Tuesday, September 6, 2011
Makongoro Nyerere Aapa Kuwaning'iniza Mafisadi CCM
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere ametangaza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho(Nec), kuhoji sababu za watuhumiwa wa ufisadi kushindwa kujiuzulu hadi sasa huku akimtaka Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kuachana na watuhumiwa hao.
Msimamo huo wa Makongoro ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere unakuja kipindi ambacho kikao cha Nec ya CCM kinatarajiwa kufanyika mwezi huu baada ya kile cha Kamati Kuu (CC) kilichoketi Mjini Dodoma mwezi uliopita kutoa muda zaidi kwa watuhumiwa hao kujipima hadi mkutano huo wa Nec.
Akifungua mkutano maalumu wa Nec ya CCM wilayani Bunda, Makongoro alisema kilichopo sasa ni kama mchezo wa kuigiza ambao hauingii akilini, hivyo akasema ni vyema akawasilisha hoja kwenye kikao hicho kuhoji uhalali wa watuhumiwa hao kuendelea kubaki na nyadhifa zao ndani ya chama.
Uamuzi wa kuwataka watuhumiwa hao kujivua gamba uliamuliwa na Nec iliyoketi mjini Dodoma Aprili, ambako pia CC iliyokuwapo ilijiuzulu na kuundwa upya huku Sekretarieti iliyokuwa chini ya Katibu Mkuu, Yusuph Makamba ikivunjwa na kuundwa upya kama mwanzo wa kujenga mwelekeo mpya wa chama.
Tangu wakati huo, mpango wa kujivua gamba umekuwa ukipigwa danadana kwani awali, ilielezwa kwamba watuhumiwa walipewa siku 90 baada ya kutakiwa kupima tuhuma dhidi yao lakini baadaye CCM ikakanusha na hadi sasa wengi wao wanaendelea na nyadhifa zao.
Makongoro akizungumzia zaidi danadana hizo, alisema huenda kinachowatia kiburi kugoma kung'oka kwenye nyadhifa zao ni uhusiano wa karibu walionayo na Rais Kikwete.
Alimtaka Kikwete kuachana nao na kusimamia kikamilifu uamuzi uliofikiwa na CC ili kukijengea heshima chama hicho.
Alisema kutowajibika kwa wanachama hao kunakitia doa chama hicho mbele ya jamii ambayo imekuwa ikikiamini kutokana na historia yake ya uadilifu.
“Nasema mbele yenu; sifurahishwi na watuhumiwa hao kuendelea kubakia ndani ya chama. Nitawasilisha hoja mbele ya kikao cha halmashauri kuu kuhoji kwa nini bado wamo huku wakikichafua chama?”
Makongoro ambaye aliwataja watuhumiwa hao kwa majina, alisema kuendelea kuwamo ndani ya chama hicho kunakifanya kikose mvuto na mashiko kwa jamii.
Katika kikao cha Nec Aprili, mwaka huu Makongoro alikuwa mwiba kwa watuhumiwa hao huku akihoji mantiki ya mwenyekiti wake kuwanadi majukwaani wakati wa kampeni za urais wa mwaka jana.
Makongoro ambaye aliwasilisha hoja kwa aina yake akitumia neno 'site' kuwakilisha vijiwe vya wanachama, alisema mwenyekiti alivyowanadi watuhumiwa hao katika uchaguzi wa mwaka jana: “site walihoji sasa ndiyo nini?”
Mpango wa kujivua gamba ulitangazwa na Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM mjini Dodoma, akisema lengo ni kukihuisha chama na kukirejesha katika misingi yake ya TANU na CCM ya mwaka 1977. Chanzo: Gazeti Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Can I simply say what a relief to discover a person
that actually understands what they are discussing on the internet.
You definitely realize how to bring an issue to light
and make it important. More and more people really need to check this out and understand this side of the story.
I can't believe you're not more popular given that
you surely have the gift.
Stop by my weblog masturbation encouragement :
: http://jerkoffencouragement.org ::
Post a Comment