Tuesday, August 24, 2010

JK achanja mbuga, amwaga ahadi

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, ameahidi kununua kivuko cha Maisome katika jimbo la Buchosa mkoani Mwanza ili kuwaondolea adha wananchi wanapotaka kuvuka maeneo hayo.

Aliyasema hayo jana mjini hapa akiwa katika siku yake ya pili ya ziara yake mkoani Mwanza ya kuomba ridhaa ya wananchi kumchagua kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Rais Kikwete alisema serikali ya Marekani nayo imeahidi kununua meli maalum ya doria kwa ajili ya kuimarisha usalama katika Ziwa Victoria.

Rais Kikwete aliahidi kutoa Sh. milioni 530 kama malipo kwa wafanyakazi wa Chama Cha Ushirika cha Mkoa wa Mwanza (Nyanza) ili walipwe baada ya chama chao kufa kutokana na ubadhirifu.

Rais Kikwete aliahidi pia kutoa Sh. bilioni tano kukifufua chama hicho na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

Rais Kikwete aliahidi kuendelea kuimarisha miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza ili kuwaondolea adha wananchi.

Akiwa katika Jimbo la Buchosa, Rais Kikwete alimsimamisha mgombea ubunge kupitia CCM aliyeshika nafasi ya pili katika kura za maoni, Eric Shigongo, na wananchi wakalipuka kwa shangwe na nderemo.

Baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza, Shigongo aliahidi kuvunja makundi ya wakati wa kura za maoni na kumuunga mkono mgombea aliyeshinda.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina, jana alinogesha mikutano ya kampeni hizo kwa kueneza sera kwa lugha ya Kisukuma.

Alikuwa akizungumza Kisukuma wakati wa kampeni za CCM Jimbo la Buchosa na Sengerema hali iliyoonekana kuwakuna wananchi wengi na kumshangilia mara kwa mara.

Akiwa wilayani Geita, Kikwete alisema mgodi wa Geita Gold Mine GGM), utatoa Sh. bilioni 9 kwa ajili ya mradi wa maji wilayani humo na serikali kwa upande wake itatoa Sh. bilioni sita kwa ajili ya shughuli za usambazaji wa maji.

Alitangaza kuwa kuanzia Januari mwakani wilaya ya Geita itakuwa mkoa rasmi na kwamba shughuli za ujenzi wa makao makuu ya mkoa huo yanaendelea vizuri.

Rais Kikwete pia alisema wachimbaji wadogo wadogo wa Geita wasiingiliwe na wachimbaji wakubwa katika maeneo yao ya uchimbaji.

Akiwa Geita na Sengerema, aliahidi kuwa maeneo ya wilaya hizo yatapatiwa umeme.

No comments: