Friday, August 20, 2010

Aliyetaka kumuuza albino afungwa miaka 17

RAIA wa Kenya aliyeianza safari yake nchini mwao akifuatana na rafiki albino kwa kumrubuni kumtafutia kazi jijini Mwanza, lakini badala yake akataka kumuuza kwa Sh milioni 400, amehukumiwa kifungo cha miaka 17 jela.

Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani hapa jana ilimhukumu Nathan Mtei (28) kifungo hicho na faini ya Sh milioni 80, baada ya kupatikana na hatia ya kumsafirisha na kumtorosha binadamu kwa lengo la kumuua.

Awali akimsomea maelezo ya mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Angelo Rumisha, Mwanasheria wa Serikali, David Kakwaya, alisema mshitakiwa alitenda makosa hayo Agosti 15 mwaka huu kwa kudhamiria kumuua Robinson Mtwana (20) raia mwenzake wa Kenya ambaye ni albino.

Baada ya mshitakiwa kusomewa maelezo, Kakwaya alisema kitendo cha kusafirisha binadamu ni kosa la kisheria hivyo kuiomba mahakama ifikirie adhabu dhidi ya mshitakiwa kwa kuwa makosa hayo yanadhalilisha utu wa binadamu.

“Vitendo vya kusafirisha binadamu kwa lengo la kumuuza vilikuwa vikifanyika enzi za biashara ya Utumwa, kwa kuwa vilikuwa vikidhalilisha utu wa binadamu … biashara hiyo ilizuiwa,” alisema Mwanasheria wa Serikali.

Aliongeza kuwa mwathirika wa tukio hilo ni mlemavu wa ngozi, watu ambao wamekuwa wakiandamwa nchini na matukio ya kuuawa na inaonesha wazi lengo la mshitakiwa lilikuwa ni kuua.

“Madhara ambayo yangetokea endapo mshitakiwa angetekeleza azma yake ni makubwa na yangesababisha mwathirika huyo kuuawa, hivyo tunaiomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshitakiwa,ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye nia kama ya mshitakiwa,” alisisitiza Kakwaya.

Akisoma hukumu, Hakimu alisema tukio hilo limeleta picha mbaya kwa Tanzania, kwani imekuwa na matukio kama hayo.

Aliongeza kuwa adhabu aliyopewa mshitakiwa kwa kosa la kwanza atatumikia kwa miaka tisa jela au kulipa faini ya Sh milioni 80 na kwa kosa la pili atatumikia miaka minane.

Lakini kama atalipa faini adhabu zote zitatumika tofauti. Alibainisha kuwa adhbu hiyo imetolewa dhidi ya mshitakiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye uroho na tamaa ya fedha kama aliyonayo mshitakiwa.

Kabla ya kutoa hukumu, Hakimu alimtaka mshitakiwa ajitetee.

Aliiomba Mahakama imsamehe au iruhusu kesi ikasikilizwe Kenya kwa kuwa anategemewa na familia yake.

Mshitakiwa aliongeza kuwa mganga wa kienyeji alichangia kutenda kosa hilo, kwani anahisi alimfanyia dawa hata kuingia tamaa.

Hata hivyo, Hakimu alisema mshitakiwa anaruhusiwa kukata rufaa Mahakama Kuu ndani ya siku 45 kuanzia jana, ikiwa hajaridhishwa na hukumu iliyotolewa dhidi yake.

No comments: