circuit breakers na viginevyo ni dola za Marekani 500.00 kwa meta moja ya ujazo (1 cbm).
Mizigo maalumu kama vitenge-mazungumzo hufanyika na bei maalumu hukubaliwa.
“Kinachotisha katika utaratibu huu ni kwamba wakati gharama za usafiri wa meli hupatikana kutegemea uzito na ujazo wa mali, wao wamefika mbali zaidi kwa kukadiria ushuru na kodi za Serikali kwa ujazo (yaani cubic measurements). Kwa kawaida ushuru wa forodha hutozwa kwenye Thamani halisi ya Manunuzi, Bima na Gharama za Usafiri hadi nchini (Cost, Insurance and Freight) na si vinginevyo,” alisema mtumishi mmoja wa TRA mwenye ufahamu wa biashara hiyo akidai kwamba biashara hiyo huwa na ulinzi wa ‘wakubwa’.
Kwa mujibu wa taarifa hizi, kati ya nguvu iliyonazo kampuni hiyo ni ukaribu wake na wanasiasa ikielezwa kwamba kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kampuni hiyo ilikichangia chama tawala Sh. Milioni 200 na kwamba katika mwaka huu imeahidi kuchangia milioni 500.
Uchunguzi wa Raia Mwema umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya fedha hutumika katika kulipia ushuru kidogo, rushwa kwa maofisa sehemu mbalimbali husika, gharama za bandari na usafiri wa bandarini kwenda kwenye maghala yao.
No comments:
Post a Comment