Wednesday, September 28, 2011

Wasioona wapewa nakala 1,500 za Katiba

WIZARA ya Katiba na Sheria imeikabidhi asasi ya Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu (SWAUTI), nakala 1,500 za Katiba zilizochapwa kwa maandishi ya nukta nundu ili washiriki kikamilifu katika mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumza wakati wa kukabidhi nakala hizo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Oliver Mhaiki alisema lengo la kutengeza nakala hizo zenye thamani ya Sh milioni 32 ni kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu ya Katiba.

Mhaiki alisema upatikanaji wa Katiba kwa makundi yote ni muhimu kwa kuwa Katiba ndiyo sheria mama hivyo wananchi wanatakiwa kuifahamu na kuielewa ili washiriki kikamilifu katika kuandaa Katiba mpya baada ya miaka 50 ya Uhuru.

“Katiba hii imechapwa na Kampuni ya Edpar Corporation na gharama ya kutengeneza nakala moja ya Katiba kwa maandishi ya nukta nundu ni Sh 21,000 wakati kwa maandishi ya kawaida ni Sh 3,500, hii ni gharama kubwa ni lazima mzitunze ili ziwanufaishe na wengine,” alisema Katibu Mkuu Mhaiki.

Katibu wa Swauta, Stella Jailos aliishukuru Serikali kwa kupata Katiba hiyo ambayo hawaifahamu toka miaka 50 ya Uhuru na kuwaomba wasiishie hapo, bali wawakumbuke hata katika Katiba mpya.

Alisema, Katiba hiyo itawasaidia kushiriki katika kuandikwa kwa Katiba mpya kwa kuwa wasingeweza kutoa mapendekezo wakati yaliyoandikwa nyuma hawayafahamu na kuahidi kuwa watazisambaza nchini kupitia katika matawi ya asasi yao.

Alisema, kuna baadhi ya sheria zinazowahusu kama wananchi, lakini hawazifahamu na kuiomba Serikali kuzichapa katika maandishi hayo ili wazifahamu ambapo Katibu Mhaiki aliahidi kulishughulikia.

Mwenyekiti wa Swauti, Modesta Mpelembwa alivitaka vyombo vya habari kuweka wakalimani hasa wakati wa shughuli za Bunge zikiendelea ili wapate haki yao ya kupata habari na kuelewa nini kinachoendelea.

No comments: