-Azindua ilani ya CUF
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amezindua Ilani ya uchaguzi ya chama hicho na kuahidi kuwa iwapo atafanikiwa kuingia Ikulu atapambana vikali na 'mchwa' wanaotafuna fedha za umma.
Vile vile, Profesa Lipumba alisema ataimarisha mfumo wa ukusanyaji wa kodi ili kupunguza utegemezi wa wahisani katika bajeti ya serikali kwani ni aibu nchi kuendelea kuwa omba omba.
Akizindua ilani hiyo jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, Profesa Lipumba alisema hakuna sababu ya kuendelea kutegemea nchi wahisani wakati taifa lina rasilimali nyingi na vyanzo vingi vya mapato ambavyo vikisimamiwa vyema nchi inaweza kujitegemea.
Alisema asilimia 30 ya mapato ya serikali yanaishia mikononi mwa mafisadi hivyo kuifanya nchi kuendelea kuwa tegemezi wakati fedha hizo zingetosha kabisa kuiwezesha serikali kujiendesha.
Alisema mapato ya fedha za mfuko wa barabara ambayo yanapatikana kupitia makato katika mafuta ni makubwa, lakini yamekuwa yakipotelea mikononi mwa mafisadi wachache hivyo kukwamisha maendeleo ambayo yangepatikana kupitia fedha hizo.
Alisema akiingia Ikulu, CUF itahakikisha uchumi wa taifa unakuwa kwa angalau asilimia saba hadi 10 kwa mwaka, hali itakayowezesha huduma nyingi za jamii kupatikana kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa.
Katika Ilani hiyo, Lipumba alisema chama chake kitahakikisha asilimia 25 ya mapato ya serikali yanakwenda kuboresha sekta ya elimu nchini.
Alisema asilimia 15 ya mapato hayo ya serikali yatatumika katika kuboresha kilimo, asilimia 15 sekta ya afya na sekta nyinginezo zitapewa asilimia 20 hadi 25 ya mapato hayo.
Aidha, Profesa Lipumba alisema serikali yake itaongeza uzalishaji wa chakula kwa kiwango kikubwa ili wananchi wapate lishe nzuri tofauti na sasa ambapo wananchi wengi wanaishi kwa kubahatisha na hawana uhakika wa chakula.
Alisema idadi ya Watanzania maskini imeongezeka kutoka milioni 11 mwaka 2005 hadi kufikia watu milioni 12.5 mwaka huu na kwamba CUF itahakikisha inabadili hali hiyo kwa kuongeza ajira na kuwawezesha watu kujiajiri hivyo kuondokana na lindi la umaskini.
Alisema atajikita katika kupambana na ufisadi na rushwa kwani serikali ya sasa imeshindwa kabisa kukabiliana na vitendo hivyo na kwamba kesi zilizopelekwa mahakamani ni geresha tu.
Alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya umeme ambavyo ni gesi, upepo na jua ambavyo vinaweza kutumika kuimarisha miundombinu ya nishati ya umeme na kuondokana kabisa na umeme wa kubahatisha.
Alisema katika suala la teknolojia, CUF itahakikisha somo la kompyuta linakuwa la msingi kuanzia chekechea na kila mwanafunzi anakuwa na kompyuta yake wakati wa masomo.
“Ukizungumzia suala hili watu wanakuona kama unaota, lakini si kitu kigumu na kinawezekana kabisa tukidhamiria kuleta mapinduzi katika teknolojia ...kuna watafiti wamegundua kompyuta ndogo (laptop) ambazo zitakuwa zikiuzwa kwa dola 100 hivyo tutazinunua kwa wingi na kuzitumia,” alisema Profesa Lipumba ambaye pia ni mwenyekiti wa CUF taifa.
Alisema CUF imesimamisha wagombea ubunge katika majimbo 139 Tanzania Bara na katika majimbo 50 ya Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment