Friday, August 13, 2010

Panga lafyeka wagombea

-Baadhi ya viongozi CCM wahongwa magari
-Dar baadhi ya walioshinda wakatwa majina-
-Arusha, Mbeya na Shy mambo shaghalabaghala

WAKATI baadhi ya wanasiasa walioshindwa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya ubunge na udiwani, wakitajwa kujiunga na upinzani, tayari chama hicho tawala kimeanza mchakato wa kuwakata wagombea wake wakiwamo baadhi walioshinda kura za maoni, Raia Mwema limeelezwa.

Habari za ndani ya vikao vya CCM zimeeleza ‘panga’ limeanza katika ngazi ya mikoa na tayari halmashauri za chama hicho katika baadhi ya mikoa zimemaliza kazi ya kuwachuja wagombea na kupeleka taarifa hizo kwenye vikao vya juu.

Kwa mujibu wa habari hizo ambazo gazeti hili limezipata, baadhi ya wagombea waliokatwa katika vikao hivyo wamerudishwa baada ya kubainika kuwapo kwa nguvu kubwa ya fedha katika kushinikiza uamuzi wa vikao hivyo hali inayoashiria kuenea kwa uoza katika mchakato wa kuwapata wagombea.

Wakati hayo yakijiri, habari za uhakika zinaeleza kwamba baadhi ya wagombea hao wa CCM wametumia fedha nyingi katika kuhakikisha wao na watu wanaowaunga mkono wanapitishwa akiwamo kiongozi mmoja anayetajwa kuhongwa gari mkoani Dar es Salaam kwa lengo la kuhakikisha anatekeleza matakwa ya mgombea mmoja mwenye malengo ya kushika nafasi mojawapo ya juu mkoani humo.

Kwa mujibu wa habari hizo, mgombea huyo (ambaye pamoja na aliyepewa gari kwa sasa hatutawataja) ametumia fedha nyingi katika kuhakikisha anasimika viongozi katika karibu kila kata za mkoa anakotoka na wengi kati ya hao akiwa anawafadhili na kuwasimamia katika kuhakikisha wanapitishwa na vikao vyote vya CCM kuanzia ngazi za wilaya, mkoa hadi Taifa.

Maeneo mengi mkoani humo yalishuhudia si tu vurugu bali pia aibu ya kwamba baadhi ya viongozi wamehusika moja kwa moja kuvuruga uchaguzi katika baadhi ya maeneo kwa maslahi binafsi, baadhi wakielezwa kukiri hadharani kwamba walihongwa na baadhi ya wagombea na watu wazito wenye maslahi katika uchaguzi wa mwaka huu.

Tayari kumeibuka malalamiko kadhaa katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara (soma pia ukurasa wa 4 [Kanda ya Ziwa], ukurasa wa 5 [Kanda ya Kaskazini] na ukurasa wa 6 [Kanda ya Kusini]) na Visiwani ambako baadhi ya wagombea wakiwamo wabunge waliomaliza muda wao na wagombea wapya, wamelalamikia kuwa kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa taratibu na matumizi makubwa ya fedha.

Taarifa zaidi za kiuchunguzi na ambazo hivi karibuni zimethibitishwa na uongozi wa juu wa CCM kitaifa, zinabainisha kuwa si rufaa zote za wagombea zitapatiwa ufumbuzi, ishara zikionyesha baadhi ya wagombea wanaweza kukataliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa ambao wanapewa nafasi kufanya hivyo na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Kanuni za Sheria hiyo mpya ya Gharama za Uchaguzi inatoa nafasi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia taarifa za utafiti kutoka kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa, kugoma kuteua majina yaliyowasilishwa na chama husika kugombea uongozi kama itabainika mhusika amekiuka sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na kuhusika katika vitendo vya rushwa.

Nguvu hizo alizopewa Msajili wa Vyama vya Siasa zilipingwa na baadhi ya wabunge na wanasiasa ndani ya CCM kwa madai kuwa zinaingilia shughuli za vyama vya siasa na kwamba ni vema uamuzi wa nani agombee ukaachwa katika chama husika cha siasa kama chombo cha mwisho.

Mazingira ya nguvu za Sheria ya Gharama za Uchaguzi yanajidhihirisha kutaka kutumika na tayari hivi karibuni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alikemea namna matumizi ya rushwa yaliyojitokeza katika kura za maoni za CCM akieleza kuwa atashangaa kama chama hicho kitawapitisha wanaotuhumiwa kuhusika na tatizo hilo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ndogo ya nidhamu ya chama hicho, amethibitisha kuwa si rufaa zote zitakazoweza kusikilizwa kutokana na wingi wake na muda wa kufanya hivyo kuwa mfupi lakini akiahidi kuwa uamuzi utaendelea kufanyika na ikibidi wagombea walioshinda kwa mchezo mchafu kuenguliwa bila kujali kama wakati wa uteuzi kwa maana ya Tume ya Uchaguzi na CCM kwenyewe umepita.

Msekwa alitoa maelezo hayo Jumatatu wiki hii na kunukuliwa na gazeti la CCM, Uhuru, akisema wataendelea kuyafanyia kazi (malalamiko) hata baada ya uteuzi wa wagombea na adhabu zitatolewa hata kama mtuhumiwa ameshinda ubunge au udiwani na kwamba watendaji wa chama hicho waliozembea na kuvuruga uchaguzi pia wataadhibiwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye majimbo mbalimbali ya uchaguzi nchini ambako CCM imeendesha mchakato wa kura za maoni, kuna taarifa kuwa mbali na TAKUKURU kukusanya ushahidi na wakati mwingine kulazimika kukamata na kuwahoji baadhi ya wagombea, baadhi ya maofisa wa Serikali walikuwa wakifuatilia nyendo za wagombea katika kinachoelezwa kuwa walikuwa wakikusanya taarifa huru za mwenendo wa kura hizo za maoni. Taarifa hizo zinaaminika kuwasilishwa katika baadhi ya vyombo vya dola na kulinganishwa na zile za maofisa wa TAKUKURU.

