JAJI Mkuu Mohamed Othman Chande, amesema mabadiliko ya Katiba yatakayofanyika nchini yasiwe ya kuiga kutoka nchi nyingine bali yawe ya Watanzania wenyewe.
Jaji Chande alisema hayo Dar es Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kufungua jengo jipya la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) cha Jaji Mwalusanya uliokwenda sambamba na sherehe za miaka 16 ya LHRC.
Alisema “haki za binadamu si za kijamii tu au kisiasa, bali zinalenga kwa watu wote kuwa na haki ya kupata kazi, nyumba ... kuna nchi kama Kenya na Afrika Kusini zimefanya
mabadiliko ya Katiba, hivyo kama sisi tunafanya mabadiliko tuangalie wananchi wetu na si tuige katiba za wenzetu”.
Alisema pamoja na kwamba ni kweli Katiba iliyopo ina upungufu, marekebisho yanatakiwa waachiwe Watanzania wenyewe kwa faida yao.
Akizungumzia adhabu ya kifo Jaji Mkuu alisema adhabu hiyo inakiuka Katiba na katika mchakato wa marekebisho, suala hilo litaangaliwa.
“Utafiti unaonesha kwamba kila mwaka nchi mbili au tatu zinafuta adhabu ya kifo, na Tanzania ni nchi ambayo adhabu hiyo haitekelezwi, kwa sababu inaathiri haki za binadamu na msimamo wa Umoja wa Mataifa unaosisitiza nchi zote kufuta adhabu hiyo,” alisema.
Kuhusu kesi za uchaguzi, alisema tayari mahakama zimeanza kuzisikiliza zaidi ya 20 katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kilwa na Arusha Mjini.
Aidha, alitaka wananchi waelimishwe zaidi kuhusu sheria ili wafahamu haki zao na kuitaka Serikali kukamilisha sera ya kutoa msaada wa kisheria haraka ili kusaidia wasiojiweza wapate haki zao.
Pia alisema kwa kutambua mchango wa kituo hicho, mahakama imeahidi ushirikiano wa hali ya juu katika utoaji haki.
Mwenyekiti wa Bodi ya LHRC, Askofu Elinaza Sendoro, alisema kituo hicho kimekuwa
kikitoa msaada wa sheria kwa wasio na uwezo ambapo katika kesi wanazopokea nyingi ni mashauri ya ndoa na viwanja (migogoro ya ardhi).
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Francis Kiwanga, alisema ardhi inayofaa kwa kilimo inaweza kutoweka kutokana na kutolindwa na kugawanywa bila mpangilio maalumu.
“Wapo wajanja wachache kwa kutumia viongozi walio serikalini, wanawadanganya wananchi na kuwapora ardhi, hivyo ukiwapo uwezeshaji wa sheria, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ardhi nchini,” alisema.
Alisema bado suala la utawala wa ardhi halijapangwa vizuri, hivyo upo umuhimu wa kuwajengea wananchi uwezo wa kufahamu haki za ardhi ili wazilinde.
No comments:
Post a Comment