Na Juma Nyumayo, Dar es Salaam
KUTOKANA na migogoro mingi inayoibuka katika ngazi ya kaya na familia hapa nchini kutokana na kuwa na mahusiano mabaya katika kuzalisha na kumiliki mali, familia hizo zimetakiwa kujenga na kuboresha mahusiano yao kwa kufuata vigezo vya uwazi na upendo hatua kwa hatua kabla mali wanazozalisha hazijawatesa kwa kuwagombanisha kwa kile kinachodaiwa nani mmiliki halali kati ya mwanamke na mwanamume.
Hilo ni moja ya azimio lililofikiwa na washiriki wa warsha ya Uchumi na Ukombozi wa mwanamke kimapinduzi inayoendeshwa na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia cha TGNP katika Ukumbi wa kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha dar es Salaam.
Katika hali ya kubaini tatizo kuu la wanandoa pia familia nyingi kusambaratika kutokana na migogoro ya nani amiliki mali, au kurithi wanawarsha hao wamechambua mbinu mbalimbali na kuja na mapendekezo ambayo huenda yakapunguza tatizo linalozikabili familia nyingi hapa nchini hasa kutokana na mfumo dume unamtenga mwanamke kumiliki mali hasa zenye thamani.
Sheikh wa wilaya ya Liwale, Adam Mpelengana, alisema ni muhimu kwa wanaume wote kutambua kuwa wanawake ni wasaidizi wa mwanamume na ni jukumu la mwanamume kumpenda na kufanyia haki anazostahili badala ya kumuachia kazi nyingi bila usaidizi.
"Mwanamke anatakiwa aenziwe apendwe kwa kila namna, haifai kuendekeza mila na desturi za kumtumikisha mwanamke,' alisisitiza Sheikh Mpelengana.
Awali Mchungaji wa KKT toka Shinyanga, Odorus Gyunda , alisema ni muhimu kubainisha wazi ukatili wanaofanyiwa wanawake ni kinyume cha mapenzi ya mungu.
"imeelezwa wazi kuwa Mwanaume ampende mke wake na mwanamke amtii mumewe," alisema na kubainisha kuwa hayo hayawezekani kama hakuna upendo na mawasiliano mema katika uzalishaji na taratibu zote za kuishi.
Hata hivyo wanawarsha hao wamependekeza kuwa ili kusiwe na migogoro katika matumizi ya fedha na umiliki wa mali ni vyema wenza wakashiriki kikamilifu maamuzi ya kupanga utafutaji wa fedha au mali hatua kwa hatua mapema.
jambo jingine lililoelezwa ni wanawake na wanaume kwenye kaya zinazotegemea kilimo wajue mahitaji yao ya chakula mapema wakati wa kuandaa mashamba ili wasije uza chakula chote kwa tamaa ya fedha.
Wakijadili suala la kudhibiti matumizi na kuweka kumbukumbu za mapato katika ngazi ya kaya washiriki hao wamependekeza kuwe na daftari la pamoja la kuwekea kumbukumbu za mapato na matumizi katika kila hatua.
Aidha wamewaasa wanawake kuwa makini na mchango wa nguvu kazi zao katika kuhudumia familia pia kuzalisha mali katika kaya na kuhoji matumizi na shughuli za kila mmoja katika kaya husika.
Vilevile imeelezwa wazi kuwa usafi na kujali afya za wanafamilia ni mtaji mkubwa katika kuleta mahusiano mema katika kutumia muda na kumiliki mali za kaya.
Washiriki hao hawakuishia hapo, walisema hayo yatawezekana iwapo, kutatengwa walao siku moja katika wiki kuzungumzia masuala na maendeleo ya kaya husika kwa kuwahusisha mume, mke na watoto ili kaya ziendeshwe kwa shughuli na bajeti zenye mtazamo wa kijinsia zaidi.
No comments:
Post a Comment