Katika hatua nyingine, baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, wamepongeza utaratibu wa CCM kuwapa wanachama wake nafasi ya kupiga kura za kupendekeza wagombea wakisema hali hiyo kwa sehemu kubwa imesaidia kufichua viongozi wasio na maadili mbele ya jamii.

Kati ya wasomi hao ni Profesa Samuel Mushi ambaye anasema: “Nawapongeza CCM kuamua mchakato wa kura za maoni kufanywa kwa uwazi. Ni uamuzi ambao umetuwezesha kubaini ule uchafu ambao ungeweza kufichwa chini ya zulia. Ni sawa na mtu anaweza kufagia na kuficha uchafu kwenye kapeti akijidai nyumba yake safi.”

Akizungumza na katika mahojiano ya simu na Raia Mwema wiki hii, Profesa Mushi alisema rushwa si jambo jipya, bali ni la muda mrefu na limekuwa likizusha malalamiko mengi miongoni mwa wananchi akiweka bayana kuwa sasa nchi imedhihirika imeingia katika kile alichokiita danger zone (ukanda wa hatari).

“Kitendo hiki kilichojionyesha CCM si cha kufumbiwa macho hasa kwa upande wa wahusika, lakini CCM kama taasisi inapaswa kupongezwa kwa kuamua kuweka uwazi kwenye chaguzi zake. Ni kama vile kimechoka kuonekana kinafungamana na watoa rushwa. Lakini kikubwa kwa upande wa nchi ni kutambua kuwa sasa tupo kwenye danger zone na kwa hiyo ni lazima turejee nyuma kimaadili na kujisahihisha na kukataa wasiotaka kujisahihisha kuwa viongozi wetu.

“Vyombo vya dola lazima vionyeshe dhamira ya kutuondoa kutoka kwenye danger zone, vipiganie dhamira hiyo. Napenda kuipongeza TAKUKURU kwa hatua zake hizi za awali kushughulikia tatizo hili. Sheria zitumike kikamilifu,” alisema Profesa Mushi.

Alipoulizwa kuhusu wimbi la wafanyabiashara kuamua kupenya zaidi kwenye siasa huku kukiwa na mazungumzo ya kuandaliwa kwa muswada unaolenga kutenga siasa na biashara, alisema uamuzi wao huo unaendeleza kile kilichoanza kujitokeza tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili, baada ya kufa kwa Azimio la Arusha lililokuwa likipigania masharti na maadili ya uongozi.

“Tangu wakati ule walipoua Azimio la Arusha na kuanzisha Azimio la Zanzibar utaona kuwa nguvu huria ilichukua nafasi yake. Zilianza siasa za soko huria, matajiri walipata njia ya kushawishi na kuhakikisha mifumo ya sheria, kibiashara na hata mifumo ya kisiasa kulinda maslahi yao. Wakapata fursa baadhi wakitumia nguvu za fedha kupenya kwenye siasa kwenye uwaziri…kwa hiyo ni haki yao kwa kuwa mifumo ya sheria imebadilishwa.

“Tatizo kuwa na wimbi la wafanyabiashara linaweza kujitokeza tu pale utajiri wao wanapoamua kuutumia kununua kura za wananchi na kwa mantiki hiyo kununua haki ya wananchi,” alisema Profesa huyo ambaye alipata kushiriki kuandika machapisho mbalimbali yanayoonyesha jinsi soko huria lilivyokuwa soko holela kiasi cha kuvuruga maadili mema yaliyozingatiwa awali katika Azimio la Arusha.

Kwa upande wake, Profesa Haji Semboja, ambaye ni gwiji wa uchumi alizungumzia mchakato wa kura za maoni CCM akisema:

“Mimi natofautiana kidogo. Kama mchumi sitaki kuiita hii eti ni rushwa inayotishia uchumi…kwa nchi masikini kama Tanzania kilichofanywa na wagombea hawa wa CCM ni kama uwezeshaji.

“Tusiache kukabili tatizo kubwa zaidi na wote kujielekeza kwenye tatizo dogo na la mpito. Tukumbuke hii ni nchi yenye watu masikini na kwa hiyo kampeni wakati mwingine ni lazima zihusishe wagombea kujinadi kwa kuzingatia yale ambayo washindani wengine hawawezi kuwa nayo.

“Hakuna anayeweza kujinadi bila kuwa na uwezo wa kuwawezesha wananchi. Tofauti inayojitokeza ni kuzidiana uwezo tu kati ya washindani.””

Hata hivyo, alisema anasubiri kwa hamu kuona jinsi TAKUKURU watakavyoweza kusimamia Sheria ya Gharama za Uchaguzi mara baada ya kampeni kuanza kwa kuwa kwa wakati huo matumizi ya fedha kwa sehemu kubwa yatakuwa yakifanywa na chama cha siasa badala ya mgombea mmoja mmoja, na kwamba inavutia zaidi kuona kama chombo hicho kitakuwa na ubavu wa kudhibiti vyama vyote kwa usawa, kikiwamo CCM.

Lakini akizungumzia kuhusu vigogo walioanguka alisema; “Lakini ieleweke kuwa kwa wale ambao hawakupita si kwamba hawatakiwi au hawawezi bali kilichotokea ni wapiga kura za maoni katika maeneo husika kutaka mabadiliko ya kiongozi au viongozi.

No comments: