Na Juma Nyumayo, Dar es Salaam
MIGOGORO ya Ardhi inayoendelea katika mikoa mbalmbali hapa nchini imetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya wanawake katika harakati zao za kujikwamua kiuchumi pia kuleta ukombozi wa mwanamke na maendeleo stahiki hapa nchini.
Hayo yameibuliwa na washiriki wa warsha inayoendelea katika Ukumbbi wa Kitivo cha Uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa uwasilishaji wa mifumo na vikwazo vinavyozuia wanawake kujikwamua kiuchumi.
Akiwasilisha Mada hiyo, Mwezeshaji toka TGNP, Rehema Mwateba alisema ni vyema washiriki wakaeleza hali halisi ya umiliki wa ardhi na migogoro inayendelea kujitokeza hivi sasa ikilinganishwa na mifumo iliyopo katika kumkomboa mwanamke kimapinduzi.
Mshiriki mmojawapo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro,Kibena Kingo, ametolea mfano wa mapigano yanayoibuka marakwa mara na yanayoendelea wilayani kwake kati ya wafugaji na wakulima, ambapo chanzo kikiwa ni matumizi ya Ardhi na kwamba mgogoro huo ni mkubwa.
Imeelezwa wafugaji hao wanaotokea mikoa ya kaskazini na kati wanalishia wanyama wao mazao ya wakulima bila kujali na hivyo kuwakwaza wananchi wewnyeji ambao wengi wao ni wakulima wa mazao ya chakula.
"Mgogoro wa ardhi ni mkubwa na waathirika wakubwa ni wanawake na watoto, hata hivyo ni lazima hatua zichukuliwe ili kutatua migogoro hii kabla hayajatokea mauaji makubwa," alishauri Kingo.
Wakati kingo akielezea mgogoro wa ardhi Morogoro bado Mwezeshaji toka TGNP Darus Badi alipaza sauti yake na kuthibitisha kuwa mtandao huo una rekodi ya migogoro ipatayo 60 ya ardhi katika mkoa huo na kwamba kuna haja ya kulichukulia uzito tatizo hilo.
" Tuna migogoro tunayoijua kule Morogoro na tukiwa kama wanaharakati lazima tushirikiane kuchukua hatua," alisema Badi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa halamashauri ya Mbinga Prisca haule alisema migogoro mingi ya ardhi huko Mbinga imeibuka kutokana na wakazi wa huko kutafuta maeneo ya kulima baada ya kuishiwa ardhi maeneo ya milimani.
"Kuna migogoro ya ardhi katika familia na nje ya familia kupigania ardhi ya kulima," alisema na kubainisha kuwa bado kuna mipango mibovu na sera isiyoeleweka katika umiliki wa ardhi.
Hata hivyo lawama azikuachwa kwa wawekezaji katika vitalu vya mbuga za wanyama hadi migodi ya madini kama ya Buzwagi, Geita hadi huko Namtumbo kwenye Urani( Uranium) ambako wananchi wa kawaida na hasa wanawake wanaona kama mchezo wa kuigiza wasijue kinachoendelea kwenye ardhi yao.
Lawama kibao zimeelekezwa pia kwa Mamlaka za vijiji na Miji kugawa ardhi kwa upendeleo na hasa kwa wale wanaotoa kitu kidogo kwaajili ya kupata viwanja vya makazi na kuwaacha kabisa wanawake nyuma.
Wakati wa Ufunguzi wa warsha hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Jinsia ya TGNP, Dkt. Diana Mwiru, aliwaasa washiriki kujadili mada mbalimbali kwa lengo la kujenga uelewa na kusaidi jamii tunapoelekea kusherehekea tamasha la Jinsia na Mika 50 tangu Tanganyika kupata Uhuru wake.
Dkt. Mwiru,alisema, katika miaka 50 iliyopita wanawake wa nchi hii wameendelea kuachwa nyuma katika kumiliki na utoaji wa maamuzi juu ya rasilimali ikiwa ni pamoja na ardhi.
No comments:
Post a Comment